Tafuta

Ubalozi wa Tanzania uliopo Roma, Italia Jumapili tarehe 6 Machi, 2022, ulifanya Mkutano Mkuu wa Watanzania wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Italia (Diaspora). Ubalozi wa Tanzania uliopo Roma, Italia Jumapili tarehe 6 Machi, 2022, ulifanya Mkutano Mkuu wa Watanzania wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Italia (Diaspora).  

Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia Wafanya Mkutano Mkuu na Diaspora

Ilikuwa ni fursa kwa watanzania wanaoishi nchini Italia, kukutana kwa lengo la kufahamiana. Kusikiliza taarifa za Jumuiya za watanzania nchini Italia; kujadiliana ili kuendelea kudumisha Hekima, umoja na amani ngao muhimu za watanzania mahali popote pale walipo. Lengo ni kudumisha uhuru na umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Na Jubilata E. Shayo, Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia, -Roma.

Ubalozi wa Tanzania uliopo Roma, Italia Jumapili tarehe 6 Machi, 2022, ulifanya Mkutano Mkuu wa Watanzania wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Italia (Diaspora). Mkutano huo ulifanyika chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia na kuhudhuriwa na Wanadiaspora takriban 100 akiwemo Mhashamu Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Hii ilikuwa ni fursa kwa watanzania wanaoishi nchini Italia, kukutana kwa lengo la kufahamiana. Kusikiliza taarifa za Jumuiya za watanzania nchini Italia; kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kuendelea kudumisha Hekima, umoja na amani ngao muhimu za watanzania mahali popote pale walipo. Lengo ni kuweza kudumisha uhuru na umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Watanzania wanaoishi nchini Italia wakutana ili kufahamiana
Watanzania wanaoishi nchini Italia wakutana ili kufahamiana

Haki, umoja na amani ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda na kudumisha mshikamano, umoja wa kitaifa na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu. Mkutano huo uliofanyika kwa mafanikio ulilenga kuukutanisha Ubalozi wa Tanzania na Jumuiya mbalimbali za Watanzania nchini Italia kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya pande hizi mbili. Sanjari na hilo, mkutano huo ulijadili masuala mbalimbali yanayowahusu Wanadiaspora ikiwemo changamoto za kiutendaji na ushirikiano katika Jumuiya zao ambazo zilianishwa wazi kwenye taarifa za kiutendaji zilizowasilishwa na Viongozi wa Jumuiya.  Nchini Italia zipo Jumuiya sita zinazotoka maeneo ya Roma, Napoli, Modena “Central North”, Genova, Modena na Umoja wa Watanzania Wakatoliki unaojumuisha Wakleri, Watawa, Waseminari na walelewa wa Utawa wanaofanya kazi za kitume hapa Italia.

Mkutano uliazimia kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya Wanadiaspora na Ubalozi kwa kuanisha mkakati thabiti wa kuboresha mawasiliano baina ya pande mbili. Aidha, Ubalozi  kama mlezi wa Wanadiaspora hao utazitembelea Jumuiya hizo kwa ajili ya kusaidia kuwasimamia katika uchaguzi wa viongozi, kuandaa au kuboresha Katiba za Jumuiya na kutafuta suluhu ya kudumu dhidi ya changamoto wanazokabiliana nazo.  Kwa kipekee, Mheshimiwa Balozi Kombo alitoa wito kwa Watanzania hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vilevile, aliwahimiza kujisajili katika daftari la Diaspora wa Italia ili kuwa na takwimu na kumbukumbu sahihi za Watanzania waliopo Italia. Takwimu na kumbukumbu hizi zitasaidia Ubalozi kuwaunganisha Wanadiaspora na wabia wa maendeleo ambao wana nia au tayari wanaendesha shughuli zao nchini Tanzania na wanahitaji kushirikiana na Diaspora.

Tanzania Diaspora

 

08 March 2022, 15:53