Tafuta

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na MSD kulishughulikia suala hilo. WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na MSD kulishughulikia suala hilo.   (AFP or licensors)

MSD Wanatafuna Fedha Ya UVIKO-19 Bila Huruma, Hadi Kero!

Serikali ya Tanzania imekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na MSD kulishughulikia suala hilo. Waziri Mkuu ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wataalamu wa ununuzi na ugavi pamoja na wasimamizi kwenye uzinduzi wa Juma la Ununuzi wa Umma.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dar es Salaam.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) kulishughulikia suala hilo. Waziri Mkuu ametoa onyo hilo Alhamisi, Mei 5, 2022 wakati akizungumza na wataalamu wa ununuzi na ugavi pamoja na wasimamizi kwenye uzinduzi wa Wiki ya Ununuzi wa Umma iliyoanza katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC, Jijini Arusha. "Pamoja na uwepo wa taasisi zinazosimamia manunuzi yanayofanywa katika ofisi zetu, bado wasimamizi wa manunuzi hawajaona huruma kwa walipakodi wetu kwa kuendelea kufanya manunuzi kwa gharama kubwa," amesema Waziri Mkuu na kutolea mfano manunuzi yaliyofanywa na maafisa manunuzi wa MSD ambao wamenunua vifaa kwa gharama kubwa tofauti na bei halisi ya soko.

Upigaji fedha MSD unatisha
Upigaji fedha MSD unatisha

Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema wako baadhi yao ambao hawafanyi kazi ipasavyo na wanatumia njia ambayo haikubaliki. “Hapa nina mfano ambao haufurahishi lakini ni lazima niuseme kwa sababu niko na nyie wataalamu wa ununuzi.” mAmesema kupitia fedha ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alienda kukopa nje, ilitolewa fedha kupitia Wizara ya Afya ili zinununue vifaa vya tiba kwa ajili ya hospitali za mikoa, za rufaa, vituo vya afya na zahanati kwa nia ya kuwapunguzia mzigo Watanzania wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za tiba. “MSD ilipata mgao wa fedha na ilipaswa kununua baadhi ya vifaa na nataka nitoe mfano huu: Walipaswa kununua kipimo cha sukari (blood glucose test) kwa sh. 150.00 lakini wao walikinunua kwa sh. 300.00. Walipaswa kununua kifaa cha kupima mkojo (urinalysis) kwa sh. 200.00 lakini wao walikinunua kwa sh. 780.00” “Walitakiwa kununua kipimo kidogo cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa sh. 2,100 lakini wao walikinunua kwa sh. 4,500; pia walitakiwa kununua kipimo kikubwa cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa sh. 3,800 lakini wao walikinunua kwa sh. 6,300; na walitakiwa kununua kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo na ini (Renal and Liver Function Test) kwa sh. 6,000 lakini wao walikinunua kwa sh. 40,000.”

Akitoa mfano mwingine, Waziri Mkuu amesema MSD walipaswa kununua mashine ndogo ya kupimia kemia ya mwili (chemistry analyzer-semi automated) kwa sh. 1,357,200.00 lakini wao waliinunua kwa sh. 6,786,000 ilhali mashine kubwa ya kupimia kemia ya mwili (chemistry analyzer-full automated) iliyopaswa kununuliwa kwa sh. 10,530,000.00 wao waliinunua kwa sh. 49,000,000. “Walipaswa kununua mashine kubwa ya kupimia hematolojia ya mwili (hematology analyzer 5-part dff full automated) kwa sh. 20,826,000 lakini wao waliinunua kwa sh. 117,000,000. Walipaswa kununua mashine ya kupima mfumokinga wa mwili (Immunology Analyzer Full Automated) kwa sh. 37,440,000.00 lakini wao waliinua kwa sh. 149,760,000.00; na mashine ya kuchata maji kwa ajili ya kutumika katika kusafisha damu walipaswa kuinunua kwa sh. 32,660,880.00 lakini wao waliinunua kwa sh. 129,000,000.00.” “Sasa wataalamu wa manunuzi mtuambie, hii inatokea kwa sababu ya nini? Na kwa maslahi ya nani?” alihoji na kuongeza: “Haya yanafanywa na watu wachache wasiokuwa na nia njema kwa fedha za walipakodi wa Tanzania.

Kuongeza bei kwa bidhaa na huduma si uadilifu katika manunuzi
Kuongeza bei kwa bidhaa na huduma si uadilifu katika manunuzi

Tungeweza kupata vifaa vingi lakini tumenunua kifaa kimoja tu kwa sababu kuna mtu mmoja anatukwamisha kwa kununua bidhaa hii moja kwa bei ya juu.” “Niambieni ni kweli aliyepokea fedha hizo bado anazo? Je, huyu aliyeendesha hilo zoezi hajaenda kufuata fedha nyingine? PSPTB wamesema kazi yao ni kuchukua hatua kwa watumishi wanaokiuka maadili ya taaluma hii. Hatuwezi kukubali fedha za kununua vifaa halafu mtu mmoja ananunua kifaa cha shilingi milioni 12 kwa shilingi zaidi ya milioni 100! Hebu nenda kaangalie.” Waziri Mkuu amesema usimamizi uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) umeokoa kiasi cha shilingi bilioni 98.16 lakini zipo kasoro nyingi zinazohusu ununuzi, usimamizi wa miradi na matumizi mabaya ya fedha za miradi zilizoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa yake ya mwaka 2020/2021. Waandaaji wa mkutano huo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) na unahudhuriwa na wadau mbalimbali wa ununuzi nchini wakiwemo madiwani.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. "Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi," amesema. Waziri Mkuu ametoa wito huo hivi karibuni katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, Jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania. Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani. "Mheshimiwa Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii," amesisitiza.

Gharama ya mafuta imepanda katika soko la dunia, na gharama ya maisha imepanda.
Gharama ya mafuta imepanda katika soko la dunia, na gharama ya maisha imepanda.

Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta. "Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza, kwa kutathmini maombi 24 ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata. Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” amesema. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, Bw. January Makamba, Makatibu Wakuu, pamoja na watendaji wakuu wa Taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

08 May 2022, 13:40