Virusi vya Arbo ni tishio kubwa kwa karibu watu bilioni nne ulimwenguni
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Virusi vya Arbo vinaweza visiwe ni kitu ambacho watu wengi wanakifahamu, lakini ni tishio kubwa kwa karibu watu bilioni nne, ndiyo maana Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, limezindua mpango wa kuzuia virusi hivyo kusababisha janga jipya la kimataifa. Virusi vya arbo vinavyojulikana zaidi ni vya baadhi ya magonjwa hatari zaidi duniani yanayoenezwa na mbu, kama vile homa ya kidingapopo, homa ya manjano, Chikungunya na Zika. Magonjwa haya yanawakilisha tishio la kila wakati na kubwa la kiafya katika sehemu za tropiki duniani ingawa kuna idadi inayoongezeka ya milipuko ya virusi vya magonjwa hayo ulimwenguni, kwa mujibu wa WHO.
Lengo la mpango wa kimataifa wa Arbovirus litakuwa kuzingatia rasilimali katika ufuatiliaji wa hatari za magonjwa hayo
Akizungumzia juu ya habari hiyo Dk. Mike Ryan, Mkuu wa mipango ya dharura wa WHO, ameeleza kuwa mpango huo utaruhusu mamlaka za afya kukabiliana na matishio makubwa lakini yanayohusiana yanayoletwa na homa ya kidingapopo, homa ya manjano, Chikungunya na Zika, katika maeneo tofauti ya nchi duniani. “Kwa kila moja ya magonjwa haya kumekuwa na faida katika nyanja tofauti za hatua za ufuatiliaji, utafiti na maendeleo. Lakini uendelevu wa hatua hizo mara nyingi ni mdogo kulingana na upeo na muda na ukubwa wa mahonjwa na miradi mahususi ya magonjwa hayo. Kuna hitaji la dharura la kutathmini upya zana zilizopo na jinsi zinavyoweza kutumika katika magonjwa hayo yote ili kuhakikisha mwitikio mzuri, ushahidi wa hatua zilizochukuliwa, wafanyikazi walio na vifaa na mafunzo yanayohitajika na ushiriki wa jamii.” Shirika la Afrika Duniani (WHO) linasema lengo la mpango wa kimataifa wa Arbovirus litakuwa kuzingatia rasilimali katika ufuatiliaji wa hatari za magonjwa hayo, kuzuia janga la kimataifa, kujiandaa, kugundua na kukabiliana, na milipuko hiyo. WHO imesisitiza kwamba hatua za kimataifa ni muhimu, kwa kuzingatia masafa na ukubwa wa milipuko ya virusi vya arbo, haswa vile ambavyo hupitishwa na mbu aina ya Aedes. Shirika la Afya Ulimwenguni limeonya kuwa ufikiaji wa mbu hao unakua, pia, ukichochewa na mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu duniani na kuongezeka na kukua kwa miji.
Homa ya kidingapopo kila mwaka huambukiza watu milioni 390 katika nchi 130
Kila mwaka, homa ya kidingapopo huambukiza watu milioni 390 katika nchi 130 ambako ni janga. Na homa hii inaweza kusababisha uvujaji wa damu katika ubongo na kifo. Homa ya manjano inaleta hatari kubwa ya milipuko katika nchi 40 na husababisha homa ya manjano na homa kali ya kuvuja damu na hatan kifo. Chikungunya haijulikani sana, lakini iko katika nchi 115 na husababisha ugonjwa mbaya wa mifupa au arthritis. Virusi vya Zika vilipata umaarufu duniani kote mwaka wa 2016 wakati vilipogundulika kusababisha kasoro za kuzaliwa kwa watoto kama vile kuzaliwa na kichwa kikubwa au microencephaly na imegunduliwa katika nchi 89. WHO inaamini kwamba ingawa kuna chanjo ya homa ya manjano, kwa wengine, kinga bora ni kuzuia kuumwa na mbu kwanza.
Pengo la usawa wa kiafya
Akiendelea na ufafanuzi wake Dk. Ryan amebainisha kwamba kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa mpango huo tarehe 31 Machi 2022 kwa miaka miwili kumekuwa na dalili za watu kufurahishwa na mpango huo licha ya shinikizo la janga linaloendelea hivi sasa la UVIKO-19 kwa sababu kuna wasiwasi unaoongezeka juu ya magonjwa ya arboviral kuenea na kusababisha milipuko mikubwa ya kikanda, na kuathiri watu wasio na vifaa vya kutosha kukabiliana na milipuko hiyo. Amesema cha muhimu katika mpango huo wa WHO ni kujenga uwezo wa kukabiliana na vimelea vya magonjwa ya arboviral katika vituo vya afya vya mstari wa mbele, na pia katika ngazi ya kikanda na kimataifa. Dk ameongeza kusema kuwa: “WHO iko tayari kuongoza na kuunga mkono mipango hii ya kimkakati ya kujiandaa na janga hili na kujenga muungano wa kimataifa wa nchi na washirika ili kukabiliana na hatari inayoletwa na vimelea hivi”.