Mashambulizi dhidi ya vijiji na makundi ya kujihami huko Niger. Mashambulizi dhidi ya vijiji na makundi ya kujihami huko Niger. 

UNICEF yalaani mashambulizi dhidi ya raia ikiwemo watoto huko Niger

Tarehe 2 Januari 2021 mashambulizi dhidi ya raia yalitekelezwa na makundi yaliyojihami kwenye vijiji vya vitatu huko Niger mpakani na Mali.Miongoni mwa walipoteza maisha hata watotowa kike 10 na wasichana 7 chini ya umri wa 16.Inadaiwa wengine waliteketezwa moto.Mkuregenzi wa UNICEF amesema,ukatili ambao unapuuza maisha ya watoto na familia unapaswa kulaaniwa vikali.Ni ukiukaji wa haki za watoto,kimataifa na binadamu.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeelezea kusikitishwa na mashambulizi ya Jumamosi tarehe 2 Januari 2021 yaliyotekelezwa na makundi yaliyojihami dhidi ya raia kwenye vijiji vya Tchoma Bangou na Zaroumadareye, nchini Niger karibu na mpaka na Mali. Duru zinasema kwamba takriban watu mia moja wameuwawa ikiwemo watoto 17. Taarifa ya UNICEF kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dakar, Senegal na New York, Marekani inasema kwamba taarifa zisizothibitishwa zinaonesha kwamba watoto wote waliopoteza maisha, wavulana kumi na wasichana saba walikuwa chini ya umri wa miaka 16, na inadaiwa kwamba wengine waliteketezwa moto.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, Bi. Henrietta Fore amesema, “idadi isiyojulikana ya watoto manusura wa shambulio walipata majeraha makubwa, huku wengine wengi wamelazimika kuhama makwao. Karibu watoto 11 wametenganishwa na familia zao.” Aidha Bi. Fore amesema,“ukatili ambao unapuuza maisha ya watoto na familia unapaswa kulaaniwa vikali. Vitendo hivyo vya kikatili ni ukiukwaji wa haki za watoto, haki za kimataifa na haki za binadamu. UNICEF inatoa wito kwa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya watoto, familia zao na jamii.”  

Shambulio hili linafuatia lingine lililofanyika mnamo Desemba huko Toumour nchini Niger kwenye eneo la Diffa ambapo watu 45 ikiwemo watoto 10 waliuwawa. Shambulio hilo liliharibu hifadhi ya chakula, miundombinu ya maji na madarasa mawili na kuathiri watu takriban 21,000. Aidha UNICEF imetoa  rambi rambi za dhati kwa familia za wahanga na kuelezea mshikamano wa UNICEF kwa ajili ya watoto na familia nchini Niger.  UNICEF aidha iko tayari kusaidia serikali ya Niger katika kusaidia manusura na familia zilizoathirika na kulinda haki za watoto  wote. 

05 January 2021, 12:17