Waziri mkuu Kassim Majalia ametoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa Pili wa Bunge la kumi na mbili tarehe 13 Februari 2021. Waziri mkuu Kassim Majalia ametoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa Pili wa Bunge la kumi na mbili tarehe 13 Februari 2021. 

Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi na Mbili Umeahirishwa Tanzania

Waziri mkuu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Shughuli za Bunge, Utekelezaji wa mpango wa Bajeti ya Serikali 2020-2021; Elimu, Kilimo, Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi hasa uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo, maarufu kama "wamachinga", Michezo! Bila shaka hapa washabiki wa Timu ya Soka ya Simba, wamesikia "Neno la Waziri mkuu" bila kusahau "Visit Tanzania".

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma, Tanzania.

UTANGULIZI 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema hadi leo hii tunapohitimisha shughuli zote zilizopangwa katika Mkutano huu wa Pili wa Bunge la Kumi na Mbili.

2.                 Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naungana tena na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salamu za pole kwa Bunge lako Tukufu na kwa familia za waliokuwa Wabunge, Mheshimiwa Martha Umbula Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara na Mheshimiwa Atashasta Nditiye, Mbunge wa Muhambwe waliotangulia mbele za haki wakati wakiendelea kulitumikia Taifa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao kwa amani.

3.                 Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wenzangu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na wengine kusababishiwa madhara mbalimbali kutokana na ajali za barabarani na matukio mengine. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe subra na awape nafuu majeruhi wetu wapone haraka.

4.                 Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana wewe binafsi, Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa majadiliano ya hoja kuhusu kujadili Hotuba ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati akifungua Bunge la Kumi na Mbili sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

5.                 Mheshimiwa Spika, ninawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu yenye dhamira ya dhati kabisa ya kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika kipindi chote cha miaka mitano. Mjadala huu umeendelea kuthibitisha uimara wa Bunge katika kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba wa kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu.

SHUGHULI ZA BUNGE: Maswali na Majibu

6.                 Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge 164 na Mawaziri saba walichangia hoja ya kujadili Hotuba ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati akifungua Bunge la Kumi na Mbili. Aidha, Waheshimiwa Wabunge 126 walichangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

7.                 Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 125 ya msingi na mengine 289 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali. Kadhalika, maswali 14 ya papo kwa papo yaliulizwa na kujibiwa na Waziri Mkuu.

Kamati za Kudumu za Bunge

8.                 Mheshimiwa Spika, natambua kuwa shughuli za utangulizi za Mkutano huu zilianza tarehe 18 hadi 31 Januari 2021 kwa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge sambamba na Chaguzi za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. Hivyo, nitumie fursa hii kuwapongeza wajumbe wote kwa kufanikisha upatikanaji wa viongozi wa Kamati hizo ambao wameaminiwa na kuchaguliwa kuongoza Kamati zetu.

9.                 Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba tutatumia nafasi hizo vizuri katika kuleta ushirikiano, mshikamano na kufanya kazi pamoja kama wawakilishi wa wananchi na kutekeleza majukumu yetu kwa kuisimamia na kuishauri Serikali.

10.            Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake, itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kamati hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi na uwajibikaji hususan wakati huu tunapoelekea kwenye maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2021/2022.

11.            Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu Mawaziri kwa kujibu vizuri pamoja na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge.

Miswada ya Serikali

12.            Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 uliowasilishwa na Serikali katika Mkutano huu. Aidha, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa Mwaka 2021 (The Accountants and Auditors (Registration) (Amendment) Act, 2021) pamoja na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2021 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.2) Act, 2021) ilisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano huu.

13.            Mheshimiwa Spika, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 ambao kwa msingi wake ulikusudia kufanya marekebisho katika Sheria ya Tafsiri ya Sheria (Sura ya 1), Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Sura ya 11) na Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi (Sura ya 216). Lengo la marekebisho hayo ni kuweka msingi wa lugha ya Mahakama, Mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki kuwa ni Kiswahili badala ya Kiingereza kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa, lugha ambayo inaeleweka na inatumika katika shughuli zote za kijamii na za maendeleo nchini.

14.            Mheshimiwa Spika, marekebisho haya yataimarisha mfumo wa upatikanaji haki kwa wananchi ambao wanakusudiwa kuzitumia sheria husika. Serikali itafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa nanyi Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unawanufaisha wananchi wote hapa nchini.

Mjadala wa Hotuba ya Rais

15.            Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu moja ya agenda iliyochukua nafasi kubwa ni hoja ya Serikali ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo tuliihitimisha vizuri na kwa mafanikio makubwa.

16.            Mheshimiwa Spika, kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kutekeleza yale tuliyokusudia kama wajibu wetu. Hivyo basi, nitumie tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako tukufu kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa utekelezaji.

Mpango wa Taifa wa Maendeleo

17.            Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili kuhusu tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017-2020/2021), kujadili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022-2025/2026) pamoja na kutoa maoni na ushauri kuhusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

18.            Mheshimiwa Spika, kipekee, naomba nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.), Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuwasilisha vizuri Mpango mbele ya Bunge lako pamoja na Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis (Mb.) Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ufafanuzi mzuri walioutoa wakati wa kuhitimisha hoja hii.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2020/2021 KATIKA NUSU YA KWANZA JULAI – DESEMBA 2020

19.            Mheshimiwa Spika, Juni, 2020 Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi trilioni 34.88 ikiwa ni bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021. Kiasi hicho kinajumuisha, shilingi trilioni 22.10 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.78 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

20.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020, ridhaa ya matumizi iliyotolewa ilikuwa shilingi trilioni 13.12 sawa na asilimia 82.8 ya lengo. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 10.52 ni fedha za matumizi ya kawaida sawa na asilimia 95.2 na shilingi trilioni 2.60 ni fedha za maendeleo sawa na asilimia 54.2.

21.            Mheshimiwa Spika, kwa upande wa fedha za maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 730.7 kutoka kwa washirika wa maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi na hivyo kufanya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kufikia asilimia 69.4. Kadhalika, kiasi cha shilingi bilioni 254.6 kilitumika kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa ya watumishi, makandarasi na watoa huduma.

Mfumuko wa Bei

22.            Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nchini umeendelea kuwa tulivu na kubakia katika viwango vya chini. Kwa mfano, mfumuko wa bei kwa Desemba 2020 ulikuwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na asilimia 3.8 Desemba 2019. Kwa hiyo, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021, mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 3.2, ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.0.

23.            Mheshimiwa Spika, kiwango hicho cha mfumuko wa bei kilitokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha katika masoko ya ndani na nchi jirani, bei ndogo ya mafuta kwenye soko la dunia, utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani, na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti.

Mafanikio, Changamoto na Mikakati katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021

24.            Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu, Bunge lako tukufu lilipokea na kujadili mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026.

 

25.            Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mipango hiyo kwa kipindi cha mwaka 2021/2022, nami nitumie nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote baadhi ya mambo makubwa na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2020/2021.

26.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 (yaani Julai hadi Desemba 2020) yapo mafanikio mengi yaliyopatikana. Kadhalika, zipo changamoto zilizoibuka na kuifanya Serikali kuja na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo katika kipindi cha miezi sita ya pili ya mwaka ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2020/2021.

27.            Mheshimiwa Spika, niruhusu japo kwa uchache nieleze baadhi ya mafanikio machache yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021. Aidha, baadhi ya mafanikio ni muendelezo wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

28.            Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo ni pamoja na Serikali kugharamia kwa mara ya kwanza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kutumia fedha za ndani ambapo shilingi bilioni 268.5 zilitumika. Serikali pia ililipa shilingi bilioni 254.6 madeni ya wazabuni na watumishi yaliyohakikiwa; shilingi trilioni 3.64 mishahara ya watumishi; shilingi bilioni 124.8 kwa ajili ya kugharamia sera ya elimumsingi bila ada na shilingi bilioni 105.1 kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, uimarishaji wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) na kukuza ujuzi kwa vijana.

29.            Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kama ifuatavyo: -

 i.            Ujenzi wa Reli ya Kati Kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 49.2. Aidha, tayari Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km 133). Shilingi bilioni 274.1 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021. Baada ya kukamilika matengenezo hayo, tutaanza kuunganisha vipande vya Tabora - Kigoma na Tabora – Mpanda.

     ii.            Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115): Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 25.8 ambapo shilingi bilioni 128.9 zimetumika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021;

 iii.            Kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania: Serikali imekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa ndege aina ya Bombadier Dash 8-Q400 na Boeing 787-8 Dreamliner na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege tatu (3), ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni Dash 8-Q400 De-Havilland na hivyo kuwezesha Serikali kuwa na ndege mpya 11 kutoka ndege moja (1) iliyokuwepo mwaka 2015 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12 ambapo ndege tatu (3) zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/2022 ili ziweze kutoa huduma. Shilingi bilioni 2.8 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021;

   iv.            Viwanja vya Ndege na Rada: Kukamilika kwa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) chenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka; kuendelea na ujenzi wa viwanja vya Geita (asilimia 86), Songea (asilimia 91) na Mtwara (asilimia 49.0); kukamilika kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni 759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga vinavyogharimu Euro milioni 50 sawa na shilingi bilioni 136.85; kuanza kwa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege Musoma; kukamilika kwa ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege na kununuliwa kwa magari mapya matatu (3) ya zimamoto yenye uwezo wa kubeba lita za maji 10,000 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA); kupanuliwa kwa barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege cha Dodoma; kufungwa kwa mifumo ya kuongoza ndege (AGL) katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Tabora na Mwanza; na kupanuliwa na kukarabatiwa kwa viwanja vya ndege vya Bukoba, Mwanza, Arusha, Nachingwea na Iringa. Shilingi bilioni 4.5 zimetumika  katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021;

     v.            Usambazaji wa Umeme Vijijini kupitia mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini na makao makuu ya wilaya (REA - III): Hadi Desemba 2020, jumla ya vijiji 10,018 kati ya vijiji 12,317 sawa na asilimia 81.3 vilikuwa vimeunganishiwa umeme ambapo katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2020/21 shilingi bilioni 171.9 zimetolewa na kazi inaendelea;

   vi.            Kuboresha usafiri wa abiria na mizigo katika Maziwa Makuu:

Ziwa Victoria: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo; kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza; kupatikana kwa mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa meli za MV Umoja na MV Serengeti; kukamilika ukarabati wa meli za MV. Clarias na ML. Wimbi.

Ziwa Tanganyika: kukamilika kwa mikataba kwa ajili ya Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba; na ukarabati wa meli ya MT Sangara kwenye Ziwa Tanganyika ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021 shilingi bilioni 12.8 zimetumika. Tumeboresha bandari za Kibirizi, Sibwesa, Kagunga, Kabwe, Kasanya na sasa tunajenga bandari Kalema ambapo shilingi bilioni 86.4 zimetumika.

Shughuli nyingine zilizokamilika ni: Ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero; ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; ukarabati wa majengo na ofisi za bandari za Ziwa Victoria; kuboresha eneo la kushukia abiria Mwanza North; na ukarabati wa ‘Link Span’ ya bandari ya Mwanza South;

Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja; na ujenzi wa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 umekamilika na imeanza kufanya kazi. Shilingi bilioni 1.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021;

vii.            Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,208.62 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka 2019/2020 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa. Ujenzi huu umeongeza uwiano wa mtandao wa barabara za lami nchini kutoka asilimia 6.8 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 8.9 mwaka 2019/2020;

viii.            Uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba - Dodoma: Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba yatakayotosheleza watumishi wote. Katika mwaka 2019/2020, Serikali imekamilisha usanifu wa majengo husika. Aidha, mradi wa ujenzi wa barabara (km 51.2) kwa kiwango cha lami katika Mji wa Serikali utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni 89.13 unaendelea, ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 13.21 yamefanyika na ujenzi umefikia asilimia 56;

   ix.            Miradi ya Vivuko: Kukamilisha ujenzi wa vivuko vipya vya Kigongo - Busisi (Mwanza), Bugolora – Ukara (Mwanza) na Kayenze – Bezi (Mwanza). Aidha, ujenzi wa kivuko kipya cha Nyamisati – Mafia (Pwani) na Chato – Nkome (Geita) umekamilika. Vilevile, ujenzi wa boti mpya tano (5) za uokozi kwa ajili ya kisiwa cha Ukerewe (Ilugwa, Nafuba na Gana), kivuko cha Magogoni – Kigamboni na Lindi – Kitunda unaendelea. Pia, ukarabati mkubwa wa MV Kigamboni umekamilika na ukarabati wa kivuko MV Sengerema umefikia asilimia 90;

 x.            Mifugo: Kujenga kiwanda kipya cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Ltd chenye uwezo wa kuzalisha jozi na soli za viatu 1,200,000 kwa mwaka na kuchakata ngozi futi za mraba 13,000,000 kwa mwaka; kuimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC kilichopo USA River, Arusha kwa kununua kifaa (Chiller) kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha kimiminika cha naitrojeni; kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati vya nyama vya Tanchoice (Pwani), Elia Food Oversees Limited (Arusha) na Binjiang Company Limited (Shinyanga); kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverage Company Limited (Arusha); kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience Africa Limited (Pwani) chenye uwezo wa kuzalisha chanjo aina 37; na kuendelea kuboresha huduma za malisho ya mifugo na majosho.

   xi.            Uvuvi: Kuongezeka kwa uzalishaji/uvunaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 362,645 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.48 mwaka 2015/2016 hadi tani 497,567 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 2.34 mwaka 2019/2020; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara kutoka tani 23,000.58 mwaka 2015/2016 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/2020; kuongezeka kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda masoko ya Ulaya ambapo katika mwaka 2019/2020, jumla ya kilo 777,750.0 za mabondo zilisafirishwa; kuongezeka kwa mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 379.25 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 506.24 mwaka 2019/2020; na kuendelea na maandalizi ya ujenzi wa bandari ya uvuvi (Mbegani). Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021 shilingi milioni 606.7 zimetumika;

 

xii.            Miradi ya Maji: Kukamilika kwa miradi 1,423 ya maji iliyotekelezwa mijini na vijijini. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika kwa miradi ya maji katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 90); utekelezaji wa mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega umefikia asilimia 98; kukamilika kwa asilimia 76 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Mwanza; kukamilika kwa asilimia 62 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Arusha; na kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji  wa Same – Mwanga – Korogwe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65. Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na umehusisha maeneo ya Kibamba hadi Kisarawe, Mlandizi hadi Chalinze, Kisarawe-Pugu-Ukonga, Mkuranga-Vikindu, Jet-Buza, Kisarawe, Kigamboni, Mkuranga, Chalinze, Mbezi Luis hadi Kiluvya, Tegeta, Wazo, Madale, Mivumoni, Mabwepande na Bagamoyo (maeneo ya Vikawe, Zinga, Mapinga na Kerege).

Kwa ujumla miradi yote iliyotekelezwa imewezesha wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma ya maji ambapo wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama  imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020 kwa mijini na kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 70.1 mwaka 2020 kwa vijijini. Aidha, kwa Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa maji safi umeongezeka kutoka asilimia 72 mwaka 2015 hadi asilimia 90 Desemba, 2020. Shilingi bilioni 226.7 zimetumika katika nusu ya kwanza ya 2020/2021. Kazi ya usambazaji maji vijijini inaendelea;

xiii.            Afya: Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya ambayo imefikia hatua mbalimbali ikiwemo: asilimia 98 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala; Ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Rufaa Njombe umefikia asilimia 73; ujenzi wa jengo la mama na mtoto, upasuaji, radiolojia na maabara katika Hospitali ya Rufaa Simiyu umefikia asilimia 50. Shilingi bilioni 64.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya afya, ununuzi wa vifaa, vitendanishi, dawa na chanjo; na

xiv.            Miradi ya Kimkakati ya Kuongeza Mapato Katika Halmashauri: Katika kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaongeza mapato kwa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao, Serikali ilitoa shilingi bilioni 91.4 kwa ajili ya kugharamia miradi 26. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 50.6 zilitolewa mwaka 2019/2020. Miradi ya ujenzi iliyotekelezwa ni pamoja na; stendi za mabasi (9), machinjio (2), viwanda vidogo (3), maegesho ya malori (2), masoko (9) na ghala la mazao (1). Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2020/2021, Serikali imetoa shilingi bilioni 19.9 kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati;

30.            Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio hayo makubwa ambayo nimejaribu kueleza kwa uchache, vilevile, katika utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021, zipo changamoto kadhaa zilizojitokeza. Changamoto hizo ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara uliosababishwa na mafuriko; kupungua kwa shughuli za kibiashara duniani kutokana na athari za mlipuko wa homa kali ya mapafu; kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi; na ukwepaji kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, hususan kupitia biashara za magendo, kutokutoa na kudai stakabadhi za kielektroniki wakati mauzo yanapofanyika na kasi ndogo ya ukusanyaji wa kodi ya majengo.

31.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Juni 2021, Serikali itaendelea kuchukua hatua na kutekeleza mikakati mbalimbali kwa lengo la kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ili kufikia malengo kwa kipindi kilichobaki cha mwaka 2020/2021. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya majanga na kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko na kuimarisha ukaguzi wake.

32.    Mheshimiwa Spika, halikadhalika, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima; kuhakikisha nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa na hivyo, kuendana na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi; kuhakikisha miradi inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya miradi mipya; kudhibiti ulimbikizaji wa madai; na kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika miamala na shughuli za Serikali.

33.            Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Serikali itatekeleza mikakati mahususi ya kuongeza mapato kwa kufanya yafuatayo:-

Mosi:          Kuimarisha mifumo ya usimamizi kwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanatumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD);

Pili:             Kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka zinazokusanya mapato ya Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika kufanya doria maeneo ya mipaka ya nchi kavu, baharini na kwenye maziwa ili kudhibiti biashara za magendo;

Tatu:          Kukasimisha jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa Halmashauri na Serikali za Mitaa.

34.            Mheshimiwa Spika, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kuibua hoja ambazo zilifanya mjadala wetu humu Bungeni kuwa wa kina na wenye kutoa msisimko wa kiwango cha juu. Yote hayo, yalitokana na ukweli kwamba Waheshimiwa Wabunge, waliibua hoja na kuchangia kwa umakini mkubwa kwa lengo kujenga na kusaidia taifa letu.

35.            Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine kupitia hoja na michango yao, Waheshimiwa Wabunge wamegusia masuala muhimu ikiwemo elimu, kilimo, uwezeshaji, uwekezaji, viwanda na miundombinu ambayo yamekuwa kitovu cha mjadala na michango ya Waheshimiwa Wabunge. Kwa msingi huo, naomba nitumie fursa hii adhimu kutolea ufafanuzi baadhi ya masuala muhimu yaliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge.

ELIMU

Miundombinu ya Elimu

36.            Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu wa Pili wa Bunge lako tukufu, Waheshimiwa Wabunge wameibua hoja nyingi kuhusu changamoto ya miundombinu ya shule hususan sekondari, suala la ujuzi na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Nyingi ya changamoto hizi, zinatokana na utekelezaji mzuri wa sera ya Elimumsingi Bila Malipo sambamba na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule na vyuo ambao umechangia kuongezeka kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na hata darasa la kwanza kila mwaka.

37.            Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa samani na miundombinu, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ya muda mfupi na muda mrefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa Darasa la Saba wanajiunga na kidato cha kwanza bila kujali ni chaguo la kwanza au la pili na kuhakikisha miundombinu yote na samani zote kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi hawa inakamilika ifikapo tarehe 28 Februari, 2021.

38.            Mheshimiwa Spika, Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 1.2 kwa ajili ya mradi wa maboresho ya elimu ya sekondari yaani (Secondary Education Quality Improvement Programme - SEQUIP).  Mradi huo, uliidhinishwa mwaka jana licha ya kelele nyingi kutoka kwa watu wasiokuwa na uzalendo na nchi hii.

39.            Mheshimiwa Spika, mradi huo, utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitano (2020/2021 - 2025/2026) utakuwa ni mwarobaini kwa changamoto ya miundombinu ya shule za sekondari kwani shule mpya 1,026 zitajengwa kote nchini. Kati ya shule hizo, shule mpya 26 zitakuwa za Bweni zenye uwezo wa kupokea wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,500 kwa kila mkoa na zitajengwa kwa awamu tatu.

40.            Mheshimiwa Spika, kadhalika, Shule mpya 1,000 za kutwa zitajengwa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa kila shule. Shule hizo zitajengwa kwenye kata 718 zisizo na sekondari za kata na kwenye maeneo yaliyoelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi. Hivyo basi, nitumie nafasi hii kuwaelekeza viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa wasimamie kikamilifu utekelezaji wa mradi huu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mikopo ya Elimu ya Juu

41.            Mheshimiwa Spika, kuhusu mikopo ya elimu ya juu, kwa mwaka huu 2020/2021 Serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 55,287 ambapo wanafunzi 28,041 sawa na asilimia 5 wamehitimu elimu ya sekondari katika shule mbalimbali za binafsi. Serikali itaendelea kuzingatia kigezo pekee cha uhitaji wa mwombaji sambamba na kurahisisha matumizi ya mtandao katika uombaji na utoaji wa mikopo.

42.            Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ufanisi wa utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, Serikali imefanya maboresho ya kisheria, kimfumo na kiutendaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015/2016 – 2019/2020). Matunda ya maboresho hayo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo kutoka wastani wa shilingi 28.9 bilioni mwaka 2016/2017 hadi kufikia wastani wa shilingi 192 bilioni mwaka 2019/2020.

43.            Mheshimiwa Spika, Serikalini inafarijika na inapokea kwa mikono miwili michango yenye afya na tija kuhusu hatma ya mikopo inayotolewa na Serikali baada ya miaka 15 ya uwepo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

44.            Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba Serikali kwa upande wake, ipo tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kuhusu namna bora zaidi ya kuufanya mfuko huu uwe endelevu na wenye manufaa katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi, katika kuufanya mfuko huo uwe endelevu na himilivu; nitumie fursa hii kuelekeza mambo yafuatayo;

Kwanza:     Ninaitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ishirikiane na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuboresha huduma zake na kurahisisha urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika waliojiari katika sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa mnufaika na mwajiri.

Pili:             Ninawasihi wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu, ambao bado hawajajitokeza na kuanza kurejesha, wafanye hivyo mara moja;

Mwisho:     Ninawataka waajiri wote nchini katika sekta binafsi na sekta ya umma, watoe kipaumbele kwa makato ya mikopo ya elimu ya juu kama yalivyo makato mengine ya kisheria; na

Ukuzaji Ujuzi

45.            Mheshimiwa Spika, ukuzaji ujuzi ni miongoni mwa hoja iliyoungwa mkono na Wabunge wengi wakati wa kuchangia hoja mbalimbali hususan ya elimu wakati wa mkutano huu. Hivyo, nami nitumie nafasi hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Januari, 2021 vijana 10,178 wamepatiwa mafunzo na kutathminiwa ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa mafunzo nchi nzima ambapo vijana 9,736 wamefaulu na kupatiwa vyeti na Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA).

46.            Mheshimiwa Spika, vyeti hivyo vinawawezesha kutambulika, kujiendeleza kiujuzi, kujiajiri pamoja na kupata kazi katika taasisi na kampuni mbalimbali. Vijana hao ni wenye ujuzi katika fani za uashi, useremala, ushonaji, ufundi bomba, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi magari, ufundi umeme, ukarabati wa bodi za magari, upishi na uhudumu katika hoteli. Aidha, vijana 36 wamegharamiwa na Serikali kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa nchini Israel.

47.            Mheshimiwa Spika, katika nusu ya pili ya mwaka 2020/2021 vijana wapatao 4,616 watapatiwa mafunzo na kurasimishwa ujuzi walionao kupitia mfumo huu. Aidha, mwezi Januari 2021, vijana 1,203 wa vyuo vya elimu ya juu na kati wamehitimu mafunzo ya uzoefu wa kazi kupitia kampuni mbalimbali kulingana na fani walizosomea, na Wahitimu 2,037 wamewezeshwa na wanaendelea kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika taasisi binafsi na za umma ambayo yatachukua muda wa kipindi cha mwaka mmoja. Vilevile, Wahitimu 2,421 wanaandaliwa kwa ajili ya kuanza mafunzo mwezi Machi, 2021 katika fani za ushonaji nguo, useremala, uashi, uchorongaji vipuri, ufundi magari, umeme, bomba, terazo, upishi, na utoaji huduma za mahoteli, utengenezaji wa simu, majokofu, viyoyozi, upakaji rangi, uandishi wa alama, utengenezaji wa umeme wa magari, utengenezaji wa nywele na utanashati, uchoraji, n.k.

Barabara

48.            Mheshimiwa Spika, kumejitokeza mjadala unaohitaji uboreshaji miundombinu ya barabara za mijini na hasa za vijijini. Vyombo vyetu vya TANROADS na TARURA vinafanyia kazi na sasa tunakusudia kuongeza uwezo wa vyombo hivyo. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tumepokea ushauri wenu na tutaufanyia kazi ili tuweze kufanya maboresho.

KILIMO

Hali ya Kilimo katika Msimu huu wa kilimo

49.            Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mvua wa mwaka 2020/2021, mvua za vuli zilizoanza mapema mwezi Septemba zimeendelea kunyesha kwa kiwango cha juu ya wastani katika maeneo mengi hasa ya Kanda ya Ziwa Victoria. Katika maeneo mengine ya Pwani ya Kaskazini na Kanda ya Kaskazini Mashariki, mvua zilichelewa kuanza (Novemba) na zimeendelea kunyesha hadi katika mwezi Januari, 2021.

50.            Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Januari, mwenendo wa unyeshaji wa mvua hizo umeendelea kwa kiwango cha juu ya wastani katika maeneo mengi. Mwelekeo unaonesha kuwa mvua hizi zitachangia upatikanaji wa chakula katika kipindi cha mwezi Februari na kuendelea kabla ya mavuno mengine kuanzia mwezi Mei, 2021. Vilevile, hali ya malisho ya mifugo na upatikanaji wa maji umeendelea kuwa mzuri katika maeneo yote nchini.

Kuimarisha Kilimo cha Umwagiliaji

51.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, Serikali imefanikiwa kujenga na kukarabati skimu za umwagiliaji 179 ambazo zimeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 50.7. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 (yaani Revised National Irrigation Master Plan - RNIMP 2018) ambao umeainisha hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha Umwagiliaji.

52.            Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi wa maghala 14 ya kuhifadhia mavuno katika skimu za umwagiliaji za Ngana na Makwale (Kyela), Magozi na Tungamalenga (Iringa), Mbuyuni-Kimani, Ipatagwa, Kongolo-Mswiswi na Motombaya (Mbarali), Lekitatu (Arusha), Mombo (Tanga), Uturo (Mbeya), Bagamoyo (Pwani), Mkindo na Mkula (Morogoro).

53.            Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo, kati ya maghala hayo, maghala 6 yamewekewa na vinu vya kukobolea mpunga.

54.            Mheshimiwa Spika, nimeamua kusema haya ili Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujuma wafahamu kwamba tunatambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji na tunachukua hatua.

Upatikanaji wa pembejeo za kilimo na uzalishaji wa mbegu

55.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati ambayo ni pamoja na kupata mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kutoka kila mkoa kabla ya msimu wa kilimo kuanza na kuwasiliana na Makampuni ya pembejeo na kuyahimiza kusambaza pembejeo hizo mapema kulingana na mahitaji ya kila mkoa.

56.            Mheshimiwa Spika, pia, Serikali inaboresha mifumo ya uzalishaji, uagizaji na uthibiti wa mbegu bora na viuatilifu hapa nchini ikiwemo kuimarisha uzalishaji wa pembejeo hizo ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji na upatikanaji wake kwa wakati.

 

57.            Mheshimiwa Spika, katika kufikia malengo, Serikali itaongeza eneo la ASA la uzalishaji wa mbegu kutoka hekta 4,925 (2019/2020) hadi hekta 6,923 ifikapo 2025 na eneo la TARI kutoka hekta 1,033.2 hadi hekta 3,663.24 ifikapo 2025.

Huduma za Ugani

58.            Mheshimiwa Spika, uzalishaji na tija katika kilimo, pamoja na mambo mengine huchangiwa na maarifa na ujuzi unaotolewa na Maafisa Ugani kwa wakulima. Kwa mantiki hiyo, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa kila kijiji, mtaa na kata vinakuwa na Afisa Ugani angalau mmoja ili kuwawezesha wakulima kupata maarifa na ujuzi wa kuzalisha mazao kwa ufanisi na tija.

59.            Mheshimiwa Spika, idadi ya Maafisa Ugani waliopo nchini ni 6,704 ikilinganishwa na mahitaji 20,538. Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa Maafisa Ugani, Wizara inaendelea kusomesha Maafisa Ugani tarajali katika ngazi ya Cheti na Diploma ambapo kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 jumla ya wataalamu wa kilimo 8,657 walihitimu katika vyuo vya mafunzo ya kilimo ngazi ya Cheti na Diploma.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

60.            Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, suala la uwezeshaji Wananchi iwe kwenye sekta ya kilimo au ujasiriamali na biashara ndogo na za kati ni miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Suala hilo, pia limejitokeza wazi wazi kwenye hotuba ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati akifungua Bunge la 12.

61.            Mheshimiwa Spika, katika hotuba hiyo, Mheshimiwa Rais aliielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa inaimarisha uratibu na usimamizi wa Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili Watanzania waifahamu ilipo, vigezo vya kutolea mikopo na aina ya mikopo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na mikopo hiyo ili kuinua vipato vyao, kupunguza umaskini na tatizo la ajira.

62.            Mheshimiwa Spika, licha ya changamoto zinazokabili mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020, mifuko na programu za uwezeshaji za serikali zimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani zaidi ya shilingi trilioni 2.22, kunufaisha zaidi ya watu milioni 4.9 na taasisi 5,499.

63.            Mheshimiwa Spika, vilevile, kupitia mifuko ya uwezeshaji wa makundi maalumu ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu Halmashauri 185 zimefanikiwa kutoa shillingi bilioni 93.3. Fedha hizo, zimewezesha upatikanji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi 32,553 kote nchini. 

64.            Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tumeanza kuchukua hatua zenye kulenga kuboresha huduma za mifuko na programu za uwezeshaji. Tarehe 17 Novemba, 2020 tulianza zoezi la tathmini ya utendaji wa programu na mifuko takriban 20. Aidha, tayari taarifa ya awali kutoka ngazi ya Wataalamu imekamilika na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika.

65.            Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Februari 2021 nilifungua wiki ya maonesho ya nne ya mifuko na programu za uwezeshaji kwa kanda ya Kaskazini yanayofanyika kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Arusha. Ni Matumaini yangu kwamba kupitia maonesho hayo wananchi wa mkoa wa Arusha, mikoa ya kanda ya Kaskazini pamoja na wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini watapata uelewa mpana kuhusu shughuli za mifuko na programu za uwezeshaji.

Mabenki na Mifuko ya Fedha Kuchangia Kilimo

66.            Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walieleza kwa kina kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima na wafanyabiashara wetu hususan wadogo katika shughuli zao za kiuchumi na kujiongezea kipato hususan masuala ya uzalishaji, masoko, ufungashaji bora wa bidhaa, huduma za fedha, elimu ya ujasiriamali, teknolojia n.k.

67.            Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba mchango wa sekta ya fedha hususan mabenki na mifuko ya hifadhi za jamii kwenye kilimo bado ni mdogo kwani hadi sasa upo kwenye asilimia 8.5 sawa na shilingi trilioni 1.65. Kwa msingi huo, Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na Benki na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuona namna ambavyo watachangia katika shughuli za kilimo na mnyororo mzima wa thamani.

Uwezeshaji wa Wajasiriamali Wadogo (Machinga)

68.            Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini sana mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) katika kukuza uchumi, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, kuondoa umaskini na kuleta maendeleo endelevu nchini. Sekta hii ya wafanyabiashara wadogo nchini inakadiriwa kuwa na wajasiriamali milioni 3.1 ambao wameajiriwa sawa na takriban asilimia 23.4 ya nguvu kazi ya Taifa.

69.            Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wadau wa sekta hii wanaendesha shughuli zao bila kubughudhiwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kugawa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo. Hata hivyo, licha ya mafanikio makubwa ya vitambulisho hivyo, vimeonesha kuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji maboresho hususan katika kuwasaidia kupata mikopo na mitaji kutoka kwenye taasisi za fedha ili waweze kuendesha shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

70.            Mheshimiwa Spika, katika kuwasadia wajasiriamali wadogo kupata mitaji kwa urahisi kupitia taasisi za fedha, Serikali imeanza taratibu za kuboresha Vitambulisho vya Wafanyabiashara Wadogo kwa mwaka 2021. Vitambulisho hivyo vitakuwa vya kielektroniki na  vitaboreshwa zaidi hatua kwa hatua ili viwawezesha wafanyabiashara wadogo kukopa kutoka taasisi za fedha ikiwemo programu na mifuko ya uwezeshaji.

71.            Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Januari, 2021 nilipata fursa ya kufungua Kongamano la Wafanyabiashara Wadogo (maarufu Wamachinga) lililofanyika Jijini Dar es Salaam. Lengo la Kongamano hilo, pamoja na mambo mengine lilikuwa ni kuwashirikisha wadau hao kuhusu namna nzuri zaidi ya kuboresha vitambulisho vya wafanyabiahara wadogo (Wamachinga) ili waweze kuvitumia kupata mitaji au mikopo kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha.

72.            Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) kwa kutekeleza vyema jukumu la usambazaji wa bidhaa nchini kwa bei nzuri wanazozimudu wananchi hasa wale wa kipato cha chini. Aidha, nitoe rai kwa Machinga wote kuepuka kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa wanaowatumia kukwepa kodi; kwa kuwapa bidhaa nyingi bila kutoa risiti za kielektroniki zenye kiwango halisi cha bei ya kununulia bidhaa husika.

73.            Mheshimiwa Spika, wakati tunaendelea na zoezi la kuboresha vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, naagiza viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa washirikiane na viongozi wa wafanyabiashara wadogo kwenye maeneo yao ili kupata orodha yao na kuwaandalia maeneo ya kufanyia biashara zao.

MICHEZO

74.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha hivi karibuni nchi yetu imepata mafanikio mbalimbali hususan katika mpira wa miguu. Nitumie nafasi hii kutoa pongezi zangu kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa mafanikio makubwa yanayojitokeza kwa upande wa soka na michezo mingine kama ngumi hapa nchini. Mathalan, katika kipindi hiki tumeshuhudia Tanzania ikishiriki fainali za mashindano ya Afrika ya Mpira wa Miguu kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani (CHAN) ambayo yamekamilika hivi karibuni huko Cameroon.

 

75.            Mheshimiwa Spika, nizipongeze pia timu za Taifa za umri wa chini ya miaka 20 na 17 ambazo zimefuzu kushiriki katika mashindano ya Fainali za Bara la Afrika kwa mwaka 2021. Timu hizi zitakwenda kushiriki katika fainali za michuano hiyo katika nchi za Morocco kwa U-17 na Mauritania kwa timu ya U-20. Vilevile, naipongeza timu ya Wanawake U-17 kushinda kombe la COSAFA kwa mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini, Novemba 2020.

76.            Mheshimiwa Spika, kwa upande wa soka la vilabu, naipongeza Namungo FC kwa kufanikiwa kuvuka hatua mbili za awali kuelekea kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na pia niwatakie kila la heri kwenye mchezo wao utakaochezwa kesho Jumapili huko nchini Angola.

77.            Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia mabingwa wa Soka Tanzania, timu ya Simba Sports Club kwa kufanikiwa kufuzu kuingia hatua ya makundi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, na jana kushinda mchezo wake wa kwanza katika hatua ya makundi wakiwa ugenini dhidi ya Klabu ya AS Vita huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nitumie nafashi hii kumpongeza Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, mwanadada Barbra Gonzalez kwa ubunifu na kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii na hivyo kulipa heshima Taifa letu kwa kulitangaza kupitia jezi yao kwa maneno VISIT TANZANIA huu ni uzalendo wa hali ya juu ambo unapaswa kupongezwa na kuigwa.

78.            Mheshimiwa Spika, mchambuzi maarufu wa michezo nchini Bw. Ali Kamwe, kupitia ukurasa wake wa instagram, ameeleza vizuri maana ya matumizi ya neno VISIT TANZANIA na namna nchi yetu itakavyonufaika na ubunifu huo. Kwa mujibu wa maelezo yake, neno VISIT TANZANIA linakadiriwa kutazamwa na wapenzi wa soka takriban milioni 500 kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wapenzi hao wa mpira kupitia vituo vya Televisheni vya Canal Algérie, BeIN Sports, Eurosport, ESPN, Arryadia, GTV ya Ghana, MENA beIN Sports na West Africa Canal+ wameshuhudia mchezo wa jana. Kwa lugha nyingine ni kwamba neno 'VISIT TANZANIA' lililopo sehemu ya kifuani mwa jezi ya Klabu ya Simba litaonekana kupitia chaneli hizo kwa kila dakika 90 ambazo Simba itashuka dimbani iwe dhidi ya Al-Ahly (Misri), El-Mereikh (Sudan) au dimba la nyumbani kwa Mkapa (Tanzania). Tutavuta watalii wengi kuifuatilia Nchi yetu.

79.            Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kung’ara pia kwenye medani ya masumbwi. Kwa upande huo wa masumbwi, nawapongeza mabondia Mfaume Mfaume kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa East and Central Africa mwezi Decemba 2020; Bondia Ibrahimu Class Mgendera kwa kushinda Ubingwa wa World Boxing Federation Intercontinental lightweight (WBF). Vilevile, nawapongeza Bondia Tonny Rashidi aliyefanikiwa kutetea mkanda wake wa African Boxing Union (ABU) na Bondia Shabani Hamadi JONGO aliyeshinda ubingwa wa WBF International Cruiserweight mwishoni mwa Januari 2021. Bila kuwasahau Mabondia walioonesha uwezo mkubwa wa kina Hassan Mwakinyo, Twaha Kiduku na Dulla Mbabe ambaye atapanda ulingoni tarehe 26 Februari, 2021.

HITIMISHO

80.            Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu muhimu mliyoitoa kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wetu. Nimshukuru Katibu wa Bunge, wasaidizi wake na watumishi wote wa Bunge kwa huduma nzuri na msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia kwa kipindi chote tulichokuwa tukitekeleza majukumu yetu ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 12.

81.            Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia viongozi na watendaji wa Serikali na taasisi zake ambao wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, umahiri na ufanisi mkubwa. Hongereni sana kwani juhudi zenu zimekuwa chachu ya kufanikisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Pili wa Bunge la 12. Vilevile, nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitowashukuru wanahabari kwa uchambuzi mzuri wa hoja na mwenendo mzima wa Bunge na kuwahabarisha wananchi.

82.            Mheshimiwa Spika, vilevile, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma ambazo wamekuwa wakizitoa kwa washiriki wa Bunge hili. Pia, niwashukuru madereva wote waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa Bungeni na ninawatakia heri katika safari ya kurejea nyumbani.

83.            Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 30 Machi 2021 siku ya Jumanne saa tatu kamili asubuhi katika ukumbi huu hapa Jijini Dodoma.

84.            Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa hoja.

 

13 February 2021, 12:59