2021.09.13  Katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi  Amina J. Mohammed, nchini Tanzania amepata kuzungumza na Rais Samia Suluhu huko Chamwino Dodoma. 2021.09.13 Katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed, nchini Tanzania amepata kuzungumza na Rais Samia Suluhu huko Chamwino Dodoma. 

Naibu Mkuu wa UN atembelea nchini Tanzania

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed,amefanya ziara maalum ya siku mbili nchini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Miongoni mwa yale yaliyozungumzwa akiwa na rais huko Ikulu Chamwino ni kumpongeza Rais Samia kwa kushika nafasi ya Urais na kumtakia heri katika majukumu yake.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican.

Mapema wiki iliyopita, kiongozi wa Umoja wa Mataifa alifanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania. Huyo alikuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi Ammina Mohammed. Salamu za Katibu Mkuu wa UN, kuunga mkono jitihada za SDG, usawa wa utoaji chanjo ya Uviko, huduma za kiafya kwa mama na mtoto pamoja na maji safi ndizo mada zilizokuwa katikati ya mazungumzo hayo. Kwa mujibu wa taarifa kamili kutoka Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma Tanzania ilibainisha kuwa: Katika ziara yake tarehe 11 Septemba, 2021 Bi. Mohammed amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Chamwino, Mkoani Dodoma. Katika mazungumzo yao  Bi. Mohammed awali ya yote amewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres na kumpongeza Rais Samia kwa kushika nafasi ya Urais na kumtakia kila la heri katika majukumu yake.

Bi Mohammed amemuhakikishia Rais Samia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kumuunga mkono katika jitihada zake mbalimbali za kuiletea maendeleo Tanzania, ikiwemo kufikia malengo ya maendeleo Endelevu (SDGs). Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazochukua dhidi ya janga la UVIKO-19 ambapo amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kuhakikisha kuwepo na usawa wa upatikanaji wa chanjo na wanaendelea na majadiliano na taasisi za Kifedha kuona ni jinsi gani zinasadia nchi zinazoendelea kukabiliana na ugonjwa huo. Bi Mohammed vilevile, ameahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita za kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.

Kwa upande wake Rais Samia amempongeza Bi Amina J. Mohammed kwa kuteuliwa tena kushika nafasi hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumhakikishia ushirikiano zaidi kwa kuwa Umoja wa Mataifa kupitia taassisi zake mbalimbali ni mbia wa maendeleo nchini.  Rais Samia amemueleza kuwa serikali yake inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ambapo katika kipindi cha miezi mitatu idadi ya wawekezaji imeongezeka.

13 September 2021, 15:26