Mgogoro nchini Ethiopia unaendelea kwani Waziri Mkuu anasema kuendelea mbele kukabiliana na waasi. Mgogoro nchini Ethiopia unaendelea kwani Waziri Mkuu anasema kuendelea mbele kukabiliana na waasi. 

Ethiopia:Umoja wa mataifa watoa tahadhari kuondoa watu kimataifa

Mabalozi mjini Addis Ababa wamepokea mwaliko wa kuondoka nchini bila kuchelewa.Mapigano kutoka kaskazini yanakaribia mji mkuu baada ya vita vya zaidi ya mwaka mmoja kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Tigray.Wakati huo huo,njaa inashika kasi na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linabainisha kuwa litafikia zaidi ya watu 450,000 katika wiki mbili zijazo.

Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.

Vyombo vya habari vya kitaifa nchini Ethiopia vinasema Waziri Mkuu Abiy Ahmed ameelekea kuwaongoza wanajeshi katika mapigano yanayoendelea nchini humo. Haya yanafanyika wakati jamii ya kimataifa ikiwa imeingia hofu kuhusiana na mzozo huo unaozidi na wakati wapiganaji wa Tigray wakidai kuukaribia Mji Mkuu Addis Ababa huku raia wengi wa kigeni wakiambiwa waondoke nchini humo. Taarifa za vyombo vya habari nchini humo zinasema naibu Waziri Mkuu Demeke Mekonne Hassen sasa ndiye atakayechukua jukumu la shughuli za kawaida za serikali kufuatia kuondoka kwa Waziri Mkuu Ahmed. Marekani inawashauri raia wake kuondoka Ethiopia sasa “maadamu safari za ndege zilizopangwa bado ziko wazi.”  “Ondokeni kabla mambo hayajabadilika” ni ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa hakika, ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa ni vigumu kuwasaidia raia wa Marekani nchini Ethiopia kama chaguzi za kibiashara hazitapatikani tena”. Afrika Kusini na Kenya zilihimiza pande zinazozozana nchini Ethiopia kusitisha mapigano mara moja baada ya waziri mkuu, Abiy Ahmed, kuahidi kupigana akiwa mstari wa mbele, akiwaongoza wanajeshi dhidi ya waasi wa Chama cha uhuru wa watu  cha Tigray (Tplf).

Msemaji wa serikali Legesse Tulu amezungumzia kwa kina kuhusiana na kuhamishwa huko kwa baadhi ya madaraka kwa muda katika afisi ya naibu waziri mkuu. Haya yanafanyika wakati Umoja wa Mataifa ukiwa unasema umeamrisha kuondolewa nchini humo kwa wafanyakazi wake wa kimataifa na familia zao huku Ufaransa ikiwa nchi ya hivi karibuni ya Magharibi kuwaambia raia wake waondoke katika nchi hiyo iliyozongwa na mzozo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. “Kutokana na hali ya ukosefu wa usalama nchini humo na kwa ajili ya kuchukua tahadhari tu, Umoja wa Mataifa umeamua kupunguza nyayo zake Ethiopia na kuwahamisha kwa muda wafanyakazi wake. Ni muhimu kufahamu kwamba baadhi ya wafanyakazi watasalia ili kutimiza majukumu yetu muhimu, alisema Dujarric. Kundi la Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF wiki hii lilidai kwamba limeuteka mji mmoja ulioko kilomita 220 hivi kutoka Mji Mkuu Addis ingawa madai yanayotolewa katika uwanja wa mapambano nchini Ethiopia si rahisi kuyathibitisha kutokana na ukosefu wa mawasiliano.

Mnamo Jumatatu tarehe 22 Novemba Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliapa atawaongoza wanajeshi wake katika mapambano katika kile ambacho serikali imekiita ‘vita vinavyoendelea’ katika nchi ya pili yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika. Mambo haya yanatilia mashaka matumaini ya kufikishwa mwisho kwa mapigano hayo ambayo yamezua hofu kwamba huenda yakaenea katika eneo zima la Pembe ya Afrika. Lakini mjumbe wa Marekani Jeffrey Feltman amesema anaona hatua zikipigwa kuelekea kusitishwa kwa mapigano katika mazungumzo kati ya pande mbili zinazozozana nchini Ethiopia ingawa anahofia kwamba mapambano ya kijeshi huenda yakalemaza juhudi hizo. Masuala yanayotarajiwa kuletwa kwenye meza ya mazungumzo na ingawa masuala hayo yanafanana, tofauti zinaibuka katika suala lipi kulipa kipau mbele katika mazungumzo hayo.

Kwa wakati huo huo, Umoja wa Mataifa unabainisha kuwa mamia ya maelfu ya watu wako katika hali ya njaa na kwa maana hiyo wametoa nguvu kubwa katika usambazaji wa chakula cha msaada kwa miji ya kaskazini mwa Ethiopia. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limetangaza kuwa katika muda wa wiki mbili zijazo msaada utawafikia zaidi ya watu 450,000 katika miji ya Kombolcha na Dessie, katika eneo la Amhara, ambako maghala yamesambaratishwa siku za hivi karibuni, huku vibanda na vifaa vikiwa vimeharibiwa. Ni miji hii ambayo hutokea kwenye mipango muhimu katika barabara kubwa inayoelekea Addis Abeba.

24 November 2021, 13:28