Sensa ya Watu na Makazi Nchini Tanzania 2022: Changamoto Zake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini Tanzania ni ile ya mwaka 2012. Hivyo Sensa ya mwaka 2022 ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anakiri kwamba, Sensa ya Watu na Makazi 2022 ni zoezi linalokabiliwa na changamoto za kimila, na desturi ndani ya jamii za kitanzania wanaoamini kwamba kuhesabiwa ni balaa na nuksi. Serikali isingependa kusikia asilimia ya watu haikuhesabiwa. Watu wanahesabiwa kwa ajili ya huduma ya kiuchumi na maendeleo. Hakuna sababu iliyojificha nyuma ya pazia. Serikali haiwezi kupanga mipango ya maendeleo bila ya takwimu sahihi za watu na makazi. Hili ni zoezi linalodumu kwa muda wa siku saba, kumbe, wananchi waendelee kutoa ushirikiano. Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, misimamo mikali ya kiimani na kidini; imani za uchawi na ushirikina ni kikwazo kikubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watanzania wanahimizwa kujitokeza ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania kwa mwaka 2022.
Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., wa Jimbo Katoliki Morogoro ameishauri Serikali kuhakikisha kwamba, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zinasaidia kuboresha maisha na huduma za watanzania vijijini, ili wasikate tamaa na kutokuona umuhimu wa kushiriki matukio makubwa kama haya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Wale walioteuliwa na Serikali kushiriki mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi watekeleze wajibu huu kwa nidhamu, taratibu, kanuni na sheria, ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Kwa upande wake, Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, anawahimiza watanzania kushiriki kikamilifu katika zoezi kwa kuzingatia ukweli na uwazi na kamwe wasiwafiche watoto wenye ulemavu, ili Seikali iweze kutambua mahitaji yao na kuwasaidia kwa wakati muafaka.
Maana ya Sensa ya Watu na Makazi. Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. Takwimu hizi za msingi ndizo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo. Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na: Kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa. Taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali za nchi. Taarifa za msingi za hali ya kidemografia yaani idadi ya watu, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote;
Ni kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi; Taarifa itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira; na Msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia. Takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa. Madodoso ya Sensa: Sensa ya mwaka 2022 kama zilivyo sensa zilizopita inatumia aina mbili kuu za madodoso. Dodoso refu linalotumika kuhoji asilimia 30 ya maeneo yote ya kuhesabia watu na Dodoso fupi linalotumika kuhoji kwenye asilimia 70 ya maeneo yote ya kuhesabia watu. Madodoso Mengine ni: Dodoso la Taasisi ambalo ni mahsusi kwa ajili ya wasafiri, waliolala mahotelini/nyumba za wageni, na waliolazwa hospitalini; na Dodoso la Wasio na Makazi maalum ambalo ni mahsusi kwa watu wote wanaolala maeneo yasiyo rasmi, kwenye baraza za majengo mbalimbali, kwenye madaraja na maeneo mengine. Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022. Utekelezaji wa sensa ya watu na makazi hufanyika katika awamu kuu tatu ambazo ni Kipindi Kabla ya Kuhesabu Watu, Wakati wa Kuhesabu Watu na Kipindi Baada ya Kuhesabu Watu.
Kipindi Kabla ya Kuhesabu Watu: Kipindi kabla ya kuhesabu watu kinajumuisha Uandaaji wa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sensa na nyaraka nyingine, Utengaji wa Maeneo ya Kuhesabia Watu na Uzalishaji wa Ramani, Uandaaji wa Nyenzo (Madodoso na Miongozo mbalimbali); Uhamasishaji, Sensa ya Majaribio Kuunda kamati za sensa; kufanya mikutano na wadau wa takwimu; kufanya manunuzi, kufanya uchaguzi wa aina ya teknolojia itakayotumika, kuajiri wadadisi na wasimamizi, usambazaji wa vifaa; na kufanya maandalizi ya Tathmini ya Sensa. Kipindi cha Kuhesabu Watu. Kipindi cha kuhesabu watu kinajumuisha kazi kuu na ya muhimu katika zoezi hili la kuhesabu watu. Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zitawasaidia wafanyabiashara kutathmini uwezo wao wa kibiashara au uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji. “Wafanyabishara wakubwa kwa wadogo hutumia takwimu za sensa kutathmini uwezo wa kibiashara wa makampuni, uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji na kupitia takwimu za sensa, menejimenti na bodi za makampuni ya biashara na taasisi za uwekezaji za ndani na nje hupata uhakika wa kitakwimu ambao huwaongezea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati,” amesema.
Ametoa kauli hiyo Jumatatu, Agosti 15, 2022 wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi juu ya umuhimu wa ushiriki wao kwenye Sensa ya Watu na Makazi inayofanyika nchini Tanzania kuanzia Agosti 23, 2022 kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Amesema wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wanategemea takwimu za sensa kufanya maamuzi ya uwekezaji ikiwemo huduma mbalimbali kama maduka makubwa, upanuzi wa shughuli zao kama maghala ya kuhifadhia na kusambazia bidhaa, maeneo bora ya kutangaza biashara zao, masoko mapya na kubuni bidhaa mpya pamoja na aina ya huduma kama za hospitali, sehemu za starehe na sehemu za kufanyia mazoezi. Amemshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia, kuthamini na kutilia mkazo mkubwa masuala ya takwimu na kuruhusu mwaka huu Tanzania ifanye Sensa kwa mujibu wa Miongozo ya Umoja wa Mataifa. “Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuridhia kutekeleza sensa ya sita mwaka huu kinaonesha uimara wa uongozi wa Kiongozi wetu na utekelezaji wa takwa hili ni kwa faida ya nchi yetu na ulimwengu kwa jumla.” “Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu kwa kuwa moja ya mikakati ya kiuchumi ya Tanzania ni kuvutia uwekezaji na kuboresha kiwango cha maisha cha wananchi wake. Uwepo wa takwimu bora za Sensa ya Watu na Makazi utasaidia kuharakisha utekelezaji wa mikakati hiyo,” amesema Waziri Mkuu. Akizungumzia umuhimu wa sensa kwa wafanyabiashara Waziri Mkuu amesema: “Kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara, sensa ni chanzo cha msingi cha taarifa za kidemografia na ukuaji wa soko la bidhaa na huduma katika nchi zote duniani.
Takwimu zote za biashara zinahitaji takwimu za idadi ya watu kama kigezo cha msingi cha kufanya maamuzi ya uwekezaji, uzalishaji na biashara.” Ametoa pongezi pia kwa vyombo vya habari kwa ushiriki wao mkubwa katika kutoa hamasa kwa jamii na kuwaelezea umuhimu wa sensa ikiwemo kuwajulisha kuwa sensa hiyo itafanyika lini. Amesema utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Julai mwaka 2022 ulionesha kuwa asilimia 98 ya Watanzania wanatambua uwepo wa sensa “Kitendo cha kuwaonesha wananchi nini kitaulizwa, kimesaidia kuwaandaa wananchi kuhusu zoezi hili. Wasanii mbalimbali nchini wametoa elimu kwa kiwango kikubwa, viongozi wa dini nao wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuwaandaa wananchi, ninawashukuru sana.” Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau hao, Waziri wa Nchi (OWM-SBU), Bw. George Simbachawene alisema mpaka sasa maandalizi ya zoezi la sensa yamefikia asilimia 95. “Asilimia hii tano iliyobakia tusiidharau. Kulingana na muda uliobaki, mimi pamoja na wenzangu tutajitahidi ili tufike kwenye ufanisi unaotarajiwa wa asilimia 100,” alisema. Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Paul Makanza alisema wameshirikiana na Serikali katika vikao kadhaa na kuainisha maeneo saba ambayo wanaweza kuunga mkono. Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni utoaji wa huduma, vifaa, utoaji elimu, usafiri, usafirishaji wa vifaa, utoaji wa matangazo na kuchangia mafuta ya magari. Alisema baadhi ya kampuni za simu zilianza kurusha jumbe fupifupi kwa wateja wao, vituo vya Redio na Televisheni navyo vilianza matangazo kuhamasisha jamii.