Siku ya Kimataifa ya Radio:inaendelea kuwa kiungo nafuu zaidi kusikilizwa kokote
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tarehe 13 Februari ni Siku ya kimataifa ya redio duniani, sambamba na siku ambayo Redio ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa mnamo 1946. Kauli mbiu ambayo imeongozwa mwaka 2022 ni “ Imani kwa Radio. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mnamo mwaka 2013 kufuatia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2012. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO katika fursa hiyo linasema malengo ya mwaka huu yanazingatia kwa historia yake ya zaidi ya karne moja, redio imeendelea kuwa moja ya vyombo vya habari vinavyotumika na kuaminika zaidi. Kwa mujibu wa Audrey Azoulay Mkurugenzi Mkuu UNESCO amesema kwa “Miaka nenda miaka rudi, radio imekuwa ikitoa taarifa zinazowafikia watu kwa wakati huo huo na utafutaji na usambazaji wa habari zenye maslahi kwa umma unaozingatia ueledi, na wakati huo huo kupatia watu burudani na mafunzo,” Hata wakati wa sasa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, radio imeweza kuziba pengo hilo la kidijitali la kati ya mbinu za kitamaduni za kusikiliza radio na mbinu za kisasa kwa kuja na mifumo mbalimbali ya kuhakikisha taarifa zake zinasikikika kupitia majukwaa mbalimbali kama vile podikasti na kwenye wavuti na hata simu za viganjani.
Janga la Uviko-19 limemomonyoa imani kwa vyombo vya habari
UNESCO inasema matukio ya hivi karibuni na janga la ugonjwa wa Corona au UVIKO-19 yamemomonyoa imani kwa vyombo vya habari na kuchochea kusambaa kwa haraka kwa taarifa za uongo na upotofu katika vyombo vya habari. Lakini “hata hivyo ingawa tafiti zinaonesha kuporomoka kwa imani ya umma katika mitandao ya kijamii na intaneti, bado kuona ongezeko kubwa la imani ya umma kwenye habari. Na raia wengine bado wana imani kubwa na radio kuliko vyombo vingine vya habari,” inabainisha UNESCO. Pengo la kidijitali bado linaonesha hali kubwa baina ya jamii na maeneo lakini radio inaendelea kuwa kiungo nafuu zaidi ambacho kinaweza kusikilizwa kokote hata ambako hakuna umeme wa uhakika au kiunganisho cha intaneti. Radio imeendelea kuwa jumuishi na uwepo wa redio za kijamii umeziba pengo la kupata taarifa kwa baadhi ya jamii zilizo pembezoni ambazo sasa zinahizi kuwa zinawakilishwa vyema na vyombo vya habari vya eneo lao.
Vituo vya Radio vizingatie imani kwa kuandaa vipindi huru na ubora
Na ndiyo katika mantiki hiyo katika siku hii ya radio duniani, UNESCO imetoa wito kwa vituo vya radio duniani kusherehekea siku hii kwa kuzingatia maeneo makuu matatu ambayo ni: Imani kwa uandishi wa habari wa radio kwa kuandaa vipindi huru na vya ubora wa juu. Hapa ikimaanisha kuheshimu maadili ya kimsingi ya uandishi wa habari. Radio imekumbwa na changamoto kubwa katika zama za sasa za kasi ya kidijitali lakini ili kuendelea kujenga imani kwa msikilizaji wake, imeendelea kuhakiki na kuthibitisha taarifa zake kabla ya kuzipeleka hewani kwa maslahi ya umma na kujenga jamii endelevu kwa wote.
Imani na uwezo wa radio kufikia wengi bila kujali hadhira yake
Pili Imani na uwezo wa radio kufikia wengi kwa kujali hadhira yake. Hii ikimaanisha kuwa radio inaweza kukidhi matakwa ya wasikilizaji iwe kimakundi au kieneo. Kwa mfano vipindi kwa watu wenye ulemavu, wakimbizi, wanawake na hata viziwi. Na hatimaye ambayo ni ya tatu ni imani na uhalisia wa redio katika kuhakikisha ushindani kwa kuona ni kwa jinsi gani redio inaweza kuendelea kuwepo pindi kuna janga la kifedha katika matangazo ya biashara. Mada hii inauganisha suala la redio kuendelea kujikimu kiuchumi na uwezo wake wa kuvutia na kuendelea kukidhi mahitaji ya hadhira yake.