FAO: Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo vijijini. FAO: Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo vijijini. 

Mkutano wa Utangulizi wa Mifumo ya Chakula Roma: Kilimo Vijijini

FAO: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo vijijini pamoja na kutekeleza kwa vitendo sera na mikakati mbalimbali ya kupambana na baa la njaa duniani. Jumla ya watu milioni 811 waliathirika kwa baa la njaa duniani katika kipindi cha mwaka 2020, ikilinganishwa na idadi ya watu milioni 161 waliopekenywa kwa baa la njaa katika kipindi cha Mwaka 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Bwana António Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa  ametuma ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano wa utangulizi wa Mifumo ya Chakula mjini Roma, tarehe 27 Julai 2021 ili kuzishawishi nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba zinaweka mifumo mizuri zaidi ya chakula ili kuhakikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu “SDGs” yanafikiwa mwaka 2030. Madhara makubwa yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yanaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika baa la umaskini, njaa na utapiamlo wa kutisha kwa watoto. UVIKO-19 imesababisha ukosefu wa uwiano wa huduma ya afya hasa katika nchi zinazoendelea duniani. Ni matumaini ya Umoja wa Mataifa kwamba, mikutano hii ya utangulizi, itaisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupata suluhu ya changamoto ya kashfa ya baa ya njaa na umaskini sanjari na ukosefu wa huduma bora za afya. Lengo kuu la Umoja wa Mataifa ni kuendelea kujizatiti katika mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030.

Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, inajizatiti zaidi katika mchakato wa kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umepelekea watu zaidi milioni 130 kutumbukia katika baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Kwa upande wake Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo vijijini pamoja na kutekeleza kwa vitendo sera na mikakati mbalimbali ya kupambana na baa la njaa duniani. Jumla ya watu milioni 811 waliathirika kwa baa la njaa duniani katika kipindi cha mwaka 2020, ikilinganishwa na idadi ya watu milioni 161 waliopekenywa kwa baa la njaa katika kipindi cha Mwaka 2019. Janga la UVIKO-19 limepelekea kushuka kwa pato la wakulima vijijini.

Umoja wa Mataifa

 

 

 

 

28 July 2021, 15:24