Nov,18-Siku ya I Kimataifa ya Kuzuia&Kuponya Unyonyaji,Nyanyaso kwa Watoto
Na Angella Rwezaula,– Vatican.
Katika fursa ya Siku ya Kwanza ya Kuzuia na Kuponya nyanyaso za kijinsia kwa watoto, mnamo tarehe 18 Novemba 2022, litafanyika Kongamano lililohamasishwa na Tume ya Ushirikiano ya Kimataifa na Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto. Hii ni kutaka kutimiza kile ambacho hivi karibuni mnamo tarehe 7 Novemba 2022, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa[UN] lilipitisha azimio lililoidhinisha kuwa kila tarehe 18 Novemba ya kila mwaka iwe Siku ya Kimataifa ya Kuzuia na Kuponya Unyanyasaji, Unyonyaji wa Kijinsia kwa Watoto.
Siku hiyo ya Kimataifa ilianzishwa kwa msaada mkubwa wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Kulinda Watoto, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Umoja wa Mataifa na shukrani kwa juhudi ya Mtandao wa Kimataifa wa Ushirikiano ambao unaoongozwa na waathirika ambao unaofanya kazi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, jumuiya za kitawa, serikali na ulimwengu wa wasomi ili kukuza ufahamu wa haja ya kuzuia unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto(CSA) na kuleta utambuzi wa kitaasisi kwa changamoto zinazowakabili waathiriwa na waathirika.
Katika tukio la Siku hiyo ya Kwanza, Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto, pamoja na Mtandao wa Ushirikiano wa Kimataifa, kwa njia hiyo umehamasisha kongamano litakalo fanyika katika Nyumba Kuu la Wajesuti, iliyopo nja ya Borgo Santo Spirito 4, tarehe 18 Novemba 2022. Majadiliano ya Jopo la pande zote mbili yataongozwa na mada, Hatua ambazo Serikali Zinaweza Kuchukua Kuzuia Unyanyasaji wa Kijinsia kwa Watoto. Pamoja na wageni waalikwa katika tukio hilo ni pamoja na hotuba kutoka kwa Mheshimiwa Bi Fatima Maada, Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone na wazungumzaji wengine ni Profesa Marci Hamilton, JD: Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Child Global, na Profesa wa Mazoezi katika Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Pennsylvania Marekani, Thomas Muller, Mkurugenzi, ECPAT International, Cornelius Williams, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto, cha UNICEF, Eirlian Abdul Rahman, FRSA MSc, Prajna Leadership & Julio Frenk DrPH Fellow Harvard T.H. Chan School of Public Health, Mheshimiwa Afra Mohamed Alsaabri, Mkurugenzi Mkuu - Wizara ya Uvumilivu na Ushirikiano Umoja wa Falme za Kiarabu, Sarah Ahmad, Mwenyekiti Ofisi ya Maslahi ya Ulinzi wa Mtoto huko Punjab, Pakistan.