Tafuta

2021.03.07:Siku ya wanawake kimataifa:Harakati za kujikwamua wajane wa kijiji cha Rwabwere na Iteera-Kyerwa,Tanzania 2021.03.07:Siku ya wanawake kimataifa:Harakati za kujikwamua wajane wa kijiji cha Rwabwere na Iteera-Kyerwa,Tanzania  

Siku ya Wanawake Duniani:machungu yapo wanayopitia katika maisha!

Katika Siku ya Wanawake Duniani,tutazame jinsi gani wengi wanapitia machungu,mahitaji yao na majukumu msingi wanayobeba katika jamii zao ambazo mara nyingi hazina suluhisho.Ni wakati sasa wa kutambua kuwa tofauti kubwa huchochea ubunifu mkubwa.Tunahitaji wanawake katika masuala ya yote ya Sayansi,Teknolojia,Uhandisi na Hesabu ili dunia isiendelee kuwa na ubunifu kutoka kwa wanaume tu.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican.

Katika kuelekea  kilele cha Siku ya Wanawake Duniani 2021, tarehe 8 Machi, tutazame ni jinis gani wanawake wengi wanapitia machungu, mahitaji yao na dhima muhimu na ya msingi wanayobeba katika jamii zao ambazo mara nyingi hazipati suluhisho. Pamoja na kwamba nchi nyingi zimejumuisha tayari usawa wa kijinsia kwenye katiba zao lakini bado wanawake wanazidi kupitia dhuluma wakiwa nyumbani na kwenye maeneo ya kufanyia kazi.  Kutokana na kwamba serikali hazihakikisha vya kutosha  kuwepo kwa usawa wa kijinsia umepelekea hadi sasa mamilioni ya wanawake  duniani kuendelea kukumbwa na ukosefu wa haki hizo  msingi na usawa kazini, manyanyaso ya manyumbani mwao na kwenye maisha yao ya kawaida kwa ujumla. Mara nyingi mifumo dume inajidhirihisha wazi, lakini pia ipo ya kisiri siri, illiyo jifunika ngozi ya kondoo, wakati ndani ni mbwa mwitu. Wanawake wengi wanavumilia kwa kutotaka kuvunja heshima na kumbe matokeo ni vitendo vya ukatili wa kuvuka mipaka hadi kufika mauti ya kila siku.

Katika ujumbe wa siku kama hii mwaka jana, 2020, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa wa masuala ya wanawake UN Women Bi. Phumzile Mlambo-Ngukca katika ujumbe wake wa siku ya wanawake duniani alikuwa amesema kwamba kaulimbiu ilikuwa inahusu kizazi chenye usawa ambacho kinajikita na masuala  yanayowakabili wanawake na wasichana vizazi na vizazi. Bi Ngukca aliongeza alisema “hatuna usawa duniani hivi sasa na wanawake wanaghadhibishwa na kutiwa hofu na mustakbali wao, kimsingi hawana uvumilivu tena na mabadiliko na ni kitu ambacho kimetawala maisha yao kwa muda mrefu.” Alisisitiza kuwa “wasichana wanahudhunishwa na hali ya dunia yetu, ukatili unaoelekezwa kwao na kasi ndogo ya mabadiliko katika masuala yanayowahusu kama elimu”  Vile vile alisema kuwa  sera zinahitajika ambazo zinachagiza usawa katika huduma za msingi za kuhudumia watoto na kuhudumia familia lakini pia kwa wanaofanya kazi katika sekta zisizorasmi.

Katika muktadha wa siku hii ka hakika inapiga picha ya halisi ya kile ambachomwanamke katika mataifa yote yawe yanayoendelea na yaliyoendelea inajionesha bayana. Wanawake kwa mfano vijijini mara nyingi wanakosa ulinzi wa kijamii na kisheria katika maisha yao yote, ahata kwa mapato na akiba ya wajane mara nyingi ni ndogo. Katika nchi nyingi wanajane hawana haki za kurithi kama wanaume, hii ikimaanisha kwamba wanaweza kunyang’anywa ardhi na  vitu, na hata haki na fursa za kuwa na watoto wao. Hata katika sehemu ambazo sheria haibagui, haki hizo zinapaswa kutekelezwa na kutumia sawa. Na isitoshe katika baadhi ya jamii wajane wengi hutengwa, hunyanyaswa na kufanyiwa ukatili ikiwemo ukatili wa kingono, kudhalilishwa na kuingizwa katika ndoa za shuruti. Kwa hakika siku hii ya wanawake lazima hata wajane watazamwe kwa umakini na wasaidiwe wote bila kujali umri, mahali  waliko au mfumo wa kisheria ili kuhakikisha kwamba hawaachwi nyuma.

Watoto wao wanawategemea, na inasitikitisha kuona jamii wakati mwingine inaonesha thamani ya mwanamke mwenye mume, wakati ujane unaweza hata kumlazimisha mwanamke awe nje ya mfumo wa familia au kabila na kumuacha katika hali ya kutojiweza akikabiliwa na changamoto nyingi kama umaskini, upweke na kutengwa. Siku ya Kimataifa ya wanawake kwa maana hiyo inagusa kila mantiki ya kijamii.Na wakati huo huo, siku hii inaangazia bidi ya wanawake ambayo inaafanywa kwa ajili ya kulinda Maisha, kusaidia jamii, kuwa mstari wa mbele katika ngazi ya maamuzi, kwenda madaraka na kila sekta yoyote. Ni kuhimiza bidii ya kazi na malezi bora ya watoto ambao ni kizazi kijacho.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila tarehe 8 Machi ya kila mwaka. Siku hiyo ilianza kuadhimishwa tarehe 8 Machi 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuridhia siku hii kutumika kama siku rasmi ya kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake. Siku ya wanawake duniani kwa mara wa kwanza ilisherehekewa katika mwaka 1911 ambapo mataifa kumi na moja yalikusanya wanawake mia moja walipoanza kuadhimisha siku hii. Mwaka 1908 jumla ya wanawake elfu kumi na tano waliandamana katikakatika mji wa New York wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, kupata ujira wa kuridhisha na kupewa haki ya kupiga kura. Mwaka 1909 mwanamke kwa jina la Clara Zetkin alipendekeza kuanzishwa kwa siku ya wanawake duniani katika mkutano wa wafanyakazi wanawake uliofanyika katika jiji la Copenhagen nchini Denmark.

Mara kadhaa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekuwa akihamasisha usawa wa jinsia katika Nyanja mbali mbali kuanzia ya kilimo hadi kufikia teknolojia ya sasa kwa ajili ya kujenga mustakabali bora zaidi kwa wote. Ni wakati  sasa wa kutambua kuwa tofauti kubwa huchochea ubunifu mkubwa! Bila kuwa na wanawake kwenye Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu, dunia itaendelea kuwa na ubunifu kutoka kwa wanaume, na uwezo wa wanawake na wasichana utasalia kufichika na bila kutumika. Ni lazima kuhakikisha wasichana wana fursa ya elimu wanayopaswa kuwa nayo na wanajiona kwenye mustakabali wautakao wenyewe iwe uhandisi, programu za kompyuta, teknolojia ya roboti au hata sayansi ya afya. Haitoshi kuwavutia wanawake kwenye nyanja ya sayansi au teknolojia, tunapaswa pia kuhakikisha wanabakia humo na kuhakikisha ajira zao hazikumbwi na vikwazo na kwamba mafanikio yao yanatambuliwa na kuungwa mkono na jamii ya kimataifa ya sayansi, kwa mujibu wa UNESCO.

07 March 2021, 18:40