Tanzania:Uzinduzi wa mpango wa kuimarisha uchumi wa wawanake vijijini Zanzibar na bara
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Chakula na Kilimo (FAO), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kushughulikia masuala ya wanawake, (UN Women) tarehe 12 Oktoba 2022 yamezindua programu ya miaka mitano ya kuongeza kasi ya Uwezeshaji wa mradi wa uimarishaji uchumi wa wanawake wa Vijijini. Katika mradi huo unaofadhiliwa na nchi za Norway na Sweden, utakaogharimu dola za Marekani milioni 5, utawanufaisha zaidi ya wanawake 8,000 wa vijijini katika mikoa ya Singida, Dodoma na Zanzibar kwa kusaidia ustawi wao kupitia mnepo katika sekta ya kilimo. FAO inaeleza kuwa nchini Tanzania chakula kinazalishwa na wakulima wadogo, huku wanawake wakichangia nguvu kazi kubwa na kupata asilimia 80% ya mapato yao kutokana na kilimo cha kujikimu. Kwa bahati mbaya, ukosefu wa usawa wa kijinsia unaojikita katika mifumo dume ya kibaguzi na kanuni za kijamii huzuia wanawake kupata huduma za ugani za kilimo, masoko, ardhi na huduma rasmi za kifedha.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Bwana Suleiman Masoud Makame, Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Zanzibar amesema: “usawa wa kijinsia ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Tanzania inatambua hili na imepitisha sera zinazoendeleza usawa wa kijinsia. Kama serikali tunatambua na kuthamini ushirikiano unaoendelea wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kuunga mkono juhudi zetu za kuendeleza usawa wa kijinsia hasa katika sekta ya kilimo. Mpango huu wa pamoja wa FAO, IFAD, WFP na UN Women ni onesho la uungwaji mkono huu unaoendelea.” Kwa niaba ya mashirika ya utekelezaji wa mradi huo, Bi Sarah Gordon-Gibson, Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania amesema: “uzinduzi wa mpango huu wa pamoja umekuja wakati muafaka kwani unakuja wakati sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto lukuki. Ushirikiano kati ya mashirika manne ya Umoja wa Mataifa - FAO, IFAD, WFP na UN Women, unaleta pamoja utaalamu wa wataalamu wa kilimo, maendeleo ya vijijini na jinsia ambayo ni muhimu katika kutatua changamoto na kujenga uwezo wa kustahimili. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Sima Bahous amesema, “ni wazi kuwa wanawake wa vijijini wanakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinaathiri uwezo wao wa kuongeza tija na kipato chao. Tunahitaji kuongeza uungaji mkono wetu sasa na katika siku zijazo ili kusaidia kukabiliana na changamoto hizi na kusaidia njia za wanawake wa vijijini kufikia maendeleo.” Programu hiyo itawajengea uwezo wanawake katika kilimo bora kinachoendana na tabianchi ili kukabiliana na changamoto za majanga ya tabia nchi ambayo yanaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake kutokana na upungufu wa upatikanaji wa rasilimali za kilimo, ukosefu wa mamlaka ya kufanya maamuzi na mikakati dhaifu ya kukabiliana na hali hiyo.
FAO inaeleza kuwa janga la COVID-19 pia liliathiri sekta ya kilimo na mifumo ya chakula ya ndani kupitia ufikiaji wa soko na kuongezeka kwa gharama za pembejeo. Mradi utatoa uendelezaji biashara, mafunzo ya uongozi na upatikanaji wa masoko kwa vikundi vya kujitegemea, kwa kusaidia Vyama vya Akiba na Mikopo vilivyopo na vipya vya Vijiji ili kusajiliwa rasmi na kupata fedha. Mradi huo nchini Tanzania ni sehemu ya awamu ya pili ya programu ya kimataifa inayotekelezwa pia katika nchi za Nepal, Niger, Visiwa vya Pasifiki na Tunisia. Awamu ya kwanza ya programu ilizinduliwa mwaka 2014 nchini Ethiopia, Guatemala, Kyrgyzstan, Liberia, Nepal, Niger na Rwanda.