Tafuta

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, tarehe 12 Julai 2022 amepata fursa ya kuwahutubia wajumbe wa AMECEA, Jijini Dar es Salaam: Uchafuzi na uharibifu wa mazingira chanzo cha magonjwa mapya. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, tarehe 12 Julai 2022 amepata fursa ya kuwahutubia wajumbe wa AMECEA, Jijini Dar es Salaam: Uchafuzi na uharibifu wa mazingira chanzo cha magonjwa mapya. 

Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Homa ya Mgunda, Ruangwa, Lindi

Field Fever na kwa Kiswahili "Homa ya Mgunda" Leptospirosis ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na Bakteria aina ya Leptospira interrogans. Ugonjwa huu umekuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika Mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia.

Na Ummy A. Mwalimu - Dar es Salaam, Na Pd. Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, kuanzia tarehe 10-18 Julai 2022 limeadhimisha mkutano wake mkuu wa 20 Jijini Dar es Salaam. Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji. Mkutano huu umenogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Serikali ya Tanzania imetia nia ya kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo AMECEA katika mchakato wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA umehudhuriwa na wajumbe zaidi 270 kutoka ndani na nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Jumanne, tarehe 12 Julai 2022, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewahutubia wajumbe wa AMECEA katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Jijini Dar Es Salaam.

Maaskofu wakisikiliza kwa makini hotuba ya Rais Samia Sukuhu Hassan
Maaskofu wakisikiliza kwa makini hotuba ya Rais Samia Sukuhu Hassan

Katika hotuba yake amekazia ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau mbalimbali katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utunzaji bora wa mazingira ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Papa Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Dar es Salaam inazidi kung’aa kwa usafi Barani Afrika. Serikali ya Tanzania imezindua sera mpya za mazingira. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni tema ambayo imejadiliwa kwa kina na mapana katika Vitabu Vitukufu kwa Dini, Maradhi mapya na hatimaye, umuhimu wa kudumisha amani kama sehemu ya uwajibikaji na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu vitabu vya dini na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote alikuwa na haya ya kusema: Mwenyezi Mungu ameumba kila kwa kipimo, na tunapoharibu kipimo kile tunaharibu maisha yetu. Tunapokwenda kutunza vipimo alivyotuumbia tunatunza maisha yetu wenyewe. Na tunaona mifano hai; tunakata misitu, joto alilotuumbia Mwenyezi Mungu limebadilika sasa limeongezeka kwa sentigredi 2 kwasababu tumekata misitu bila kupanda mingine. Kina cha bahari nacho kimepanda, hakipo kama vile Mwenyezi mungu ametuumbia. Mwenyezi Mungu ametuumbia kila kitu kwa pimo ili tuvitumie na tusidhurike.

Quran Tukufu pia inasema: Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwishatengenezwa. Mungu alishatutengenezea na kututaka tusifanye uharibifu katika nchi. Lakini, papo hapo ametutuma tutumie alivyoviumba lakini tusifanye uharibifu. Kuna maradhi ambayo huko nyuma hayakuwepo lakini kwakuwa tunaharibu misitu vile viumbe ambavyo ilikuwa vihifadhiwe huko misituni sasa vinasambaa vinakuja kwa wanadamu. Kuna kila aina ya maradhi mapya yanazuka hambayo hatukuwa nayo. MARADHI MAPYA: Nilikuwa nazungumza na Waziri Mkuu juzi, ametoka ziara Mikoa ya Kusini Lindi, ameniambia ameona maradhi mapya yameingia, watu wanatokwa na damu za pua na wanadondoka chini. Hatujui ni kitu gani, wanasayansi wamehamia huko kwa uchunguzi zaidi kwa kuwa ni watu wengi wanaougua kwa mfululuzo, na yote ni kwa sababu tunaharibu makazi ya viumbe kule walikowekwa na Mungu, tunawasogeza kwetu wanatuletea maradhi.

Vyanzo vya maji ambayo si safi na salama yanaweza kusababisha maradhi.
Vyanzo vya maji ambayo si safi na salama yanaweza kusababisha maradhi.

Ifuatayo ni taarifa ya ugonjwa wenye dalili za homa inayoambatana na kuvuja damu katika halmashauri ya Ruangwa mkoa wa Lindi 18 julai 2022, Ruangwa – Lindi iliyotolewa na Ummy A. Mwalimu (Mb) WAZIRI WA AFYA. Ndugu wananchi, Itakumbukwa kuwa tarehe 07 Julai 2022, Wizara ya Afya ilipokea taarifa kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi ya uwepo wa wagonjwa wenye dalili za homa inayoambatana na kutoka damu katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi. Kufuatia taarifa hizo, Wizara ilituma timu ya wataalam kutoka ngazi ya Wizara na wengine kutoka Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Chuo kikuu cha Mzumbe, Wataalam kutoka Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa wa Lindi na Halmashauri za Kilwa na Ruangwa pamoja na wataalam wa Mifugo wa Halmashauri za Ruangwa na Kilwa ili kufanya uchunguzi wa ugonjwa huu. Aidha tulipata ushiriki wa wataalam kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani (US CDC).

Ndugu wananchi, hadi kufikia siku ya tarehe 17 Julai 2022, jumla ya wagonjwa 20 na vifo vya watu watatu (3) vimetolewa taarifa. Aidha, kwa sasa, wagonjwa wawili pekee wenye dalili ndiyo bado wamelazwa katika eneo lililotengwa kwa ajili ya matibabu. Vile vile, timu zimeendelea na ufuatiliaji wa watu waliotangamana na wagonjwa (contacts) ambapo mpaka sasa, hakuna aliyeonesha dalili za ugonjwa huu. Ndugu wananchi Itakumbukwa kuwa, taarifa ya awali ya sampuli zilizopimwa katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (National Public Health Laboratory) zilionesha majibu hasi (negative) kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na UVIKO-19. Vile vile, uchunguzi zaidi ulioendelea kwenye Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na Wakala wa Maabara ya Mifugo umeonesha majibu hasi (negative) kwa ugonjwa wa Influenza, Kimeta (Anthrax), Crimean Congo Hemorrhagic Fever (CCHF), Yellow Fever, Chikungunya, West Nile Virus na Rift Valley Fever. Ndugu Wananchi Katika kuongeza wigo wa utambuzi wa chanzo cha ugonjwa huu, uchunguzi katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umefanyika ili kubaini uwezekano wa kuwa na sumu au kemikali zinazoathiri Afya ya Binadamu. Majibu kutoka maabara hii yameonesha kuwa, hakuna sumu au kemikali yoyote yenye uwezekano wa kuathiri afya ya binadamu.

Ndugu Wananchi Nachukua fursa hii kuwataarifu kuwa, kwa sasa upimaji wa sampuli za wagonjwa kutoka maabara zetu umethibitisha mlipuko huu kuwa wa ugonjwa wa Leptospirosis, Field Fever (na kwa lugha ya Kiswahili inajulikana kama Homa ya Mgunda). Leptospirosis ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na Bakteria aina ya Leptospira interrogans. Ugonjwa huu umekuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika Mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia. Wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala, na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu. Kwa Tanzania, ugonjwa huu si mpya, na ulishawahi kutokea mwaka 2014 katika Halmashauri ya Buhigwe mkoani Kigoma. Ndugu wananchi Ugonjwa wa Leptospirosis huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi. Maambukizi ya ugonjwa huu kwenda kwa binadamu hupitia njia zifuatazo; i. Kugusa mkojo (au maji maji mengine ya mwili) kutoka kwa wanyama wenye maambukizi. ii. Kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi. iii. Kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huu aidha, bakteria wanaweza pia kuingia mwilini kupitia ngozi au utando wa mucous (macho, pua au mdomo) na kupitia ngozi yenye mikwaruzo. Maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.

Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa wote
Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa wote

Ndugu Wananchi Mgonjwa aliyeambukizwa vimelea vya ugonjwa huu huanza kuonesha dalili katika kipindi cha kati ya siku tano (5) hadi 14 na wakati mwingine dalili huweza kutokea kati ya siku mbili (2) hadi 30. Dalili za ugonjwa huu zinajumuisha homa, 4 kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, uchovu wa mwili, mwili kuwa na rangi ya manjano, macho kuvilia damu, kutoka damu puani pamoja na kukohoa damu. Ndugu Wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo: i. Kutafuta watu wengine wenye dalili ili kuwapatia huduma ii. Kutoa huduma kwa wagonjwa pindi wanapojitokeza iii. Kuwezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vifaa vya kujikinga na maambukizi iv. Kutekeleza dhana ya Afya Moja (One Health Concept) kwa kuwashirikisha wataalam wa Mifugo, Wanyama pori, Kilimo na Mazingira katika kudhibiti ugonjwa huu v. Kutoa mwongozo wa kitaalam wa jinsi ya kubaini wagonjwa zaidi na kuwahudumia vi. Kutoa elimu kwa jamii ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huu. Ndugu Wananchi, Kwa bahati nzuri ugonjwa huu unaweza kuzuilika na unatibika. Wizara inatoa wito kwa watu wote kuzingatia yafuatayo: i. Kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo kuepuka kugusa maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama na kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa au kutibiwa ii. Wagonjwa wenye dalili za homa, kuvuja damu, kichwa kuuma na mwili kuchoka kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate matibabu sahihi  iii. Kutoa taarifa za wagonjwa wanaoonesha dalili zilizotajwa hapo juu endapo watabainika kuwepo ndani ya jamii.

Kabla ya kuhitimisha nipende kutoa pongezi kwa Wataalam wetu wa Afya ngazi ya Halmashauri ya Ruangwa na Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na viongozi wao, jinsi walivyoweza kubaini kwa haraka tishio hili na kutoa taarifa mapema. Hii inaonesha jinsi eneo la Ufuatiliaji wa Magonjwa (Disease Surveillance) lilivyoimarishwa, endeleeni na utaratibu huo na hii iwe kwa nchi nzima. Aidha, nawapongeza wataalam wote kutoka taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa walioshiriki katika ufuatiliaji wa ugonjwa huu. Hitimisho Ndugu wananchi Wizara inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huu na kuendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu. Hivyo Serikali inawaasa Wananchi kutokuwa na hofu kwani ugonjwa huu unaendelea kudhibitiwa.

Imetolewa na; Ummy A. Mwalimu (Mb) WAZIRI WA AFYA.

Ugonjwa wa Mgunda
19 July 2022, 15:59