Afrika ya Kusini kuwa Nchi ya kwanza barani Afrika kutengeneza chanjo ya Uviko
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Katika harakati za mapambamo ya upatikanaji sawa wa chanjo za UVIKO -19, ambazo zimeiina nchi ya Afrika Kusini katika mkakati huo, hatimaye imezindua kiwanda cha kwanza katika bara Afrika siku ya Jumatano tarehe 19 Januari 2022 huko Cape Town ambacho kitatengeneza dozi kuanzia mwanzo hadi mwisho na ambacho kinafadhiliwa na mmilionea mmoja wa bayoteknolojia Patrick Soon-Shiong.
Dozi bilioni moja kwa mwaka ifikapo mwaka 2025
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo kutoka Marekani lakini mwenye asili ya China, na ambaye alizaliwa Afrika Kusini amesema kuwa “Lengo ni kuzalisha chanjo ya kizazi cha pili, na tunataka kuitengeneza barani Afrika, kwa ajili ya Afrika, na kuisafirisha ulimwenguni kote”, Chanjo za kwanza zitatolewa mwaka huu na lengo ni kufikia dozi bilioni moja kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.
Ramaphosa: Leo tunathibitisha kwamba tunajitosheleza kama bara
Kufuatia na tukio hilo, naye Rais wa Afrika Kusini Bwana Cyril Ramaphosa alisema: “Leo tunathibitisha kwamba tunajitosheleza kama bara, na tunapaswa kujivunia kile tunachofikia,". Nchi ya Afrika iliyoathiriwa zaidi na virusi hivyo, ina zaidi ya kesi milioni 3.5 ikiwa ni pamoja na vifo 93,400, wakati bara la Afrika lilirekodi kesi zaidi ya milioni 10 mwezi Januari, kulingana na taarifa za Umoja wa Afrika. Hata hivyo maambukizi yameongezeka tangu kirusi kipya cha aina ya Omicron kilipogunduliwa nchini Afrika Kusini mwishoni mwa mwezi Novemba 2021.