UVIKO-19 Chanzo Cha Ongezeko la Ugonjwa wa Kifua Kikuu Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO anasema, inakadiriwa kwamba watu milioni 10.6 waliugua ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) katika kipindi cha mwaka 2021, kukiwa na ongezeko la 4.5% kutoka 2020, na watu milioni 1.6 walifariki dunia kutokana na TB pamoja na wagonjwa 187, 000 waliokuwa na maambukizi ya Ugonjwa wa UKIMWI. TB sugu kwa dawa kulingana na taarifa ya WHO uliongezeka kwa 3% kati ya Mwaka 2020 na 2021, na kesi mpya 450,000 za TB sugu (RR-TB) kwa mwaka 2021. Hii ni mara ya kwanza katika miaka mingi kuwepo na ongezeko kubwa la Ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani. Huduma za Ugonjwa wa Kifua kikuu ni kati ya huduma ambazo zimeathiriwa sana kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 katika kipindi cha mwaka 2021. Migogoro ya Vita sehemu mbalimbali za dunia, imepelekea pia wagonjwa wa Kifua Kikuu kushindwa kupata tiba muafaka kwa wakati na hivyo maambukizi kuendelea kusambaa kwa watu wengine zaidi pamoja na ugonjwa wenyewe kuwa sugu kwa tiba inayotolewa.
Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema, jambo la msingi kwa wakati huu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani ni kujenga na kudumisha mahusiano, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa, ili kuweza kujizatiti vyema zaidi dhidi ya vitisho vikali vya kiafya ulimwenguni. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao umepelekea madhara makubwa kwa watu sehemu mbalimbali za dunia. Changamoto kwa sasa ni kuwatambua na kuwapatia tiba muafaka waathirika wa Ugonjwa wa Kifua Kikuu. Idadi ya watu waliogunduliwa hivi karibuni na TB ilipungua kutoka milioni 7.1 katika kipindi cha mwaka 2019 hadi milioni 5.8 katika kipindi cha mwaka 2020. Hii ina maanisha kwamba, kuna idadi kubwa ya watu ambao hawatambuliwa kwamba, wameathirika kutokana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu na hivyo kuanza kusababisha ongezeko la watu wanaofariki dunia kutokana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu. Idadi ya watu wanaopatiwa matibabu ya RR-TB na TB sugu kwa dawa nyingi (MDR-TB) pia imepungua kati ya 2019 na 2020. Idadi iliyoripotiwa ya watu walioanza kutibiwa RR-TB mnamo 2021 ilikuwa 161 746, karibu mmoja tu. katika watatu kati ya wanaohitaji.
Taarifa ya WHO inabainisha kupungua kwa matumizi ya Kimataifa kwa huduma muhimu za TB kutoka dola za Kimarekani bilioni 6 kwa mwaka 2019 hadi dola bilioni 5.4 katika kipindi cha mwaka 2021, ambayo ni chini ya nusu ya lengo la Kimataifa la dola bilioni 13 kila mwaka ifikapo 2022. Kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita, kiasi kikubwa cha fedha iliyotumika katika kipindi cha mwaka 2021 (79%) ilitokana na vyanzo vya ndani. Katika nchi nyingine zenye kipato cha chini na cha kati, ufadhili wa Kimataifa unabakia kuwa muhimu. Chanzo kikuu ni Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund). Serikali ya Marekani ambaye ndiye mchangiaji mkubwa zaidi wa ufadhili wa Global Fund na pia ndiye mfadhili mkubwa anayechangia inachangia takribani asilimia 50% ya ufadhili wa Kimataifa dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu. Kumbe, kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kupata majibu ya haraka dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani, na kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kifua Kikuu unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2023.