Ripoti mpya ya UNDP:kila mtu anakumbwa na umaskini kwa njia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tarehe 17 Oktoba 2022 Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo Duniani, UNDP limetoa ripoti yake kuhusu hali ya umaskini duniani ambapo imeibuka na mbinu mpya ya kupima kiwango cha umaskini badala ya kutumia kiwango cha kipato anachopata mtu, kaya au taifa kwa sababu kila mtu anakumbwa na umaskini kwa njia tofauti tofauti. Taarifa ya UNDP iliyotolewa jijini New York, Marekani imesema kipimo hicho MPI kikitumia vigezo mbalimbali zaidi ya kipato kinaweza kuwa muarobaini wa kukabiliana na umaskini duniani hasa kushughulikia vigezo vinavyoingiliana ambavyo vinasababisha umaskini. UNDP kwa kushirikiana na mpango wa maendeleo wa Chuo Kikuu cha Oxford, OPHI walifanya utafiti uliomulika masuala kadhaa zaidi ya kipato cha mtu ili kuelewa ni kwa vipi watu wanakabiliwa na umaskini katika maisha yao ya kila siku, kuanzia kupata huduma ya elimu na afya hadi kiwango cha maisha kama vile makazi, maji ya kunywa, huduma za kujisafi na umeme.
Ripoti imebaini ‘mafungu ya kukoseshwa’ au watu kunyimwa haki zao za msingi, yanayochochea mwenendo unaojirudia wa umaskini ambao unaathiri wale wanaoishi katika mazingira mbalimbali ya umaskini duniani kote. Kila mtu anahisi au anakumbwa na umaskini kwa njia tofauti tofauti. Kwa mfano huko nchini Laos, “familia ambazo hazina uwezo wa kupata nishati mara nyingin zinashindwa kupeleka watoto wao shuleni kwa sababu watoto hao wanatakiwa kwenda kuchanja kuni kila siku,” amesema hayo Tasneem Mirza mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo kutoka UNDP. Kwa kuzingatia takwimu za ripoti hii ambazo zimekusanywa kabla ya kuanza kwa UVIKO -19, ripoti imemulika umuhimu wa kushughulikia mlolongo wa mafungu ya kukosa ambayo yanakwenda pamoja, ikiwemo: Zaidi ya 50% ya watu maskini duniani sawa na watu milioni 593, hawana umeme na nishati ya kupikia na Takribani 40% ya watu maskini duniani, sawa na watu milioni 437 hawana maji safi na salama na huduma za kujisafi.
Kwa maana hiyo UNDP inasema takwimu hizi zinatumika kubaini aina za umaskini ambao umetapakaa maeneo mengi. Hii ni hatua muhimu katika kuunda mikakati ya kushughulikia aina mbalimbali za umaskini kwa wakati mmoja. Ripoti inasema hata kabla ya COVID-19 na janga la sasa la hali ya gharama za maisha, watu bilioni 1.2 katika nchi 111 zinazoendelea wanaishi katika umaskini uliokithiri ukiwa na mlolongo wa vigezo tofauti tofauti. Hii ni mara mbili ya idadi ya watu ambao wanaainishwa kuwa ni maskini kwa kuwa wanaishi kwa kutumia chini ya dola 1.90 kwa siku. Mfano mwingine watu milioni 595 wanaishi kwenye kaya ambazo hakuna hata mwanafamilia mmoja amehitimu miaka 6 ya kujifunza shuleni.
Mkuu wa UNDP, bwana Achim Steiner akizungumzia ripoti hiyo alisema “wingu zito la mdororo wa kiuchumi likionekana kutanda na madeni yakighubika nchi 54 zinazoendelea, tunaona ni kwa vipi serikali zinazidi kubana bajeti zao. Ni muhimu kutumia takwimu hizi za kuleta majawabu ili kuelewa tofauti kubwa inayoweza kupatikana wakati huu ambapo rasilimali zinaendelea kupungua.” Ametolea mfano ni kwa vipi uchambuzi huu mpana wa MPI unaonesha jinsi kuondokana na matumizi ya nishati zinazoharibu mazingira na kupanua wigo wa nishati salama kunaweza kusongesha hatua kwa tabianchi na kunusuru watu milioni 600 walio maskini kupindukia kutokana na kukosa nishati salama ya umeme pamoja na nishati salama ya kupikia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 83 ya watu wenye umaskini uliojikita katika maeneo mbalimbali wako nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, idadi ambayo ni sawa na watu milioni 579 huku wengine milioni 385 wako nchi za Kusini mwa Asia. Theluthi mbili ya watu maskini wako katika nchi za kipato cha kati na asilimia 83 wako vijijini. Ikichambua kwa nchi, ripoti inasema duniani kote, India inaongoza kwa kuwa na watu maskini duniani idadi ikiwa ni watu milioni 229 ikifuatiwa na Nigeria yenye watu maskini milioni 97. Bwana Steiner anatamatisha akisema, kipimo hiki cha MPI ni muhimu katika kusambaza juhudi za UNDP duniani kote tunaposhirikiana na wadau wetu kutoka Umoja wa Mataifa na kwingineko kufikia lengo letu la kusaidia kuondoa katika lindi la umaskini watu milioni 100 ifikapo mwaka 2023.