2018-02-06  Wanawake wa kiafrika 2018-02-06 Wanawake wa kiafrika  

Covid-19 imezidisha janga la ukatili wa kijinsi dhidi ya wanawake na mfumo dume duniani

Kuna hatari ya kuendelea kwa utawala wa mfumo dume katika maisha ya umma na kuna umuhimu kwa wanawake kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi.Ni katika hotuba ya Katibu Mkuu wa UN Bwana Guterres ambapo amethibtisha mabadiliko yanayofanywa katika Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha usawa wa kijinsia katika shirika hilo.Amesema hayo katika Kamishna ya hali ya wanawake duniani iliyofunguliwa kikao cha 65 jijini New York.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Wakati wanawake wanakosekana katika kufanya maamuzi, tunaona ulimwengu kupitia mtazamo mmoja tu. Tunaunda mifano ya kiuchumi ambayo inashindwa kupima kazi yenye tija inayofanyika nyumbani. Kuna hatari ya kuendelea kwa utawala wa mfumo dume katika maisha ya umma, na kwa nini ni muhimu sana kwa wanawake kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi. Amesema hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika Mkutano wa kamisheni ya hali ya wanawake  duniani kwenye kikao cha 65 kilichofunguliwa tarehe 15  na kitahitimishwa 26 Machi 2021 ikiwa ni mara ya pili kufanyika katika mazingira ya janga la virusi vya corona au covid-19 na hivyo sehemu kubwa ya ushiriki ni kwa njia ya mtandaoni. Katibu Mkuu akiendelea amesema  janga hili lina sura ya mwanamke akisema na kwamba hali ya sasa imedhihirisha jinsi ukosefu wa usawa wa kijinsi ulivyo kwa kiasi kikubwa na umekita mizizi katika mifumo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Asilimia 24 ya wanawake wako hatari ya kupoteza kazi

Bwana Guterres amesema wanawake ni asilimia 70 ya wahudumu wa afya ulimwenguni kote na wanafanya kazi katika sekta nyingi za kiuchumi zilizoathirika vibaya wakati wa janga hili.  Ikilinganishwa na wanaume, wanawake asilimia 24 zaidi wako katika hatihati ya kupoteza kazi zao, na wanaweza kutarajia mapato yao kuanguka kwa asilimia 50 kwa kasi zaidi. Kazi ya utunzaji na huduma za bila malipo kwa wanawake na wasichana zimeongezeka sana kwa sababu ya masharti ya kusalia nyumbani, kufungwa kwa shule na vituo vyakulelea watoto, kuongezeka kwa utunzaji wa wazee na mengi mengineyo. Amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Janga la ukatili wa kingono hadi ndia za utotoni

Katibu wa Umoja wa Mataisa meongeza kusema kuwa janga la COVID-19 pamoja na mambo mengine vimezidisha janga la ukatili wa kijinsi dhidi ya wanawake kote ulimwenguni kwenye mitandao na kwingineko na kwamba, ni tatizo linaongezeka kila mwezi kuanzia ukatili wa kingono hadi ndoa za utotoni na kwamba, sasa ndiyo wakati wa kubadili mkondo na ushiriki wa wanawake katika mizani sawa ndio mabadiliko tunayohitaji.”  Hii ni pamoja na kuweka wanawake wengi katika nafasi za uongozi wa juu, kufikia usawa wa kijinsia katika viwango vya usimamizi wa juu, na kujitahidi kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika kulinda amani, upatanishi na mchakato wa ujenzi wa amani. Bwana Guterres aidha ameongeza "Tunahitaji kupiga hatua zaidi ya kurekebisha wanawaka, na badala yake turekebishe mifumo yetu. Kujikwamua na janga la COVID-19 ni fursa kwetu ya kupanga njia ya mustakabali wenye sawa. "

Mambo matano ya kuleta usawa wa kijinsia

Katibu Mkuu amependekeza hatua tano ambazo viongozi wa ulimwengu wanaweza kuzichukua ili kusongesha mbele mchakato wa usawa wa kijinsia. 1)Kutambua kikamilifu haki sawa za wanawake: pamoja na kufuta sheria za ubaguzi na kuchukua hatua nzuri. 2) Kuhakikisha uwakilishi sawa: kuanzia kwenye bodi za makampuni hadi kwenye mabunge, kutoka kwenye elimu ya juu hadi taasisi za umma kupitia hatua maalum na nafasi za upendeleo. 3) Kuendeleza ujumuishaji wa wanawake kiuchumi:  kupitia malipo sawa, mikopo inayolenga wanawake, ulinzi wa ajira zao na uwekezaji mkubwa katika uchumi wa hifadhi na ulinzi wa jamii. 4) Kuweka mpango wa dharura wa kukabiliana na majanga katika kila nchi ili kushughulikia unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, na kufuatili hilo kupitia ufadhili, sera, na utashi wa kisiasa. 5) Kutoa fursa za mpito kwa vizazi vinavyoendelea.

Wanawake wamezingirwa na ukatili wa kijinsia

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka, katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa kikao hicho amesema kwamba wale walioathiriwa zaidi na janga la COVID-19 ni wale ambao hawawezi kuhimili. Kwa sababu ya janga hilo , Bi Mlambo-Ngcuka, amesema “wanawake milioni 47 zaidi wamesukumwa kuishi kwa umaskini wa chini ya dola $ 1.90 kwa siku, wasichana milioni 10 zaidi wanatarajiwa kuwa katika hatari ya ndoa za utotoni katika miaka kumi ijayo, na wanawake wamezingirwa na unyanyasaji wa kijinsia , wanaoathirika na viwango vya juu zaidi vya unyanyasaji kutoka kwa wenzi wao wa karibu zaidi kuwahi kuonekana, katika miezi 12 iliyopita.”

Uwakilishi duni wa wanawake ni sababu ya maendeleo duni pia

Kwa kuongezea, amesema unyanyasaji dhidi ya wanawake katika maisha ya umma ni kikwazo kikubwa kwa ushiriki wao wa kisiasa, na huathiri wanawake katika sehemu zote za ulimwengu. “Uwakilishi duni wa wanawake ni sababu ya maendeleo ya polepole katika nyanja zote za usawa wa kijinsia”. Bi. Mlambo-Ngcuka amewahimiza wajumbe katika kikao hicho kuzingatia vipaumbele, na kuhakikisha kuwa wanawake wana nafasi yao katika meza kuu ya majadiliano, na kuongeza kuwa haiwezekani hali hiyo kuweza kushughulikiwa, bila wanawake wenyewe kushiriki katika kufanya maamuzi.

Rais wa ECOSOC na Rais wa Baraza Kuu

Rais wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa  (ECOSOC), Munir Akram, na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Volkan Bozkir, pia wamezungumza katika ufunguzi wa kikao hicho. Bwana Akram amesema kuwa sauti za wanawake katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinaendelea kunyamazishwa, huku kukiwa na ubaguzi na vurugu zilizoenea. Ameongeza kuwa “wanawake na wasichana wanakabiliwa na vizuizi vingi, ikiwa ni pamoja na mizozo, ugaidi, majanga ya asili, na ukosefu wa usawa wa mafunzo na ajira.”. Mkuu wa ECOSOC ametangaza kuwa maendeleo endelevu hayawezekani ikiwa wanawake wataendelea kutengwa, na ametaka muungano mpya wa kimataifa wa kuwawezesha wanawake, na kuondoa aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.

Hakuna mwanamke anayepswa kuhisi kuogopa

Naye Bwana Bozkir Rais wa Baraza Kuu kwa upande wake ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kadhaa thabiti, pamoja na kuimarisha sheria dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia; kuanzisha mifumo ya kuripoti na kurekebisha mchakato kwa ajili ya waathirika, na kujitolea kwa ufuatiliaji wa vurugu.”Hakuna mwanamke anayepaswa kuhisi haja ya kuhalalisha uwepo wake au kuogopa kujieleza. Hakuna mwanamke anayepaswa kutishiwa, kulipwa mshahara mdogo, au kudharauliwa”, amesisitiza Rais huyo. Katika Kikao hiki cha 65 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani kitakacho malizika tarehe  26 Machi, kinahusisha vikao halisi, lakini sehemu kubwa ni kupitia mtandaoni na UN Women, ni shirika la Umoja wa Mataifa linalofanya kazi kuharakisha usawa wa kijinsia ulimwenguni, kwa kushirikiana na wadau wengine, mashirika na asasi za kiraia.

16 March 2021, 15:37