Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania katika kipindi cha uongozi wake tangu mwaka 2015 hadi mwaka 2020 ametoa mwelekeo mpya wa kiuchumi na kiutawala asema Waziri mkuu Kassim Majaliwa. Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania katika kipindi cha uongozi wake tangu mwaka 2015 hadi mwaka 2020 ametoa mwelekeo mpya wa kiuchumi na kiutawala asema Waziri mkuu Kassim Majaliwa. 

Rais Magufuli Ametoa Mwelekeo Mpya: Kiuchumi na Kiutawala!

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa mwelekeo mpya wa kiuchumi na kiutawala nchini ambao umesababisha Tanzania iingie kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda uliopangwa wa 2025. Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ziendelee kutoa elimu ya uchumi wa viwanda kwa wananchi ili waweze kushiriki kujenga na kukuza uchumi wa viwanda.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dodoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa mwelekeo mpya wa kiuchumi na kiutawala nchini ambao umesababisha Tanzania iingie kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda uliopangwa wa 2025. Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ziendelee kutoa elimu ya uchumi wa viwanda kwa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu kujenga na kukuza uchumi wa viwanda. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Alhamisi, Januari 14, 2021 katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma alipozindua kitabu cha “The Game Changer: President Magufuli’s First Term in Office”. Kitabu hicho kimehaririwa na Profesa Ted Maliyamkono na Dkt. Hugh Mason. Amesema mpangilio na muktadha mzima wa kitabu hicho unabeba dhamira ya kukifanya kuwa kimbilio la rejea kwa watunga sera, wafanya maamuzi, wanataaluma na hata wananchi wa kawaida katika masuala mazima ya maendeleo ya nchi yetu.

“Kitabu hiki tunachokizindua leo, The Game Changer, kimeonesha namna sera na mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano ilivyobadili mwelekeo wa Taifa letu kimaendeleo. Nitoe rai kwa waandishi wa kitabu hiki, waangalie uwezekano wa kutoa chapisho kwa Kiswahili ili Watanzania wengi waweze kukisoma na kunufaika na maudhui yake.” Waziri Mkuu amesema kitabu kimefafanua kuwa Tanzania ni nchi yenye kuendeshwa kidemokrasia na kimeondoa shaka waliyonayo wadau wa maendeleo na wawekezaji kwa lengo la kuwawezesha kuongeza uwekezaji wao hapa nchini. Naye, Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Balozi Mhandisi Dkt. John Kijazi amesema: “Kitabu hicho kiwe chachu kwa Maprofesa wa vyuo vingine, wakae chini wafanye tafiti na kuandika vitabu vya aina hiyo ili kusaidia kuhifadhi historia ya nchi.” Amesema vitabu vya aina hiyo vitasaidia vijana kutambua kazi zilizofanywa na viongozi mbalimbai nchini Tanzania pamoja na kuenzi historia ya nchi yao!

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema kazi ya fasihi andishi ni kutunza kumbukumbu na kitabu hicho kitasaidia kuhakikisha mambo mazuri yaliyofanywa na Rais Dkt. Magufuli yanadumu kwa vizazi vijavyo. “Hakika kazi yake imetukuka.”  Naye, Mhariri Mkuu wa kitabu hicho, Profesa Maliyamkono akisoma muhtasari wa kitabu hicho, amesema kimeelezea namna Rais Dkt. Magufuli alivyoingia madarakani, hali aliyoikuta na hatua alizochukua pamoja na mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano! “Rais Dkt. Magufuli wakati anaingia madarakani aliikuta nchi ikiwa katika wakati mgumu kiuchumi, amefanya kazi kubwa ya kurekebisha mikataba mibovu ya madini, amedhibiti rushwa na kwa sasa nchi inafaidika na rasilimali zake. Hakuna kiongozi wa Afrika ambaye aliweza kuziwajibisha kampuni kubwa za madini lakini Rais Dkt. Magufuli ameweza.”

Awali, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akitoa maoni kuhusu utendaji kazi wa Rais Dkt. Magufuli alisema amefanya mambo mengi katika miaka 20 ya utumishi wake Serikalini na miaka mitano ya urais. “Rais Dkt. Magufuli ni muasisi wa wazo la ujenzi wa barabara kwa kutumia fedha za ndani.” Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema Rais Dkt. Magufuli ni mwanamageuzi wa kweli na ameipambanua nchi katika miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli ya kisasa inayowawezesha Watanzania kushindana katika uchumi. Alishauri kuwe na maandiko mengi yahusuyo viongozi. Kitabu kimetayarishwa kwa lengo la kuweka kumbukumbu ya kazi zilizofanyika na zile zilizotegemewa kufanyika katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano (2015 - 2020) chini ya Rais Dkt. Magufuli.

15 January 2021, 14:53