Zinahitajika dola milioni 138 kusaidia watu wa Kanda ya Pembe ya Afrika
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo -FAO Jumatatu tarehe 17 Januari 2022, jijini Roma, Italia wakati wakitoa ripoti ya kina kuhusu mpango wa kukabiliana na changamoto za kilimo na aina ya msaada unaoitajika kwa kila kanda wamebainisha kuwa, zinahitajika zaidi ya dola milioni 138 za ufadhili wa dharura kusaidia watu milioni 1.5 walio hatarini katika jamii za vijijini katika Pembe ya Afrika ambapo mashamba yao na malisho ya mifugo yameathiriwa na ukame wa muda mrefu. Pembe ya Afrika ni eneo ambalo tayari linakabiliwa na uhaba wa chakula unaohusishwa na hali mbaya ya hewa, vikwazo vya maliasili na migogoro, janga la COVID-19 na uvamizi wa nzige wa mnamo 2020-2021, ambao umefanya jamii kwa hakika kukabiliana na changamoto hizi hadi kufikia ukomo wa kudhoofisha uzalishaji wa kilimo.
Nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia, ndizo zilizoathirika zaidi, ambapo makadirio yanaonesha kuwa takriban za watu milioni 25.3 watakuwa hawana uhakika wa chakula ifikapo katikati ya mwaka wa 2022. Na ikiwa msaada hautapatikana na hali hiyo ikatokea basi, Pembe ya Afrika itakuwa kati ya nchi zinazokabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula duniani. Aidha ufugaji wa kuhamahama, ni njia ya kitamaduni ya ufugaji, ambayo inawaajiri zaidi ya watu milioni 200 kwenye nchi 100 kwa mujibu taarifa hiyo ya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO. Wakiwa na aina tofauti ya mifugo ya kienyeji wanaweza kubadilika kulingana na mazingira tofauti, ufugaji ni muhimu katika kupunguza umaskini na kuhakikisha uhakika wa chakula katika maeneo hayo.
Sababu saba za kwanini ufugaji wa kuhamahama ni muhimu kwa ajili ya mustakbali wa chakula: unaongeza uwepo wa chakula, unazuia mabadiliko ya tabianchi, unasaidia kama mfumo wa tahadhari ya mapema kuhusu magonjwa, unachangia kuongeza nafasi za ajira, unapunguza ushindani kati ya kula na chakula,unalinda utofauti wa wanyama, nalinda utofauti wa wanyama, na hatimaye unasaidia ukuaji wa misitu.
Unaongeza uwepo wa chakula: Katika ulimwengu ambapo upatikanaji wa mali asili na mabadiliko ya tabianchi vinazidi kutofautiana, kutegemea mahitaji ya maziwa na nyama ni hatari katika uzalishaji. Ufugaji wa kuhamama, huchangia protini nafuu na ya hali ya juu na lishe ili kutimiza mahitaji ya jamii na unaweza kusaidia nchi kutotegemea uagizaji wa chakula. Na kwa sababu wafugaji husafiri na mifugo yao kutafuta lishe na maji, mazao huwa kidogo kuliko gharama wanazotumia.
Unazuia mabadiliko ya tabianchi: Kwa mujibu wa FAO, utafiti unaonesha kuwa mandhari ya ufugaji yana uwezo wa kupunguza viwango vya hewa ukaa kwa kuwa wakati mifugo wanakula malisho inachangia mimea kuota tena. Pia wakati mifugo wanahama wanaweza kuacha mbolea ambayo inachangia kukua kwa mimea. Wafugaji pia husaidia kusimamia vyema mali asili kusaidia kulinda viumbe hao katika mazingira yote, kuanzia maeneo ya jangwa hadi sehemu zenye maji na misitu. Kwa kujumuisha ujuzi wa wafugaji wanaweza kusaidia kulinda mifumo na ikolojia.
Unasaidia kama mfumo wa tahadhari ya mapema kuhusu magonjwa: Janga la COVID-19 limetufunza jinsi ya kukabiliana na changamoto za kiafya likihitaji kutilia maanani afya ya wanyama, mazingira na wanadamu. Ni njia mojawapo inayosaidia nchi kufuatilia na kudhibiti magonjwa yanayoambukiza kati ya wanyama na wanadamu. Wafugaji wa kuhamahama wana wajibu mkubwa kwa hili kwa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu magonjwa mapya ya kuambukiza, ambayo ni tisho kwa wanyapori. Kuhakakisha uwepo wa huduma za afya ya mifugo na hatua za kuzuia ikiwemo chanjo nafuu na ya hali ya juu, ambayo itasadia kuongeza uzalishaji na kupunguza hatari ya maaambukizi ya magonjwa. Kati ya mwaka 2016 na 2018 FAO ilichanja mifugo milioni 30 katika maeneo ya wafugaji nchini Ethiopia.
Unachangia kuongeza nafasi za ajira: Ufugaji huwa ni tegemeo la maisha kwa mamilioni ya watu kwenye asilimia 75 ya nchi za dunia hii, lakini umepuuzwa kwa miaka mingi kutokana na sera na uwekezaji. Kuwasaidia wafugaji kupata elimu, habari, masoko, msaada madaktari, afya na misaada ya kifedha vinaweza kuchangia matokeo makubwa wa kiuchumi na kijamii.
Unapunguza ushindani kati ya kula na chakula: Mahitaji ya chakula yatokanayo na mifugo inayokuzwa kwa kutumia chakula asilia ambacho ni nyasi yanazidi kuongezeka na kupanua soka la bidhaa hizi na pia kuchangia fursa mpya kwa mauzo ya nje na faida. Inakadiriwa kuwa hadi watu milioni 811 duniani walikabiliwa na njaa mwaka 2020. Mifumo ya asili ya ufugaji wa kutegemea malisho inaweza kusaidia kuongeza uhakika wa chakula kwa kupunguza ushindani katika nafaka kati ya chakula cha mifugo na chakula cha binadamu.
Unalinda utofauti wa wanyama: Familia za wanyama wa kuhamahama zimekuwa zikifugwa kwa maelfu ya miaka na kuchangia katika baadhi ya viwango vya juu vya utofauti wa vinasaba kwa aina mbalimbali za wanyama. Utofauti huu wa mifugo wa kienyeji hutokana na kutegemeana kwa karibu kati ya mazingira, wafugaji na mifugo. Kutona na kuchagua kwa kuzingatia aina yamifugo na ufahamu wao wafugaji wanaendelea kuboresha mifugo wao na kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko ya mazingira , magonjwa na kubadilika kwa masoko.
Unasaidia ukuaji wa misitu: Ufugaji na misitu hutegemeana. Katika Sehemu zingine misitu iliyo karibu na maeneo yenye maji, huwa ni malisho muhimu kwa mifugo wakati wa kiangazi. Kwa kubadilishana ufugaji husaidia kudumisha na kufufua upya maeneo haya. Kwa mfano wanyama wanaocheua husaidia kumea mbegu za miti ya mshita katika misitu ya nchi kavu. Na wafugaji huwa na nafasi kubwa ya kuzuia moto wa nyika kwa kuwa wanyama wao hupunguza majani msituni na hivyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.