Tafuta

Vatican News
2020.06.20 Maneno ya Mchungaji Martin Luther King,mtetezi wa haki za binadamu alisema "Giza haliwezi kufukuza giza,ni nuru pekee inayoweza kufanya hivyo". 2020.06.20 Maneno ya Mchungaji Martin Luther King,mtetezi wa haki za binadamu alisema "Giza haliwezi kufukuza giza,ni nuru pekee inayoweza kufanya hivyo". 

Umoja wa Mataifa utaendeleza matakwa na kazi za Martin Luther King Jr!

Naibu Katibu Mkuu wa UN amesema Dk.King aliishi kwa kukumbatia maadili ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani,haki ya kijamii na haki za binadamu.Kupitia maadhimisho ya siku yake ni kusisitizia ahadi ya kazi aliyoifanya.Kwa maana hiyo nguvu ipatikane kutoka maneno yake:“Giza haliwezi kufukuza giza,bali mwanga.Chuki haiwezi kufukuza chuki ni upendo pekee.Amesema hayo katika kilele cha Siku ya King,tarehe 18 Januari.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Jumatatu tarehe 18  Januari 2021 ilikuwa ni fursa  ya kuadhimishwa siku ya kuzaliwa kwa kiongozi maarufu  Martin Luther King Jr aliyekuwa mwanaharakati mkubwa wa kupigania haki za binadamu duniani na ambaye ataendelea kukumbukwa na kuenziwa daima hasa katika zama hizi ambazo dunia imegawanyika vipande katika ukiukwaji wa haki za binadamu,chuki na ubaguzi kuendelea kusimika mizizi. Kupitia ujumbe maalum wa njia ya video kwenye kituo cha King, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amekumbusha kwamba mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka wa masumbuko kwa sababu maisha ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote  yamepotea, shughuli zimesimama kutokana na janga la corona au COVID-19 na athari za janga hilo hazisemeki.  Na hii yote ni kwamba maisha ya watu yamesambaratika, huku maadili ya pamoja yakiwekwa kwenye mtihani mkubwa na janga hilo kudhihirisha mizizi ya pengo la usawa katika jamii zetu.

Watu kutoka jamii za wachache ndiyo walioathirika zaidi kama ilivyo kwa wengine walio wachache katika jamii zetu. Lakini pia kusambaa kwa virusi hivyo vya corona kumetoa fursa mpya katika mitandao ya kijamii kusambaza chuki na taarifa za uongo, hata kabla ya janga hilo dunia ilikuwa inakabiliwa na wimbi la kauli za chuki, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, unazi wa kisasa, fikra za kuwa wazungu ni bora kuliko wengine na mifumo mingine ya ubaguzi.  Bi. Amina amesisitiza kuwa sasa ni wakati wa umoja, mshikamano na utu na maadili ya Umoja wa Mataifa ndiyo yatakayoongoza njia. Kama Dk. King alivyoukumbusha ulimwengu katika hotuba yake ya kihistoria mbele ya Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1967 kwamba “Hakuwezi kuwa na haki bila amani na hakuwezi kuwa na amani bila haki. Na ukweli huo bado una mashiko makubwa hadi leo hii .”

Kwa mantiki hiyo Bi. Amina amesisitiza kwamba wakati dunia ikihangaika  kujikwamua na kujijenga upya kutoka kwenye janga la COVID-19 na kujenga dunia bora zaidi kunahitajia kuwa na utofauti mpya ambao ni jumuishi na endelevu. Hii inamaanisha kwamba kuwekeza katika mahusiano ya kijamii na kuendeleza mbele ufikiaji wa usawa na fursa kwa wote.. Akifafanua aidha amewatazama wanaharakati wengine na kusema kwamba urithi wa mtazamo wa Dk. Martin Luther King na viongozi wengine Wamarekani weusi ambao ni wa kutetea haki za binadamu kama vile mbunge wa congress John Lewis kutoka Atlanda ambaye alijitolea kupigania usawa wa rangi au Ralph Bunche ambaye alipokea tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1950 ,kutokana na kazi yake kama mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Palestina  na mchango wake utaendelea kuhahamasisha katika safari hiyo .

Naibu Katibu Mkuu amesema Dk. King aliishi kwa kukumbatia maadili ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani, haki ya kijamii na haki za binadamu. Hivyo ameitaka dunia ikitumia maadhimisho haya ya siku ya King kusisitiza ahadi ya kazi aliyokuwa akiifanya  na kusema kwamba basi ipatikane nguvu kutoka kwa maneno ya Dk. King aliyosema kuwa  “Giza haliwezi kufukuza giza, ni mwangaza pekee ndio unaoweza kufanya hivyo. Chuki haiwezi kufukuza chuki ni upendo pekee ndio unaoweza kufanya hivyo.” Kwa kuhitimisha ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa mdau mkubwa wa kuendeleza matakwa na kazi ya Dkt. Martin Luther King Jr.

19 January 2021, 12:51