Tafuta

Mzee Augustino Lyatonga Mrema Mwenyekiti wa Chama Cha Upinzani cha TLP; Mzalendo na mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania amefariki dunia Jumapili tarehe 21 Agosti 2022. Mzee Augustino Lyatonga Mrema Mwenyekiti wa Chama Cha Upinzani cha TLP; Mzalendo na mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania amefariki dunia Jumapili tarehe 21 Agosti 2022. 

Mzee Augustino Lyatonga Mrema: 31 Desemba 1944-21 Agosti 2022

Mrema aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kati ya mwaka 1990-1994, Waziri wa kazi, maendeleo na michezo kati ya mwaka 1994-1995, Mbunge na Mwenyekiti wa Bodi ya Parole amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77. Mzee Mrema atakumbukwa na watanzania kwa mchango wake mkubwa katika mchakato wa mageuzi ya makubwa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzee Augustino Lyatonga Mrema Mwenyekiti wa Chama Cha Upinzani cha "Tanzania Tanzania Labour Party," TLP; Mzalendo na mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania amefariki dunia Jumapili tarehe 21 Agosti 2022, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, MNH, iliyoko jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa tangu 16 Agosti 2022 kadiri ya taarifa za msemaji wa Hospitali ya Muhimbili Aminieli Eligaisha. Mrema aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kati ya mwaka 1990-1994, Waziri wa kazi, maendeleo na michezo kati ya mwaka 1994-1995, Mbunge na Mwenyekiti wa Bodi ya Parole amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77. Mzee Augustino Lyatonga Mrema atakumbukwa na watanzania kwa mchango wake mkubwa katika mchakato wa mageuzi ya makubwa ya siasa nchini Tanzania kutoka katika mfumo wa chama kimoja cha siasa kuingia mfumo wa vyama vingo vya kisiasa. Mrema akaonesha upendo na uzalendo kwa nchi yake ya Tanzania. Ni kiongozi aliyesimama kidete kuhakikisha kwamba: utu, heshima na haki msingi za wanawake zinalindwa na kutekelezwa na wote. Kama binadamu, bila shaka atakuwa na mapungufu yake, ndiyo maana waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanamwombea raha ya milele na mwanga wa milele, ili aweze kuangaziwa na apumzike mbinguni.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewakumbusha watanzania kwamba, hivi karibuniTanzania imetimiza miaka 30 tangu irejee rasmi katika siasa za mfumo wa vyama vingi katika kipindi hicho, Tanzania limepitia kipindi cha furaha, majonzi, misukusuko na changamoto zote wakati Taifa lilipokuwa linaanza njia mpya. Jambo hili si jepesi, kwa sababu nyakati hizo hazikuwa rahisi duniani kote. Miaka ambayo Tanzania ilirejea katika mfumo huo ilikuwa migumu. Miaka ya mwanzoni ya 1990, ndiyo ilishuhudia changamoto kama vile kuanguka kwa iliyokuwa Urusi, vita vya wenyewe kwa wenyewe Barani Afrika, mauaji ya Kimbari na migogoro mingi ya kisiasa na kiuchumi katika nchi zinazoendelea kama Tanzania. Lakini Watanzania walipita wakati wote huo, wakiwa wamoja na wameendeleza utamaduni huo miaka 30 baadaye. Rais Samia Suluhu Hassan alipenda kutumia nafasi hii kuwapongeza wote, na ni matumaini yake makubwa, kwamba viongozi watakaokuja miaka 50 hadi 100 baadaye wataendelea kuongoza nchi iliyo moja na wananchi wasiobaguana na kupigana, hata kama wanapingana kuhusu namna ya kuendesha nchi yao. Hata hivyo, yatakuwa makosa makubwa kama watanzania wataona kuwa kazi ile imemalizika. Ana amini, sasa Tanzania inapita katika mazingira yale yale magumu yaliyokuwapo wakati wanaanza mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Viongozi wa vyama vya kisiasa wavuke changamoto watanzania wakiwa wamoja
Viongozi wa vyama vya kisiasa wavuke changamoto watanzania wakiwa wamoja

Kuna vita katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwamo kwenye nchi zilizoendelea, mfumo wa kidemokrasia wa kiliberali unapitia katika changamoto na nchi kubwa zinapambana kuwania kutawala Dunia. Ni changamoto ambazo Viongozi wa kizazi chetu wanatakiwa kuzivuka kama walivyofanya watangulizi wake. Ndiyo sababu kwenye uongozi wake, ana amini katika kile kinachojulikana kama 4R - ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya lugha ya Kiingereza; Reconciliation (Maridhiano), Resiliency (Ustahamilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya). Itakumbukwa kwamba, Mzee Augustino Lyatonga Mrema alizaliwa tarehe 31 Desemba 1944 kwenye Kijiji cha Kiraracha, Marangu. Alijiunga na masomo ya shule ya msingi kati yam waka 1955 hadi mwaka 1963, Wilayani Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Baadaye alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Patrick, Jimbo Katoliki la Moshi kuhitimu masomo yake mwaka 1965. Mwaka 1970 alijiunga na Chuo cha Siasa Kivukoni. Kati ya Mwaka 1980 hadi mwaka 1981 alikwenda Bulgaria kwa masomo zaidi na hatimaye, kutunukiwa Diploma ya Sayansi ya Ustawi wa jamii na utawala bora. Mwaka 2003 alitumwa kwenda Chuo Kikuu cha Pacific na huko akatunukiwa Shahada ya Sanaa katika Sayansi Jamii. Mzee Augustino Lyatonga Mrema amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia mwaka 1990, na wakati huohuo mwaka 1993 hadi 1994 aliteuliwa tena kuwa Naibu Waziri Mkuu, cheo ambacho hata hivyo hakikuwepo kwenye Katiba ya nchi ambayo kimsingi ndiyo Sheria Mama. Kumbukumbu zinaonesha kwamba, alipewa cheo hiki ili kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma nchini Tanzania.

Mzee Mrema alipambana sana na rushwa nchini Tanzania
Mzee Mrema alipambana sana na rushwa nchini Tanzania

Hapa anakumbukwa na wengi, kwa kutatua migogoro kwa kipindi cha siku saba au vinginevyo kukiona kilicho mnyoa Kanga manyoya, utendaji uliopelekea kupewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu. Alikuwa mcheshi na mjenga hoja mzuri. Anakumbukwa sana na watu wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwa kupambana sana na utengenezaji sanjari na matumizi ya pombe haramu ya gongo iliyokuwa inadhohofisha maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Gongo, pombe haramu inajulikana sana kama “Machozi ya Simba”, “Kabhurugutu”, “Tuttion” na “Mabomoke” kwani ilikuwa inanywewa kwa kificho kwenye magofu! Ilikuwa ni ngumu kuwashawishi wananchi wa Kanda ya Ziwa kumpigia kura ya Urais Mzee Augustino Lyatonga Mrema wakati wa pambano lake na Mzee Benjamin William Mkapa, kwa ahadi kwamba, mitambo iliyokuwa inatengeneza “Konyagi Pori” sasa ingetumika kutengeneza kinywaji safi tayari “kumwagilia nyoyo za watu.” Ilipofika mwaka 1994 alibadilishwa wizara hiyo na kuhamishiwa katika Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo. Mwaka 1995, Mrema alijiengua kutoka Chama cha Mapinduzi, CCM na kujiunga na Chama cha NCCR – Mageuzi ambako huko alienda kuwa Mwenyekiti wa Taifa na mgombea Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, akichuana vikali na Hayati Benjamin William Mkapa!

Ni jitihada za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kumnadi Mkapa na ndoto ya Mzee Mrema kuingia Ikulu, ikatoweka kama umande wa asubuhi. Baadaye kulitokea mvurugano ndani ya NCCR Mageuzi, akachomoka huko na kuanzisha chama chake cha Tanzania Labour Part (TLP) ambako aligombea urais mara mbili, mwaka 2000 na 2005. Mrema amewahi kuwa Mbunge wa Vunjo kwa vipindi kadhaa, mpaka mwaka 2015 alipoangushwa na James Mbatia. Mwaka 2016, Hayati Dr. John Pombe Magufuli, alimteua Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole kutokana na uzalendo kwa nchi yake licha ya kuwa Chama cha Upinzani. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini Tanzania wanasema kwamba, Mzee Augustino Lyatonga Mrema alikuwa ni mtanzania wa kwanza kugombea Urais baadaye akashinda Ubunge. Ni Mzalendo aliyewania na kupata uongozi kwa majimbo ya Ubunge kwa vyama vitatu tofauti. Kwa hakika upinzani wanasema ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vya Mzee Mrema. Aliwahi kugombea na kushinda uchaguzi kwa tiketi ya Chama cha Mapunduzi, Jimbo la Moshi, NCCCR-Mageuzi, Jimbo la Temeke na TLP Jimbo la Vunjo, kule KV kwa vijana wa kishua! Mrema mtu wa watu sasa anapumzika kwenye usingizi wa amani. 

Lyatonga Mrema
23 August 2022, 07:07