Mzee Augustino Lyatonga Mrema: Mchango Wake Kwa Tanzania: Haki, Utu na Heshima!
Na Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam & Pd. Richard A. Mjigwa, -Vatican.
Mzee Augustino Lyatonga Mrema, aliyefariki dunia tarehe 21 Agosti 2022 amezikwa kijijini kwake Kiraracha, Marangu kwa "Washua" Alhamisi tarehe 25 Agosti 2022. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumkumbuka Mzee Mrema imeongozwa na Mheshimiwa Padre Deogratias Matika, Wakili Askofu Jimbo Katoliki la Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumkumbuka Mhe. Augustino Lyatonga Mrema kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza mahusiano na vyama vya siasa. “Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia Serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa," amesema Waziri Mkuu. Ametoa kauli hiyo Jumatano, Agosti 24, 2022 wakati akizungumza na mamia ya waombolezaji kwenye ibada ya kumuaga marehemu Mrema katika Parokia ya Mt. Augustino Kilimahewa, Salasala, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amesema salamu za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliwasilishwa asubuhi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango. "Sisi tuliopo hapa tuna mambo mawili makubwa ya kufanya ili kumuenzi ndugu yetu Mrema. Moja ni kuenzi yale yote aliyofanya kwa upande wa Serikali na upande wa siasa lakini pili, tuendelee kumuombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho yake mahali pema peponi," amesema.
Kuhusu mazishi yake yanayofanyika Alhamisi, 25 Agosti 2022 huko Kiraracha, Marangu, Moshi, Waziri Mkuu amesema Serikali inawakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Hamad Masauni. Akizungumza na niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi hilo, DCP Anthony Luta alisema, Jeshi la Polisi litaendelea kumkumbuka Mhe. Mrema kwa mambo kadhaa ikiwemo hatua yake ya kuanzisha jeshi la ulinzi wa sungusungu, ujenzi wa vituo vidogo vya polisi na utetezi wa haki za wanawake ambapo kwa sasa wameanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi. Kwa upande wake, Askofu Msaidizi Henry Mchamungu wa Jimbo kuu la Dar es Saalam alisema umati mkubwa uliokuwepo kanisani hapo ni ishara tosha ya jinsi Bwana Augustino Mrema alivyoishi vizuri na watu wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.
Naye Paroko wa Parokia hiyo Padre Peter Assenga alisema Mhe. Mrema alikuwa akijitolea kwa mambo mengi parokiani hapo na ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake wa hali na mali. Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni pamoja na: Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Hamad Rashid, Prof. Ibrahim Lipumba, John Cheyo, Steven Wassira, James Mbatia, Joseph Selasini na Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro. Itakumbukwa kwamba, Mzee Augustino Lyatonga Mrema alizaliwa tarehe 31 Desemba 1944 kwenye Kijiji cha Kiraracha, Marangu. Alijiunga na masomo ya shule ya msingi kati yam waka 1955 hadi mwaka 1963, Wilayani Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Baadaye alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Patrick, Jimbo Katoliki la Moshi kuhitimu masomo yake mwaka 1965. Mwaka 1970 alijiunga na Chuo cha Siasa Kivukoni. Kati ya Mwaka 1980 hadi mwaka 1981 alikwenda Bulgaria kwa masomo zaidi na hatimaye, kutunukiwa Diploma ya Sayansi ya Ustawi wa jamii na utawala bora. Mwaka 2003 alitumwa kwenda Chuo Kikuu cha Pacific na huko akatunukiwa Shahada ya Sanaa katika Sayansi Jamii. Mzee Augustino Lyatonga Mrema amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia mwaka 1990, na wakati huohuo mwaka 1993 hadi 1994 aliteuliwa tena kuwa Naibu Waziri Mkuu, cheo ambacho hata hivyo hakikuwepo kwenye Katiba ya nchi ambayo kimsingi ndiyo Sheria Mama.
Kumbukumbu zinaonesha kwamba, alipewa cheo hiki ili kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma nchini Tanzania. Hapa anakumbukwa na wengi, kwa kutatua migogoro kwa kipindi cha siku saba au vinginevyo kukiona kilicho mnyoa Kanga manyoya, utendaji uliopelekea kupewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu. Alikuwa mcheshi na mjenga hoja mzuri. Anakumbukwa sana na watu wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwa kupambana sana na utengenezaji sanjari na matumizi ya pombe haramu ya gongo iliyokuwa inadhohofisha maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Gongo, pombe haramu inajulikana sana kama “Machozi ya Simba”, “Kabhurugutu”, “Tuttion” na “Mabomoke” kwani ilikuwa inanywewa kwa kificho kwenye magofu! Ilikuwa ni ngumu kuwashawishi wananchi wa Kanda ya Ziwa kumpigia kura ya Urais Mzee Augustino Lyatonga Mrema wakati wa pambano lake na Mzee Benjamin William Mkapa, kwa ahadi kwamba, mitambo iliyokuwa inatengeneza “Konyagi Pori” sasa ingetumika kutengeneza kinywaji safi tayari “kumwagilia nyoyo za watu.” Ilipofika mwaka 1994 alibadilishwa wizara hiyo na kuhamishiwa katika Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo. Mwaka 1995, Mrema alijiengua kutoka Chama cha Mapinduzi, CCM na kujiunga na Chama cha NCCR – Mageuzi ambako huko alienda kuwa Mwenyekiti wa Taifa na mgombea Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, akichuana vikali na Hayati Benjamin William Mkapa!
Ni jitihada za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kumnadi Mkapa na ndoto ya Mzee Mrema kuingia Ikulu, ikatoweka kama umande wa asubuhi. Baadaye, kulitokea mvurugano, patashika nguo kuchanika ndani ya NCCR Mageuzi, akachomoka huko na kuanzisha chama chake cha Tanzania Labour Part (TLP) ambako aligombea urais mara mbili, mwaka 2000 na 2005. Mrema amewahi kuwa Mbunge wa Vunjo kwa vipindi kadhaa, mpaka mwaka 2015 alipoangushwa na James Mbatia. Mwaka 2016, Hayati Dr. John Pombe Magufuli, alimteua Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole kutokana na uzalendo kwa nchi yake licha ya kuwa Chama cha Upinzani. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini Tanzania wanasema kwamba, Mzee Augustino Lyatonga Mrema alikuwa ni mtanzania wa kwanza kugombea Urais baadaye akashinda Ubunge. Ni Mzalendo aliyewania na kupata uongozi kwa majimbo ya Ubunge kwa vyama vitatu tofauti. Kwa hakika upinzani wanasema ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vya Mzee Mrema. Aliwahi kugombea na kushinda uchaguzi kwa tiketi ya Chama cha Mapunduzi, Jimbo la Moshi, NCCCR-Mageuzi, Jimbo la Temeke na TLP Jimbo la Vunjo, kule Marangu kwa vijana wa kishua! Mrema mtu wa watu sasa anapumzika kwenye usingizi wa amani.