Tafuta

Venezia-grandi-navi-crociera-canale-Piazza-San-Marco.jpg

Siku ya kwanza ya kimataifa ya wanawake wanaofanya kazi katika tasnia ya bahari

Katika Siku ya I ya Kimataifa ya Wanawake katika shughuli za baharini iliyofanyika tarehe 18 Mei 2022 imeongozwa na kauli mbiu: "Mafunzo-Kuonekana-Utambuzi:Kusaidia mazingira ya kazi yasiyo na vizuizi."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Siku ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake katika Usafiri wa Baharini imeadhimishwa tarehe 18 Mei 2022 ikiwa ni mara ya kwanza kabisa kwa  lengo la kutoa jukwaa la kumulika na kusherehekea mafanikio ya wanawake katika bahari na kubainisha maeneo ya kuboreshwa kwa ajili ya usawa wa kijinsia.  Siku hii ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake katika ubaharia au shughuli za baharini imeongozwa na kauli mbiu  "Mafunzo-Kuonekana-Utambuzi: Kusaidia mazingira ya kazi yasiyo na vizuizi." Katibu Mkuu wa Chama cha Kimataifa cha Usafirishaji na Biashara Baharini cha Wanawake IMO, Kitack Lim katika siku hiyo amenukuliwa akisema kwamba  “bado hakuna usawa wa kijinsia katika shughuli za baharini lakini nyakati zinabadilika. Inatambulika kuwa tofauti katika usafiri baharini hunufaisha sekta nzima. Wanawake wa baharini wanafanya kazi kila mahali ili kuunga mkono mabadiliko ya maisha yajayo yaliyopunguzwa kaboni, ya dijitali na endelevu zaidi.”

Tuchuke fursa ya kuadhimisha wanawake wanaochangia mustakabali wa baharini

Bwana Lim anaongeza "hebu tuchukue fursa hii kusherehekea wanawake wengi wanaochangia mustakabali wa baharini: kudumisha injini kwenye meli, kuendesha kampuni, kuandaa kandarasi, kupima meli, au kuongoza mkutano wa kamati wa IMO. Ingawa kuna mengi ya kusherehekea, pia kuna haja ya maendeleo zaidi kufanyika." Hata hivyo tofauti za kijinsia katika shughuli za baharini zimegawanyika sana kisekta, kwa mujibu wa takwimu za Ripoti ya Utafiti wa Wanawake katika Ubaharia au shughuli za baharini.   Ripoti hiyo IMO-WISTA (Chama cha Kimataifa cha Usafirishaji na Biashara Baharini cha Wanawake IMO-WISTA iliyozinduliwa katika Siku ya kwanza ya Kimataifa ya Wanawake katika Usafiri wa Baharini, ina taarifa kuhusu uwiano na usambazaji wa wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya baharini kutoka Nchi Wanachama wa IMO na sekta ya baharini kiujumla. Data zinaonesha kuwa wanawake wanachangia asilimia 29 pekee ya wafanyakazi wote katika tasnia nzima na asilimia 20 ya nguvu kazi ya mamlaka ya kitaifa ya baharini katika Nchi Wanachama.

Kuna tofauti kubwa kati ya sekta ndogo za kibinafsi kwa mijibu wa ripoti

Utafiti huu wa WISTA unachangia juhudi za kuunga mkono Lengo la 5 la Maendeleo Endelevu kuhusu usawa wa kijinsia.  Aidha ripoti hiyo imebainisha tofauti kubwa kati ya sekta ndogo za kibinafsi. Kwa mujibu wa takwimu iliyokusanywa kutoka kwa Mataifa Wanachama, timu za utafutaji na uokoaji katika mamlaka ya kitaifa ya baharini zinachukua wafanyakazi wachache sana wanawake (asilimia 10 tu ikilinganishwa na wanadiplomasia wa kike (asilimia 33) na wafanyakazi wa mafunzo (asilimia 30). Takwimu za tasnia zinaonyesha kuwa mabaharia wanawake ni asilimia 2 tu ya wafanyakazi na wanapatikana zaidi katika sekta ya meli za starehe, wakati katika kampuni za umiliki wa meli ni asilimia 34 ya wafanyakazi.

Tofauti za kijinsia katika tasnia ya bahari kupitia utafiti wa kwanza

Rais wa Kimataifa wa WISTA, Despina Panayiotou Theodosiou amesema, "maarifa ambayo tumekusanya kuhusu tofauti za kijinsia katika tasnia ya bahari kupitia Utafiti huu wa kwanza wa Wanawake katika Utafiti wa Bahari wa 2021 ni hatua muhimu katika azma yetu ya kuunda utofauti kamili wa kijinsia. Kama mukhtasari wa kwanza, uchunguzi huu unatoa ushahidi unaoonesha ni kazi ngapi bado inahitajika kufanywa. Lakini pia inatuonesha ambapo kuna mwanga. Sekta ya bahari inaweza kujionea yenyewe ni sekta zipi zinazosonga mbele kwa ujumuishaji wanawake na wanaume, na zipi hazina.”

19 May 2022, 16:13