Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili 10 Oktoba 2022: Kipaumbele Cha Kwanza: Afya ya Akili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 10 Oktoba inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili na kwa mwaka 2022 inanogeshwa na kauli mbiu ''Fanya afya ya akili na ustawi kwa wote kipaumbele cha kimataifa.'' Afya ya akili maana yake ni hali ya kuwa sawa kiakili na kisaikolojia au kutokuwepo kabisa kwa usumbufu wa akili ya mtu, mfano msongo wa mawazo. Ni hali ya kuwa na mawazo chanya, kuwa sawa kijamii na kisaikolojia na kuweza kuchangia katika utendaji wako wa kila siku na uwezo wa kuridhisha wa kimawazo na kitabia. Huhusisha uwezo wa mtu kufurahia maisha na kutengeneza mlingano baina ya shughuli zako kimaisha pamoja na jitihada zako kufikia uwiano mzuri kisaikolojia, kutoka kwenye msongo utokanao na magonjwa, misiba na shida mbalimbali. Afya ya akili pia ni uwezo wa mtu kuishi katika mabadiliko mbalimbali ya kimaisha na kufanyia kazi changamoto zinazoibuka kila kukicha. Uwezo wa mtu kuwa timamu kiakili huhusisha mtu kuweza kutatua matatizo mbalimbal yanayomkabili yahusishayo msongo wa mawazo katika maisha, shuguli za uzalishaji na mchango wa mtu husika katika jamii. Afya ya akili huhusisha...” ustawi wa akili, kujitambua kwa ufanisi, uhuru, umahiri, utegemezi wa ulimwengu, na kujitambua kwa uwezo wa kiakili na kihemko, kati ya wengine.”
Ustawi wa mtu ni uwezo wa kukabiliana na matatizo na changamoto za kawaida za maisha, kazi yenye tija na mchango kwa jamii yao. Tofauti za kitamaduni, tathmini ya kujifanya, na nadharia za kitaalam zinazoshindana zote zinaathiri jinsi mtu anafafanua “afya ya akili.” Wataalam wanasema, watu wenye afya bora ya akili wanaweza pia kuwa na magonjwa ya akili, na watu ambao hawana ugonjwa wa akili pia wanaweza kuwa na afya mbaya ya kiakili. Siku ya Afya ya Akili Duniani ni Siku ya Kimataifa maalumu kwa kutoa elimu ya masuala ya afya ya akili; uhamasishaji na utetezi dhidi ya unyanyapaa wa kijamii pamoja na athari zake kwa wale walioathirika na Walezi wao. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kwamba kabla ya kuibuka kwa Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 takriban mtu 1 kati ya 8 Duniani kote walikumbwa na matatizo ya kiakili, hata hivyo msaada makini wa miundombinu na kiuchumi kwa ajili yao, ulikosekana. Matatizo ya afya ya akili yapo katika maisha ya watu, familia, sehemu za kazi na jamii, na athari zake zinajionesha kwa watu wengi katika jamii.
Dalili za matatizo na changamoto ya afya ya akili ni pamoja na: Kuwa na hasira kupindukia. Kukosa furaha na kutokuona thamani katika maisha, hali inayopelekea mtu kuwa na upweke hasi. Kuwa na wasiwasi wa kupindukia, kiasi hata cha kujaribu kutema zawadi ya maisha. Hali ya kukosa usingizi. Kuwa na msongo mkali wa mawazo kiasi hata cha kushindwa kufanya maamuzi. Ni muhimu kwa jamii kufanya utafiti wa kutosha ili kuzuia magonjwa ya akili: kama watu binafsi na kama jamii na kama Jumuiya ya Kimataifa. Jamii, familia na watu binafsi wajitahidi kuwa karibu zaidi na watu wenye dalili za afya mbaya ya akili, ili kujaribu kuokoa maisha yao. Wajitahidi kuzungumza nao kuhusu hisia na changamoto wanazopitia pamoja na kumjulia hali mara kwa mara. Kama kuna dalili za hatari jamii inashauriwa kuwasiliana na kitengo cha dharura kilichoko karibu naye. Ili kulinda afya ya akili na mwili kwa ujumla. Watu wanashauriwa sivute sigara, wahakikishe kwamba, wanapata nafasi ya kulala vyema, wapende na kuthamini sana kinga, kuliko falsafa ya kuponya magonjwa. Watu wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, sanjari na kuzingatia lishe bora na mwishoni kujipatia maji safi na salama. Watu wasifiche hisia zao, waoneshe upendo na ukarimu kwa jirani zao. Waepuke matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na mitandao ya kijamii.
Shirika la Afya Duniani, WHO linasema, kuna haja ya kuendelea kutoa wito kwa serikali za kitaifa na za mitaa kuweka kipaumbele katika kupunguza mambo yanayojulikana kuwa hatari kwa afya ya akili ya watu: kama vile ukata na ugumu wa maisha, migogoro ya kijamii na kimapenzi na jambo hili linaanza kuchukua kasi ya ajabu kwa jamii nyingi. Unyanyapaa kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na dhana au Mila potofu katika jamii. Pia kuna haja ya kuwaimarisha wale wote wanaoshughulika: kulinda afya za akili kuanzia mtu mmoja mmoja hadi mashirika binafsi na kuunda nyenzo zinazohitajika kwa watu kustawi na kuneemeka. Siku ya Afya ya Akili Duniani ni nafasi ya kuzungumza kuhusu afya ya akili kwa ujumla, jinsi binadamu anavyohitaji kuitunza, na jinsi ilivyo muhimu kuzungumza kuhusu watu wanavyojisikia, ili hatimaye kupata msaada ili kumaliza tatizo na changamoto za kiafya. Uchunguzi unaonesha kwamba, waathirika wakuu wa afya ya akili ni wanaume. Vyanzo vya magonjwa ya afya ya akili vinaweza kuwa ni vya kibaiolojia, kwa kurithi au kushikwa na magonjwa mbalimbali. Kisaikolojia: baadhi ya visababishi ni malezi, familia tenge, ugumu wa maisha na kuondokewa na watu wa karubu sana katika maisha. Kijamii inakuwa ni changamoto za kiuchumi, matatizo ya ndoa na familia pamoja na upweke hasi.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, takribani watu bilioni 1 duniani kote wanaishi na matatizo ya akili. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kwa siku hii amesema, inabidi hatua zichukuliwe ili kuhakikisha kunakuwa na huduma bora ya afya ya akili kwa wote Mammbo ya kuzingatia ili kuboresha afya ya akili: Wakati wa changamoto na hali ngumu zaidi maishani, una uwezo wa kushughulikia chochote kinachokujia na kufanikiwa kupitia kila hali au hali. Kuwafikia wengine kuomba msaada sio udhaifu na katika jamii ambayo watu wengi hawapendi kuomba msaada, kuomba msaada ni ishara ya nguvu na ujasiri. Ushujaa unatokana na njia ambazo tunajifunza kufikiria na kutenda tunapokabiliwa na vizuizi. Tunaposaidia kukuza njia ya maisha inayoona vizuizi kama sehemu muhimu ya mafanikio, tunasaidia watu kukuza ujuzi wa kukabiliana na kujenga uthabiti. Kuunganishwa kwa kijamii kunaboresha ustawi wa mwili, kiakili, na kihemko. Mafungamano ya kijamii huongeza hali ya mtu kuwa mali na hazina muhimu; hukuza hisia za thamani ya kibinafsi, hutoa ufikiaji wa vyanzo vya msaada, na hupunguza hatari ya mtu kutema zawadi ya maisha.