Tafuta

2019.11.18 Mwalimu Julius Nyerere Baba wa Taifa la Tanzania (Rais wa kwanza wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar). 2019.11.18 Mwalimu Julius Nyerere Baba wa Taifa la Tanzania (Rais wa kwanza wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar). 

Tanzania:Aprili 26 ni Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar!

Tunapoelekea katika kilele cha Siku ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar mnamo 26 Aprili,awali ya yote ni vyema kutumia fursa zilizopo ipasavyo kwa maeneo haya kuleta maendeleo yatakayoinua hali ya uchumi wa Watanzania wote.Katika kuzitumia vizuri fursa hizo lazima kuulinda kuuimarisha na kuudumisha Muungano adhimu ambao kwa hakika ni dira ya maendeleo na mafanikio ya wote.

Fahamu kwa ufupi historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa tarehe 26 Aprili 1964 ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri yaTanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume mnamo  tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi hapo tarehe 26 Aprili 1964. Tarehe 27 Aprili 1964 viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano. Sheria za Muungano zilitoa tamko la Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 4 kwamba: “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitalazimika, baada ya kuungana na siku zote baada ya kuungana, kuunganishwa kuwa Dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ (Ibara ya 4 Sheria za Muungano). Jina hili la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadaye mnamo tarehe 28 Oktoba 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano,  namba 61 ya mwaka 1964. Itakumbukwa tendo ambalo lilifanyika siku hiyo ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar ikiwa ni ishara ya kuunganisha nchi mbili wakati wa Sherehe ya Muungano Dar es Salaa mnamo tarehe 26 Aprili 1964

Muundo wa Muungano wa Tanzania

Kwa kutazama muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Sababu za uwepo wa Muungano

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP. Pia, adhma ya kuwa na Muungano wa Afrika hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania uhuru katika ukanda wa Afrika walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo wa Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda. Kimsingi zipo sababu mbalimbali zilizosababisha Muungano huu kama vile historia za nchi hizi mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili.

Katiba ya Muungano

Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano tarehe 22 Aprili, 1964, na kupelekea Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mnamo tarehe 26 Aprili 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano. Halikadhalika, Sheria hizi zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar. Sheria hizi za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano. Vile vile mnamo tarehe 27  Aprili 1964, waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Sheikh Abeid Amani Karume, Kassim Abdala Hanga, Abdulrahaman Mohamed Babu, Hassan Nassor Moyo, Sheikh Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Sheikh Idris Abdul Wakil. Baada ya kuapishwa kuwa Wabunge wakateuliwa kuwa Mawaziri wa Serikali ya Muungano. Kabla ya Muungano, kulikuwa na Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1962 na upande wa Zanzibar kulikuwa na Amri za Katiba.

Marekebisho ya katiba

Katiba ya Tanganyika baada ya kufanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya Muungano iliendelea kutumika kama Katiba ya Muungano ya mpito hadi mwaka 1977 ilipopitishwa Katiba ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano. Aidha, marekebisho hayo yalimtaja Rais wa Zanzibar kuwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa ni msaidizi wa Rais kwa masuala yote ya kiutawala kwa upande wa Zanzibar, na Waziri Mkuu kuwa ni Makamu wa Pili wa Rais ambaye atamsaidia Rais kwa masuala yahusuyo upande wa Tanganyika na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliainisha mambo kumi na moja ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano ambayo ni pamoja na Katiba na Serikali ya Muungano Mambo hayo ni: Mambo ya Nchi za Nje; Ulinzi; Polisi; Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari; Uraia; Uhamiaji; Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje na Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Kuongeza mambo mengine

Mambo mengine  yanayohus katiba hiyo ni Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha; na Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu. Kuongezeka katika  Orodha ya Mambo ya Muungano, kwa mujibu wa Katiba na Sheria na Mambo ya Muungano yaliongezwa kwa kushirikisha pande zote mbili za Muungano. Mnamo tarehe 10  Juni  1965, mambo yote yahusuyo sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali (pamoja na noti); mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusu fedha za kigeni yaliingizwa kuwa jambo la 12 la Muungano. Lengo kubwa la kuongezwa kwa jambo hilo lilikuwa ni kuwa na sarafu ya pamoja ya Tanzania baada ya Muungano na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na mabenki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1964. Baada ya kuvunjika kwa Bodi hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu na mipango yake ya kusimamia mambo ya kibenki na fedha. Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo 1967 na  tarehe 11 Agosti  mambo mawili yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni leseni za viwanda na takwimu (Jambo la 13), na elimu ya juu (Jambo la 14).

Orodha kuongezeka

Mnamo 1968, suala la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia liliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano kuwa Jambo la 15. Vilevile, kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo mwaka1977 na kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, mambo yafuatayo yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo (Jambo la 16); Usafiri; Usafirishaji wa Anga (Jambo la 17) na Utafiti (Jambo la 18); Utabiri wa Hali ya Hewa (Jambo la 19); na Takwimu (Jambo la 20). Kutokana na kuvunjika kwa Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki mwaka 1979, suala la Mahakama ya Rufaa ya Tanzania nalo liliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa Jambo la 21. Vilevile, kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Nyalali iliyokusanya maoni ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Uandikishaji wa Vyama vya Siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo liliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano (Jambo la 22). Suala hilo hatimaye lilipitishwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa,  namba 258. Utaratibu uliotumika katika kuongeza idadi ya mambo ya Muungano kutoka kifungu cha 11 hadi kufikia 22 ni kupitia maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Muungano na nafasi yake ya kuunganisha na kudumisha mahusiano

Hata hivyo  Muungano umechukuwa nafasi kubwa katika kuwaunganisha wananchi na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Tanzania Bara na Tanzania viziwani Zanzibar. Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wigo mpana kwa wananchi wake kuweza kuzitumia fursa mbalimbali zilizopo za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa lengo la kujipatia maendeleo. Ni vyema tukatumia ipasavyo fursa zilizopo Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuleta maendeleo yatakayoinua hali ya uchumi wa Watanzania. Ili tuweze kuzitumia vizuri fursa hizi hatuna budi tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha Muungano wetu adhimu kwani ni dira ya maendeleo na mafanikio yetu.

25 April 2022, 15:07