Siku ya Mtandao Salama duniani. Katika siku hii UNICEF inatambua kuwa dunia kwa hakika  ipo katika wakati ambao mtandao unaenea  kwa kasi sana karibu kila nyanja ya maisha. Siku ya Mtandao Salama duniani. Katika siku hii UNICEF inatambua kuwa dunia kwa hakika ipo katika wakati ambao mtandao unaenea kwa kasi sana karibu kila nyanja ya maisha. 

Uonevu mtandaoni ni unyanyasaji kwa kutumia teknolojia za kidijitali

Wazazi,walezi na walimu wanabeba jukumu la kuhakikisha watoto na vijana wako salama mtandaoni kwa kuwa utafiti uliofanywa na Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano(ITU)ulibainisha kuwa vijana wanatumia muda mwingi mtandaoni kuliko umri mwingine.Haya yalitolewa katika fursa ya Siku ya kimataifa ya Mtanado salama duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 Februari kila mwaka.

Na Angella Rwezaula

Uonevu mtandaoni ni unyanyasaji unaotendeka katika mtandao. Marafiki wote hutaniana wao kwa wao, lakini wakati mwingine ni vigumu kujua ikiwa mtu anafurahia utani huo au unamuumiza. Madhara yanaweza kudumu kwa muda mrefu na kuathiri mtu kwa njia nyingi kwa mfano  kiakili ambapo ni kujisikia hasira, aibu, mjinga, hofu au hasira. Kihisia ni kujisikia aibu au kupoteza hari ya kufanya mambo unayopenda. Kimwili ni kuhisi uchovu (kukosa usingizi), au kupata dalili kama vile maumivu ya tumbo na maumivu ya kichwa. Haya na mengine ni masula ambayo watoto wanapaswa kuyatambua na ambayo yanawezekana kutokana katika mtandao. Tarehe 08 ya kila mwaka ni Siku ya Mtandao Salama duniani. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika siku  hii linatambua kuwa dunia kwa hakika  ipo katika wakati ambao mtandao unaenea  kwa kasi sana karibu kila nyanja ya maisha. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “ kwa pamoja kubadili mtandao ukawa bora”.

Kutokana na ukweli huo wazazi, walezi na walimu wanabeba jukumu la kuhakikisha watoto na vijana wako salama mtandaoni kwa kuwa utafiti uliofanywa na Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) ulibainisha kuwa vijana wanatumia muda mwingi mtandaoni kuliko umri mwingine. Utafiti huo wa mwaka 2020, umewaonesha kuwa na uwezekano wa kuunganishwa kwenye Mtandao kwa asilimia 24% kuliko watu wengine wote. Pia inakadiriwa asilimia 71% ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 wanatumia Intaneti, ikilinganishwa na asilimia 57%  tu katika makundi mengine ya umri, kulingana na takwimu za (ITU). Miongoni mwa masuala yanayoumiza vichwa wazazi na walezi wengi ni suala la watoto kuonewa au kunyanyaswa mtandaoni “cyberbullying“ na ndio maana UNICEF katika kuadhimisha siku hii ya mitandao salama wemekuja na mbinu kadhaa za kuelimisha namna ya kupambana na hali hizo hususan kwa watoto.

Yapo masuala  8 ambayo watoto wanapaswa kuyatambua. Uonevu wa mtandaoni ni nini? Uonevu mtandaoni ni unyanyasaji unaotendeka kwa kutumia teknolojia za kidijitali. Mtu anaweza kufanyiwa kwenye mitandao ya kijamii, majukwaa ya kutuma ujumbe, majukwaa ya michezo ya kubahatisha na hata kwenye simu za mkononi.  Uonevu huu huwa na tabia ya kujirudia lengo likiwa ni kutisha, kukasirisha au kuwaaibisha wale wanaolengwa.  Mifano ya matendo ya uonevu wa mtandaoni ni pamoja na kueneza uwongo, kutuma picha au video za aibu za mtu fulani kwenye mitandao ya kijamii, kutuma ujumbe, picha au video za kuumiza, matusi au vitisho kupitia mifumo ya ujumbe, kuiga mtu mwingine na kutuma ujumbe mbaya kwa wengine kwa niaba yao au kupitia akaunti za kughushi. Uonevu wa ana kwa ana na ule wa mtandao mara nyingi unaweza kutokea pamoja. Lakini uonevu mtandaoni huacha alama za kidijitali , na hizi kuweza kutumika kama rekodi muhimu ya kutoa ushahidi wa kusaidia kukomesha uonevu huo.

Je, unawezaje kutofautisha mzaha na uonevu mtandaoni? Marafiki wote hutaniana wao kwa wao, lakini wakati mwingine ni vigumu kujua ikiwa mtu anafurahia utani huo au unamuumiza. Wakati mwingine mtu anaweza kukuumiza nafsi na kuishia kucheka kwa kusema “natania tu,” au “usiichukulie kwa uzito sana.” Lakini ikiwa unahisi kuumia au kufikiria wengine wanakucheka, basi mzaha huo umekwenda mbali sana na nivyema kumwambia anayefanya hivyo aache mara moja. Ikiwa ataendelea hata baada ya kumwomba, basi huu unaweza kuwa uonevu. Na hali huwa mbaya zaidi inapofanyika mtandaoni kwa sababu watu wengi wanaona wakiwemo wageni. Cha kuzingatia ni ikiwa huna furaha kuhusu jambo hilo, hupaswi kukaa kimya. Na ikiwa unajisikia vibaya ni vyema kupata msaada.  Kukomesha uonevu wa mtandao sio tu kuwataja wakorofi, bali pia ni kutambua kwamba kila mtu anastahili heshima mtandaoni na katika maisha halisi.

Yapi ni madhara ya uonevu mtandaoni? Madhara yanaweza kudumu kwa muda mrefu na kuathiri mtu kwa njia nyingi: Kiakili - kujisikia hasira, aibu, mjinga, hofu au hasira. Kihisia-kujisikia aibu au kupoteza hari ya kufanya mambo unayopenda. Kimwili - uchovu (kukosa usingizi), au kupata dalili kama vile maumivu ya tumbo na maumivu ya kichwa. Hisia ya kuchekwa au kunyanyaswa na wengine, inaweza kuzuia watu kuzungumza au kujaribu kushughulikia tatizo linalowakabili. Katika hali mbaya zaidi, uonevu wa mtandao unaweza hata kusababisha watu kujiua. Uonevu mbali na kuleta athari nyingi lakini aliyefanyiwa vitendo hivyo anaweza kushinda hisia mbaya na kurejesha imani na afya yake.

Nizungumze na nani iwapo nimefanyiwa uonevu mtandaoni?  Ni muhimu sana kutoa ripoti iwapo umefanyiwa uonevu mtandaoni.  Hatua ya kwanza ni kutafuta msaada kutoka kwa mtu unayemuamini kama vile wazazi wako, rafiki yako, mwanafamilia au mtu mzima mwingine unayemuamini. Ikiwa ni shuleni unaweza kuwasiliana na mshauri, mkufunzi wa michezo au mwalimu unayempenda, na unaweza kufanya hivi kwa njia ya mtandao au ana kwa ana. Na ikiwa huna raha kuzungumza na mtu unayemjua, tafuta simu ya usaidizi katika nchi yako ili kuzungumza na mshauri wa kitaalamu. Ikiwa uonevu unafanyika kwenye mtandao wa kijamii, zingatia kumzuia mnyanyasaji na kuripoti rasmi tabia zao kwenye mtandao huo. Makampuni ya mitandao ya kijamii yana wajibu wa kuwaweka watumiaji wao salama.

Kusanya ushahidi wa uonevu: Ili kukomesha uonevu, inahitaji kutambuliwa na kuripotiwa. Kusanya na hifadhi ushahidi, iwe ni ujumbe mfupi au picha za simu, upige picha “screenshot” ili kuonesha kile ambacho kimekuwa kikiendelea. Ili uonevu ukome, inahitaji kutambuliwa na kuripoti ni muhimu. Inaweza pia kusaidia kuonesha mnyanyasaji kwamba tabia yake haikubaliki. Ikiwa uko katika hatari na unahitaji jambo hilo kutatuliwa kwa dharura basi unapaswa kuwasiliana na polisi au huduma za dharura katika nchi yako.

Jinsi ya kumsaidia rafiki aliye onewa mtandaoni:  Mtu yeyote anaweza kuwasilisha taarifa za unyanyasaji wa mtandaoni. Ukiona mtu anatendewa vitendo viovu na unamfahamu jaribu kutoa usaidizi. Ni muhimu kumsikiliza rafiki yako au mtu huyo kwanini anaogopa kwenda kutoa taarifa na kuonewa mtandaoni. Unaweza kumuuliza Je, wanajisikiaje?  Unaweza kumsaidia kwa kumjulisha kwamba si lazima aripoti chochote rasmi, lakini ni muhimu kuzungumza na mtu ambaye anaweza kusaidia.

Zingatia haya: Rafiki yako anaweza kuwa na hisia dhaifu. Kuwa mkarimu kwake, msaidie kufikiria anachoweza kusema. Jitolee kwenda naye ikiwa ataamua kwenda kutoa malalamiko rasmi. Muhimu zaidi, mkumbushe kuwa uko kwa ajili yake na unataka kumsaidia. Ikiwa rafiki yako bado hataki kuripoti tukio hilo, basi umuunge mkono kutafuta mtu mzima anayemwamini ambaye anaweza kumsaidia kukabiliana na hali hiyo. Kumbuka kwamba katika hali fulani matokeo ya unyanyasaji mtandaoni yanaweza kutishia maisha. Kutofanya chochote kunaweza kumfanya mtu ahisi kwamba kila mtu yuko kinyume naye au kwamba hakuna anayejali. Maneno yako yanaweza kuleta mabadiliko.

Je, kuna adhabu ya uonevu mtandaoni? Shule nyingi huchukulia uonevu kwa uzito na watachukua hatua dhidi ya aliyeanya uonevu. Ikiwa unadhulumiwa mtandaoni na wanafunzi wengine, ripoti kwa shule yako. Watu ambao ni waathirika wa aina yoyote ya unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na uonevu na uonevu mtandaoni, wana haki ya kupata haki na kuwajibishwa mkosaji. Sheria dhidi ya unyanyasaji, haswa juu ya uonevu wa mtandaoni, ni mpya na bado hazipo kila mahali. Hii ndiyo sababu nchi nyingi hutegemea sheria zingine zinazofaa, kama vile dhidi ya unyanyasaji, kuadhibu wanyanyasaji wa mtandao. Katika baadhi ya nchi zenye sheria hizi, waathiriwa wa unyanyasaji wa mtandaoni wanaweza kutafuta ulinzi, kuzuia mawasiliano kutoka kwa mtu maalum na kuzuia matumizi ya vifaa vya kielektroniki vinavyotumiwa na mtu huyo kwa uonevu wa mtandaoni, kwa muda au kwa kudumu. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa adhabu si mara zote njia bora zaidi ya kubadili tabia ya waonevu. Mara nyingi ni bora kuzingatia kurekebisha madhara na kurekebisha uhusiano.

Nyenzo za mtandaoni za kuzuia unyanyasaji na Uonevu kwa watoto au vijana: Kila mtandao wa kijamii hutoa zana tofauti zinazokuruhusu kuweka vikwazo kuhusu nani anayeweza kutoa maoni au kutazama machapisho yako au anayeweza kuunganishwa kama rafiki, na kuripoti visa vya uchokozi. Nyezo nyingi kati ya hizo zinahusisha hatua rahisi za kuzuia, kunyamazisha au kuripoti unyanyasaji wa mtandaoni. Kampuni za mitandao ya kijamii pia hutoa elimu na mwongozo kwa watoto, wazazi na walimu kujifunza kuhusu hatari na njia za kukaa salama mtandaoni Kumbuka ya kwanza ya ulinzi dhidi ya uonevu mtandaoni inaweza kuwa wewe mwenyewe. Fikiria kuhusu mahali ambapo unyanyasaji wa mtandaoni hutokea katika jumuiya yako na njia unazoweza kusaidia  kwa kupaza sauti yako, kuwataja waonevu, kuwasiliana na watu wazima unaowaamini au kwa kutoa ufahamu kuhusu suala hilo.  Kama umeshawahi kufanyiwa uonevu mtandaoni haupo pekeyako, tazama video hii ya vijana waliofanyowa uonevu ambao wanaeleza namna uya kukabiliana na hali hiyo. Sikiliza ushuhuda  kwa njia ya UNICEF - YouTube Bofya hapa

15 February 2022, 15:11