Tafuta

Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, tarehe 15 Agosti 2022 imemtangaza mgombea wa Kenya Kwanza, Dr. William Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, tarehe 15 Agosti 2022 imemtangaza mgombea wa Kenya Kwanza, Dr. William Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya  (AFP or licensors)

Uchaguzi Mkuu Kenya 2022: Vipaumbele vya Rais William Ruto

Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, tarehe 15 Agosti 2022 imemtangaza mgombea wa Kenya Kwanza, Dr. William Samoei Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya. Ruto ambaye ni Makamu wa Rais wa Kenya, ameshinda uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali kati yake na mgombea wa Azimio la Umoja, Raila Odinga aliyekuwa akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 9 Agosti 2022, kulifanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya. Wapiga kura walimchagua Rais, Wabunge wa Bunge la Kitaifa na wajumbe wa Baraza la Seneti; Magavana wa kaunti na wajumbe wa mabunge 47 ya kaunti. Uchaguzi mkuu nchini Kenya hufanyika kila baada ya miaka mitano. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kulikuwepo na mchuano mkali, “patashika nguo kuchanika” hasa kutoka kwa wagombea wakuu wawili ambao ni Raila Odinga wa Muungano wa Azimio One Kenya na Makamu wa Rais William Samoei Ruto wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA). Wengine walioshiriki katika uchaguzi huu ni David Mwaure Waihiga wa Chama cha Agano na George Wajackoyah wa Chama cha Roots. Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, tarehe 15 Agosti 2022 imemtangaza mgombea wa Kenya Kwanza, Dr. William Samoei Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya. Ruto ambaye ni Makamu wa Rais wa Kenya, ameshinda uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali kati yake na mgombea wa Azimio la Umoja, Raila Odinga aliyekuwa akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. William Samoei Ruto amejipatia wastani wa asilimia 50.49 %. Raila Odinga 48.85 %. David Waihiga 0.23 % na George Wajackoyah 0. 44.

Raila Odinga amepata asilimia 48.85 ya kura halali zilizopigwa.
Raila Odinga amepata asilimia 48.85 ya kura halali zilizopigwa.

 

Hata hivyo zoezi hilo limekumbwa na utata baada ya makamishna wane kati ya saba wa tume ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC kutangaza kutotambua matokeo ya uchaguzi wa rais wakidai kuwa mchakato huo umekosa uwazi katika hatua za mwisho. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, linawaalika waamini na watu wote wa Mungu nchini Kenya katika ujumla wao, kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Maaskofu wanawataka wananchi kuwa macho na habari za kughushi ili wasitumbukie katika vurugu, ghasia na fujo. Wawe watulivu baada ya kutangaziwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 9 Agosti 2022 na kwamba, jambo la msingi ni ushiriki mkamilifu katika mchakato wa ujenzi wa demokrasia ya kweli. Watu wa Mungu nchini Kenya wajivunie uzalendo wao, tayari kushikamana kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao unaosimikwa katika amani na utulivu. Vijana wawe waangalifu na kamwe wasitumiwe na wanasiasa kuvuruga amani na utulivu nchini Kenya.

Ilani ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) inazingatia ujenzi wa uchumi thabiti, kuimarisha elimu, afya, teknolojia, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na sekta ya kilimo. Ruto amesema kwamba changamoto zinazoikumba Kenya kwa sasa zinastahili kushughulikiwa kwa haraka sana na kwamba lengo lake kubwa ni kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo, ambao unaendelea kupambana na athari za maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Anapania kuimarisha ukuaji wa uchumi kwa kumhusisha kila Mkenya katika ujenzi wa taifa lake. Uchumi unaokua kwa kuzingatia zaidi watu wa kipato cha chini. Kulingana na Ruto, mfumo wa uchumi kutoka kwa watu wenye kipato cha juu ukishuka hadi kwa watu wenye kipato cha chini haufai, na kwamba mfumo bora ni kuwaangalia zaidi watu wenye kipato cha chini ambao idadi yao ni kubwa sana nchini Kenya ikilinganishwa na wenye kipato cha juu. Kila mwananchi wa Kenya apate mahitaji yake msingi.

Vurugu zimeanza kujitokeza nchini Kenya baada ya matokeo kutangazwa.
Vurugu zimeanza kujitokeza nchini Kenya baada ya matokeo kutangazwa.

Maendeleo kutoka mashinani: Dr. William Samoei Ruto amesema kwamba mfumo wa ukuaji wa uchumi unaozingatia sana watu wenye kipato cha chini, ambao umejulikana sana kenya kwa lugha ya kiingereza ‘Bottom up’, utatekelezwa kutoka kwa serikali za kaunti 47 za Kenya. Kaunti zote zitazingatia sekta muhimu za kilimo, upatikanaji wa chakula, ukuaji wa biashara ndogondogo, ujenzi wa nyumba bora, afya, teknolojia na ubunifu. Utawala wa Ruto unatarajia kusimamia yafuatayo: Kulinda katiba ya Kenya ambayo kimsingi ni Sheria mama; kubuni mazingira ya ajira kwa Wakenya, kufufua uchumi, kuboresha utendakazi wa Idara ya Mahakama, kuimarisha kiwango cha elimu, kuboresha mfumo wa afya, kuwateua majaji wote walioachwa nje na Rais Uhuru Kenyatta ndani ya siku saba. Ameahidi kuanzisha Mfuko Maalum wa Fedha kufadhili biashara ndogondogo zinazoongozwa na wanawake na vijana, pamoja na kuunda fursa za kazi katika sekta ya kilimo.

Nafasi za vijana na wanawake serikalini: Ameahidi kwamba, walau asilimia 50% ya wanawake katika Baraza lake la mawaziri huku akiahidi kuwa nyadhifa za uteuzi katika sekta ya umma zitazingatia kanuni ya theluthi mbili ya jinsia. "Vijana wetu na wanawake, ndio nguzo ya mpango wetu. Tumeweka ahadi na vijana wa nchi hii kwamba tutaunda wizara maalum kwa ajili ya vijana. Tutakuwa na msahauri mku katika ofisi ya Rais kuhakikisha kwamba mipango yote ya serikali inawashirikisha vijana. Kama muungano wa Kenya kwanza, tumekubaliana kwamba asilimia 50 ya Baraza la Mawaziri itakuwa wanawake. Tumekubaliana kwamba vijana na wanawake watanufaika zaidi na mfuko maalum wa kuinua biashara ndogondogo."

Maaskofu wanawataka wananchi kudumisha amani na utulivu.
Maaskofu wanawataka wananchi kudumisha amani na utulivu.

Ahadi kuu za Rais mteule William Samoei Ruto kwa Wakenya: Kutenga shilingi bilioni 259 kwa ajili ya kuimarisha kilimo na kuhakikisha kuna chakula cha kutosha. Kujenga nyumba 250,000 za gharama nafuu kila mwaka kwa ushirikiano na sekta binafsi. Kila mkenya kuwa na bima ya afya. Shilingi bilioni 50 kila mwaka kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo na ambao watapata mikopo kwa njia rahisi. Kuweka mfumo maalum wa kifedha kwa ajili ya kutoa makazi kwa watu milioni moja wasiokuwa na ardhi. Kuajiri wadaktari na wafanyakazi wa afya 20,000. Kuajiri walimu zaidi wanaohitajika ili kuziba pengo lililopo kwa wakati huu. Kukamilisha ujenzi wa barabara zote ambazo zinajengwa kwa sasa. Kujenga kilomita 100,000 za mfumo wa internet yaani “fibre optic.” Ili kuimarisha uhuru wa mahakama, Ruto vile vile anaahidi kuwezesha idara ya mahakama kujitegemea na kuendesha shughuli zake bila kutegemea ofisi ya Rais. Kuhusu elimu, Ruto ameahidi kupunguza pengo la sasa la upungufu wa walimu 116,000 ndani ya miaka miwili ya fedha, kukagua mfumo wa sasa unaoegemea mitihani wa kuendelea na masomo, ambao anasema haujajumulisha mamilioni ya wanafunzi kulingana na mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, kwa kutekeleza njia mbadala vigezo vya kuingia. "Sekta yetu ya elimu inakumbana na changamoto chungu nzima hasa elimu ya juu. Hakuna ufadhili wa kutosha." Alisema.

Uchaguzi Kenya
16 August 2022, 15:37