Serikali ya Tanzania itaendelea kumuenzi Marehemu Elias John Kwandikwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Serikali ya Tanzania itaendelea kumuenzi Marehemu Elias John Kwandikwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. 

Serikali ya Tanzania Kumuenzi Hayati Elias John Kwandikwa!

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itatekeleza mipango yote iliyoachwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, marehemu Elias Kwandikwa. Amesema kuwa Serikali itaenzi mipango yake na itahakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni katika Jimbo la Ushetu zinatekelezwa kama alivyoahidi. Amesema hayo Jumatatu Agosti 9, 2021.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kahama, Shinyanga.

Askofu Ludovick Joseph Minde wa Jimbo Katoliki la Moshi na Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Kahama, tarehe 9 Agosti 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya amesema marehemu Elias John Kwandikwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa. Amesema, Waziri Kwandikwa alikuwa ni mnyenyekevu, mwenye busara, hekima na mpenda maendeleo. Aidha, Askofu Minde aliongeza kuwa marehemu Kwandikwa alikuwa mfadhili mkubwa katika maendeleo ya kiroho na kimwili. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itatekeleza mipango yote iliyoachwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, marehemu Elias Kwandikwa.  Amesema kuwa Serikali itaenzi mipango yake na itahakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni katika Jimbo la Ushetu zinatekelezwa kama alivyoahidi. Amesema hayo Jumatatu Agosti 9, 2021 alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya marehemu Kwandikwa kijijini kwao Butibu, Ushetu, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania, wana-Shinyanga na wana-Ushetu waenzi mambo yote mazuri yaliyoachwa marehemu Kwandikwa. “Tumepoteza kiongozi aliyekuwa anaongoza majeshi yetu, amefanya kazi nzuri sana katika kipindi chote cha uhai wake alipokuwa anaitumikia Serikali; marehemu alikuwa mwadilifu, muwajibikaji na aliyefanya kazi kwa weledi mkubwa.” Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wabunge, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa George Simbachawene amesema marehemu Kwandikwa alikuwa ni kiongozi ambaye alitekeleza majukumu yake sawasawa na alihakikisha matokeo yanaonekana. Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Faraji Mnyepe amesema marehemu Waziri Kwandikwa ameondoka wakati wizara ikiwa inamuhitaji kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka. “Marehemu Waziri Kwandikwa alikuwa ni kiongozi mwenye upendo wa hali ya juu na alikuwa mtenda haki kwa kila mtu.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo amesema marehemu Waziri Kwandikwa alikuwa ni mtu wa kipekee, msikivu na mnyenyekevu. Amesema kuwa marehemu Waziri Kwandikwa, alikuwa ni mwepesi wa kujifunza mambo ya kijeshi na alilisaidia jeshi kwa kadri ya uwezo wake katika kipindi chote alichokuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. “Alikuwa ni kiongozi asiyependa kukaa muda mwingi ofisini bali aliwatembelea makamanda maafisa katika maeneo yao ya kazi ili kuona utendaji kazi na changamoto zinazowakabili.” Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo amesema marehemu Waziri Kwandikwa ameacha pengo kwani katika kipindi chote amekuwa na mchango mkubwa ndani ya Serikali, CCM na wananchi wa ushetu na Watanzania kwa ujumla.  “Tumepoteza kiongozi hodari, mahiri na CCM tumepoteza mtu aliyekipenda chama kwa moyo mkuu. Mwenyezi Mungu aendelee kuwa mfariji kwa familia, wana-Ushetu, wana-Shinyanga na Watanzania kwa ujumla.” Marehemu Waziri Elias Kwandikwa alizaliwa Julai 7, 1966 wilayani Kahama, Shinyanga na alifariki Agosti 2, 2021 katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 06 Agosti, 2021 aliwaongoza viongozi mbalimbali na waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Marehemu Elias John Kwandikwa. Akizungumza wakati akitoa salamu za pole, Mhe. Rais Samia amesema kifo cha marehemu Kwandikwa kimeacha simanzi na pengo kubwa si kwa familia pekee bali pia kwa Serikali na Taifa kwa ujumla. Amesema Serikali imempoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini, shupavu na mchapakazi hodari. Aidha, Mhe. Rais Samia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuongoza ibada ya kumuaga marehemu Kwandikwa ambapo mahubiri yao yametoa faraja na kukumbusha kuwa wanadamu duniani wanapita, hivyo kutakiwa kuishi kwa wema na kutenda yale ya kumpendeza Mungu. Shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Kwandikwa zimefanyika katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga, Katibu Mkuu Kiongozi-Zanzibar Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine wa vyama vya Siasa na Serikali. “Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe”

10 August 2021, 11:40