Mahakama ya Juu: Dr. William Samoe Ruto Ndiye Mshindi Uchaguzi Mkuu 2022 Kenya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mahakama ya Juu Nchini Kenya, tarehe 5 Septemba 2022 imethibitisha kwamba, Dr. William Samoei Ruto kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu nchini Kenya uliofanyika 9 Agosti 2022. Mahakama ya Juu imebaini kwamba Rais mteule alikuwa ameshinda zaidi ya asilimia 50% ya kura zote halali ziliziopigwa kama inavyooneshwa kwenye Katiba ya Kenya. Mahakama ikapima kama kulikuwa na ukiukwaji wa wa kanuni za uchaguzi wa kutosha kiasi cha kubatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu. Walichogundua ni kwamba, ukiukwaji ulikuwepo lakini si kiasi cha kubatilisha matokeo. Itakumbukwa kwamba, Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, tarehe 15 Agosti 2022 imemtangaza mgombea wa Kenya Kwanza, Dr. William Samoei Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya. Ruto ambaye alikuwa ni Makamu wa Rais wa Kenya, alishinda uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali kati yake na mgombea wa Azimio la Umoja, Raila Odinga aliyekuwa akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. William Samoei Ruto alijipatia wastani wa asilimia 50.49 %. Raila Odinga 48.85 %. David Waihiga 0.23 % na George Wajackoyah 0. 44.
Wakati huo huo, Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kwamba Alhamisi, tarehe 8 Septemba 2022 ni tarehe ya kuanza vikao vya Wabunge wa Bunge la Kitaifa na Seneti, ambao wataapishwa siku hiyo hiyo! "Mimi, Uhuru Kenyatta, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Ulinzi wa Kenya, ninateua kwamba Mkutano wa Kwanza wa Bunge la Kitaifa na Seneti utafanyika katika Majengo makuu ya Bunge," alisema kwenye Notisi ya Gazeti Nambari 10527. Bunge hilo litakuwa na wajumbe 349 wakiwemo Wawakilishi Wanawake 47 na Wabunge 12 wa Kuteuliwa. Seneti, kwa upande mwingine, itakuwa na Maseneta 67, wakiwemo Maseneta 20 Waliopendekezwa. Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, Rais anapaswa kutangaza kikao cha kwanza cha Bunge Jipya kupitia taarifa ya Gazeti la Serikali ndani ya Siku 30 baada ya uchaguzi kuhitimishwa.