Tafuta

Waziri mkuu wa Tanzania amewataka Mabalozi wa Tanzania nchi za nje, kuwahamasisha wawekezaji ili kuwekeza katika vitega uchumi na huduma nchini Tanzania. Waziri mkuu wa Tanzania amewataka Mabalozi wa Tanzania nchi za nje, kuwahamasisha wawekezaji ili kuwekeza katika vitega uchumi na huduma nchini Tanzania. 

Mabalozi wa Tanzania Ughaibuni Hamasisheni Ujio wa Wawekezaji

Waziri mkuu Kassimu Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali watoe msukumo Katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi, kuimarisha biashara pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika maeneo yao ya uwakilishi. Mabalozi wamesema, watatekeleza maelekezo hayo yote!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dodoma.

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali watoe msukumo Katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi, kuimarisha biashara pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika maeneo yao ya uwakilishi. Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza mabalozi hao kuhakikisha wanalinda taswira ya Tanzania katika nchi za uwakilishi sambamba na kujielekeza katika kuvutia watalii na kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kufanya biashara nje. Waziri Mkuu amekutana na mabalozi hao Jumatatu, Januari 17, 2022 ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. Mabalozi aliyokutana nao ni Balozi Profesa Adelardus Kilangi (Brazil), Balozi Said Juma Mshana (DR-Congo), Balozi Alex Gabriel Kalua (Israel), Balozi Said Shaib Mussa (Kuwait) na Balozi Fredrick Ibrahim Kibuta (Urusi). Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka mabalozi hao wahakikishe wanakwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa balozi kwa kubana matumizi hususani katika mambo yasiyokuwa ya lazima. “Pia mkaimarishe mahusiano kati yenu na maafisa wa ubalozi.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakutane na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) na wawasaidie kuimarisha Jumuiya zao kwa kuwa na uongozi imara. “Waunganisheni ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na kwenye shughuli za kijamii mnazozifanya huko.” Waziri Mkuu amesema mabalozi hao wanatakiwa kuitangaza sana lugha ya Kiswahili. “Naamini mkitumia ushawishi wenu katika kukitangaza Kiswahili kinaweza kuwa chanzo cha ajira kwa Watanzania nje hususan kwa walimu wa fani hiyo sambamba na kuitangaza nchi yetu.” Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake, Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Balozi Kilangi ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu kwa kukutana nao na ameahidi kwamba hawatamuangusha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake na kwamba watahakikisha wanakwenda kutekeleza maelekezo yote kwa manufaa ya Taifa.

 

18 January 2022, 11:13