Tafuta

Watanzania waonesha mshikamano wa huruma, udugu na upendo kwa kuchangia maboresho ya maisha ya Miriam Msagari binti mwenye ulemavu wa mwili kwa sasa na kwa siku za usoni! Watanzania waonesha mshikamano wa huruma, udugu na upendo kwa kuchangia maboresho ya maisha ya Miriam Msagari binti mwenye ulemavu wa mwili kwa sasa na kwa siku za usoni! 

Mshikamano wa Huruma, Udugu na Upendo kwa Miriam Msagati

Miriam Msagari baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo amewashukuru viongozi wa Tanzania kwa kuwajali wanyonge. Alisema Tanzania imepata kiongozi mzuri anayewajali wanyonge, hivyo ameahidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awazidishie baraka. “Siwezi kusahau kitu kama hiki, Mwenyezi Mungu ameniona na awabariki wote kwani mmeweka hazina yenu kwa Mungu.”

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Tanga, Tanzania

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha changamoto zote zilizokuwa zinawakabili wakulima wa zao la mkonge nchini ikiwemo ya kuibiwa mapato hazijirudii. “Awali wakulima walikuwa wanaibiwa sana jambo ambalo kwa sasa halitojirudia tena kwani Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha mkulima ananufaika, hivyo tulime mkonge unalipa.” Aliyasema hayo hivi karibuni, alipozungumza na wananchi baada ya kukagua shamba la mkulima mdogo wa mkonge lililoko Magunga Estate wilayani Korogwe. Waziri Mkuu alisema miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya pili duniani katika kilimo cha mkonge ambapo ilikuwa ikizalisha tani 200,000 kwa mwaka ikitanguliwa na Brazil. Alisema uzalishaji wa zao la mkonge nchini ulishuka kutoka tani 200,000 kwa mwaka na hadi tani 39,000, Serikali imedhamiria kuongeza uzalishaji na kufikia tani 150,000 ifikapo 2025. Naye, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisema awali wakulima wa mkonge walikuwa wakilipwa sh. 50,000 kwa tani kutokana na kuibiwa na watu wasio waaminifu ila baada ya Serikali kati bei imeongezeka hadi kufikia milioni nne.

Mkuu wa mkoa wa Tanga alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kuamua kusimamia mwenendo wa biashara ya kilimo cha mkonge na tayari wakulima wameanza kupata tija. Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saady Kambona alisema wamepokea maombi zaidi ya 2,000 ya wananchi wanaohitaji mashamba kulima mkonge. Alisema Bodi imepeleka maombi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kurudishiwa mashamba ambayo yametekelezwa ili wayagawe kwa wananchi. Alisema kwa sasa hamasa ya kilimo cha mkonge ni kubwa baada ya Serikali kuonesha dhamira ya kulifufua zao hilo na wananchi wengi wamejitokeza na wameomba mashamba. Awali, Mwenyekiti wa Magunga Amcos, Shedrack Lugendo alisema uzalishaji wa mkonge umekuwa mzuri baada ya chama chao kusimamia uzalishaji na Desemba mwaka jana walipata daraja la juu ambalo ni 3L kiasi cha tani mbili baada ya kupita miaka 10. Akizungumzia kuhusu shamba la mkulima mdogo Estohim Urio ambalo Waziri Mkuu alilitembelea alisema mkulima huyo anamiliki hekta 200 alizopewa na Bodi ya Mkonge. Mwenyekiti huyo alisema mkulima huyo amefanikiwa kupanda hekta 182 ambazo mkonge mkubwa unaovunwa ni hekta 113 na eneo lenye mkonge mdogo ni hekta 69.

Na habari zaidi zinabainisha kwamba, Kassim Majaliwa ameendesha harambee ya papo kwa papo na kuchangisha sh. milioni 18.9 ambapo kati ya hizo, sh. milioni 10 zimetolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anafuatilia tukio hili na amesema anamchangia Miriam shilingi milioni 10 ili ziweze kumsaidia katika mtaji wa biashara na umaliziaji wa ujenzi wa vyumba vya kupangisha” Fedha hiyo ilichangishwa kwa ajili ya Miriam Msagati, binti mwenye ulemavu wa mwili ili ziweze kumsaidia kama mtaji wa biashara na uendelezaji wa ujenzi wa vyumba vya kupangisha katika nyumba ambayo amekabidhiwa Ijumaa, Januari 22, 2021) na Waziri Mkuu. Gharama ya ujenzi wa nyumba na samani zilizomo ndani ni sh. milioni 47.32. Waziri Mkuu ameendesha harambee hiyo kwenye kitongoji cha Fune, kata ya Mombo wilayani Korogwe baada ya kumkabidhi binti huyo nyumba aliyojengewa na wadau mbalimbali kutokana na mchango ulioasisiwa na Waziri Mkuu Machi 5, 2020 alipomtembelea Miriam na kumpatia mchango wa sh. milioni 5 za kuanza ujenzi wa nyumba hiyo.

Waziri Mkuu alimsaidia Miriam baada ya kumsikia binti akimuomba amsaide kupata makazi yeye na bibi yake kupitia kipindi cha Wape Nafasi kinachoongozwa na Tuma Dandi, mtangazaji wa Shirika la Utangazi Tanzania (TBC1). Baada ya Waziri Mkuu kukabidhi nyumba hiyo, aliwaomba wadau wamchangie Miriam fedha ili apate mtaji pamoja na umaliziaji wa vyumba vya kupangisha ili aweze kujitegemea. Akiwa bado anaendesha harambee hiyo, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alizungumza na wananchi hao kupitia simu aliyompigia Waziri Mkuu, ambapo alimpongeza kwa kuhakikisha Miriam anapata makazi bora. “Nimeona kazi kubwa iliyofanyika hapo, hongereni sana Waziri Mkuu pamoja na uongozi wa mkoa wa Tanga nami namuongezea shilingi milioni tano afanye mtaji.”

Kwa upande wake, Miriam baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo alimshukuru Rais Dkt. Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia, Waziri Mkuu kwa uongozi wao wenye kujali wanyonge. Alisema Tanzania imepata kiongozi mzuri anayewajali wanyonge, hivyo ameahidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awazidishie baraka ili wapate mafanikio mazuri zaidi. “Siwezi kusahau kitu kama hiki, Mwenyezi Mungu ameniona, Mwenyezi Mungu awabariki watu wote walioshiki katika kufanikisha jambo hili kwani mmeweka hazina yenu kwa Mungu.” Kwa upande wake, Mwandaaji wa Kipindi Cha Wape Nafasi, Tuma Dandi alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyoshughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalumu. “Nimeishiwa maneno, leo ni siku nyingine ambayo itaingia katika historia ya maisha yangu. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu na Serikali kwa kufanikisha jambo hili kwani watu wenye ulemavu ni sehemu ya Watanzania ambao wanapaswa kuishi kama wengine.”

25 January 2021, 15:13