Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada, ametoa tamko kuhusu hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 akiomba msamaha. Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada, ametoa tamko kuhusu hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 akiomba msamaha. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Tamko la Gavana Mkuu wa Canada 2022: Ukweli Mchungu

Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada, ametoa tamko kuhusu hotuba ya Papa Francisko aliyoitoa Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 akiomba msamaha huko Maskwacis, Alberta, huku alielezea huzuni kubwa, majuto na dhuluma zilizojitokeza katika mfumo wa shule za makazi ya watu asilia wa Canada. Huu ni ukweli wa kihistoria wa watu wa Canada ambao ni mgumu kuukabili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Kutembea Pamoja” kama kauli mbiu ya hija yake ya 37 ya kitume nchini Canada ni kielelezo makini cha ujasiri wa uponyaji wa madonda ya kihistoria, ili kuanza mchakato wa: Toba, wongofu wa ndani, upatanisho wa Kitaifa na utamadunisho wa Injili kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hija ya 37 ya Kitume ya Papa nchini Canada kuanzia Dominika tarehe 24 hadi Jumamosi tarehe 30 Julai 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo kuu la hija hii ni kusaidia kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, kwa kugusa madonda ya ukosefu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, mambo waliyotendewa watu asilia wa Canada katika historia na maisha yao.

Ukweli wa kihistoria dhidi ya watu asilia wa Canada ni mchungu kuupokea
Ukweli wa kihistoria dhidi ya watu asilia wa Canada ni mchungu kuupokea

Habari kutoka Quebec, nchini Canada zinasema Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada, ametoa tamko kuhusu hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 akiomba msamaha huko Maskwacis, Alberta, huku alielezea huzuni kubwa, majuto na dhuluma zilizojitokeza katika mfumo wa shule za makazi ya watu asilia wa Canada. Huu ni ukweli wa kihistoria wa watu wa Canada ambao ni mgumu kuukabili. Watoto kutoka katika familia za watu asilia wa Canada walipokonywa na kuchukuliwa kikatili kutoka nyumbani kwao, dhuluma na nyanyaso ambazo zimeacha makovu makubwa katika akili na nyoyo za watu hawa. Familia zilisambaratika. Na athari za vitendo hivyo zinaendelea kujitokeza hadi leo.

Hii ni hija ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kitaifa
Hii ni hija ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kitaifa

Watu asilia wa Canada na haswa wale walionusurika wamerithi ndani mwao machungu ya nyanyaso na dhuluma dhidi yao na watoto wengi walipotea katika mazingira hatarishi. Maneno ya Baba Mtakatifu Francisko yasaidie sasa mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Jambo la msingi kwa wakati huu, ni kupiga moyo konde na kusonga mbele, kwa kujenga matumaini sanjari na kuunga mkono jitihada za upatanisho wa Kitaifa unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Canada. Jumuiya ya Kimataifa inakumbushwa kwamba, binadamu si mkamilifu na kwamba, bila uongozi bora na makini, taasisi zinaweza kusababisha madhara makubwa katika maisha ya watu na kwamba, kwa njia ya upatanisho wa kweli, wananchi wa Canada wanaweza kutembea na kufanya kazi kwa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lakini watu asilia wa Canada wanapaswa kujiuliza swali msingi, Je, baada ya hapa wanataka kwenda wapi na kuwa ni akina nani? Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu, ili kujenga jamii inayosimikwa kwenye: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Gavana Canada
26 July 2022, 15:24