Nchi za Afrika zimetakiwa kuwa na kauli moja kuhusu biashara ya uwindaji wa kitalii. Nchi za Afrika zimetakiwa kuwa na kauli moja kuhusu biashara ya uwindaji wa kitalii. 

Biashara ya Uwindaji wa Kitalii, Bara la Afrika Liwe Na Sauti Moja!

Dkt. Ndumbaro amezitaka nchi za Afrika kuwa na kauli moja kuhusu taratibu na bei za wanyamapori katika biashara uwindaji wa kiutalii. Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti katika vikao ana kwa ana na baadhi ya mawaziri wa Utalii wa nchi za Afrika katika Mkutano wa 64 wa Kimataifa wa Utalii uliondaliwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Utalii Duniani.

NA MWANDISHI MAALUM, - KISIWA CHA SAL-CAPE VERDE

Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, (UNWTO) limeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuweka mikakati bora ya kuwajengea uwezo watu waliopo katika sekta ya utalii nchini kuanzia Mwezi Juni 2022. Hatua hiyo inakuja kufuatia hali mbaya ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kuidhoofisha sekta ya utalii nchini na Duniani kwa ujumla huku Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikikadiriwa kupata hasara ya dola 4.8 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh. trioni 11) kwenye sekta ya utalii kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 huku watu milioni 21 wakikosa fursa za ajira Akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro katika kikao cha pembeni mwa mkutano wa UNWTO wa 64 wa Kanda ya AfriKa ukilenga kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii hasa katika kipindi ambacho sekta ya utalii inachechemea kutokana na kushambuliwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona-19.   

Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololiskashvil amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa Wadau wa Utalii na ili waweze kuendana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 katika kuendesha shughuli za utalii nchini Tanzania. Mkutano huo wa UNWTO wa 64 wa Kanda ya Afrika umefanyika kwa muda wa siku nne katika Kisiwa cha SAL nchini Cape Verde ambapo uliwakutanisha mawaziri 30 wa utalii Barani Afrika ukilenga kujadili mustakabali wa utalii Barani Afrika na Duniani kwa ujumla kufuatia uwepo wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akiwa na maofisa na Makamishna wa Uhifadhi kutoka TFS na TAWA, maofisa pamoja na Balozi wa Tanzani nchini Ufaransa Mhe, Samuel Shelukindo.

Aidha, Katika kikao hicho Katibu Mkuu amesema mafunzo hayo yatazilenga jamii zinazozunguka vivutio vya utalii ili kuzijengea uwezo wa kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utalii nchini likiwa lengo ni kutengeneza ajira nyingi zaidi kupitia sekta hiyo. Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amemueleza Waziri Dkt.Ndumbaro kuwa UNWTO iko mbioni kuandaa kalenda ya mwaka ya UNWTO ambapo Tanzania nayo itakuwepo katika orodha hiyo kuendana na matukio yatakavyopangwa katika mkutano huo. Amesema moja ya kipaumbele cha UNWTO kwa sasa ni kuitangaza Tanzania na Afrika kwa ujumla Akizungumza katika kikao hicho cha ana kwa ana na Katibu Mkuu huyo, Dkt. Ndumbaro amesema mafunzo hayo yatatoa matumaini kwa Wadau wa Utalii nchini baada ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kuwatikisa. Hata hivyo, Dkt.Ndumbaro amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kwa kufanya vizuri katika shughuli za Uhifadhi lakini katika suala la kujitangaza na kutafuta masoko ya utalii imekiwa haifanyi vizuri hivyo ujio wa mafunzo hayo yataiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika nyanja hiyo. Aidha, Dkt.Ndumbaro amemualika Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurabu Pololikashvil kuja kutembelea vivutio volivyopo nchini Tanzania na kusisitiza kuwa ataambatana naye katika ziara hiyo ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amezitaka nchi za Afrika kuwa na kauli moja kuhusu taratibu na bei za wanyamapori katika biashara uwindaji wa kiutalii. Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti katika vikao ana kwa ana na baadhi ya mawaziri wa Utalii wa nchi za Afrika katika Mkutano wa 64 wa Kimataifa wa Utalii uliondaliwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Utalii Duniani (INWTO) uliofanyika kwa muda wa siku nne nchini Cape Verde. Amesema bei za wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa pamoja na vitalu vya uwindaji wa Wanyamapori zimekuwa zikitofautiana sana kati ya nchi na hali hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli uhifadhi Barani Afrika. Akizungumza katika vikao hivyo vya ana kwa ana na Waziri wa Utalii wa Zimbabwe. Mhe.Ngobhithize Ndlovu  amezitaka nchi hizo kuwa kitu kimoja katika kuamua na kupanga bei za uwindaji wa Kitalii.

Amesema kutokana na kutofautiana kwa bei na baadhi ya kanuni na taratibu hizo Wawindaji wa kiitalii wamekuwa wakitumia mwanya huo kuzikandamiza nchi za Kiafrika kwa kupanga bei wanazotaka wao huku wakidai kuwa bei hizo cha chini zimekuwa katika nchi nyingine pia. Amesema Wawindaji hao wamekuwa wakipanga bei za uwindaji wa kiutalii na sio nchi husika huku wakidai kuwa kama bei hiyo haitawezekana basi watakwenda katika nchi nyingine ambayo utalii wake uwindaji ni bei ya chini zaidi. "Utofauti wetu huu umekuwa ukitukandamiza kama nchi kwani tulitakiwa sisi ndo tupange bei lakini kutokana na kutokuwa na umoja bei za wanyama zimekuwa zimekuwa zikiamuliwa na wao hili lazima tulikatae kwa kuungana kwa pamoja " alisisitiza Dkt.Ndumbaro

Ni katika mukadha huu, Dkt.Ndumbaro amezitaka nchi zote zinazoendesha utalii wa uwindaji zifanye mkutano kwa nji ya mtandao ili kujadili mustakabali wa biashara hiyo na kisha zitoke na kauli moja ili kuwathibiti wawindaji wa kitalii kwa ajili ya maslahi mapana ya uhifadhi barani Afrika. Amezitaja baadhi ya nchi wanachama wa SADC zinazofanya vizuri katika uwindaji wa kitalii kuwa ni Botswana, Zimbabwe pamoja, Zambia na Afrika ya Kusini. Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro ametoa ahadi kwa nchi ya Zimbabwe kama itakuwa tayari ipewe mafunzo ya kuendesha biashara ya uwindaji wa kiutalii kwa mfumo wa kidigitali ambao utasaidia kuongeza mapato maradufu. Amesema tangu kuanzisha kwa mfumo huo nchini Tanzania umeleta manufaa makubwa kwa nchi ambapo Wawindaji wa kitalii ili kuweza kupata vitalu vya uwindaji wamekuwa wakilazika kushiriki katika mnada wa kimtandao.

Naye, Waziri waUtalii wa Zimbabwe Mhe.Ngobhitithize Ndlovu amesema nchi za kiafrika lazima ziungane katika suala hilo kwani katika nchi ya Zimbabwe Wawindaji hao pia wamekuwa wakipanga bei huku wakidai kama hiyo bei haitawezekana watakwenda Tanzania ambako bei vitalu vya uwindaji ipo chini zaidi. Amesisitiza kuwa shughuli za uhifadhi zimekuwa aghali sana huku biashara hiyo ya uwindaji wa kiutalii ukibaki pale pale kutokana na kutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine Naye, Kamishna Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mabula Misungwi amesema umoja huo wa nchi za Kiafrika katika biashara ya vitalu vya uwindaji italiingizia taifa fedha nyingi za kigeni sio kwa Tanzania pekee bali kwa Afrika nzima. "Biashara hiyo imekuwa na ushindani baina yetu bila kujuana kufuatia kila nchi kupanga bei zake kulingana na matakwa ya wadau hao huku shughuli za uhifadhi zikiwa juu zaidi" amesisitiza Kamishna Mabula.

07 September 2021, 11:04