Kampeni za kuzuia malaria Afrika zinaendelea Kampeni za kuzuia malaria Afrika zinaendelea 

WHO:Malaria inazidi kupunga hata katika bara la Afrika

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya malaria ulimwenguni iliyotolewa tarehe 30 Novemba 2020 na shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO, maendeleo dhidi ya malaria yanaendelea kupungua, hasa katika nchi zenye mzigo mkubwa barani Afrika. Mapengo katika upatikanaji wa zana za kuokoa maisha yanadhoofisha juhudi za ulimwengu za kukabiliana na ugonjwa huo, na janga la COVID-19 linatarajiwa kurudisha nyuma zaidi mapambano.

Kwa msingi huo, WHO imetoa wito kwa nchi na wadau wa afya ulimwenguni kuongeza mapambano dhidi ya malaria, ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika ambao unaendelea kuchukua maelfu ya watu kila mwaka. Malengo bora ya uchukuaji hatua, zana mpya na kuongezeka kwa ufadhili vinahitajika ili kubadilisha mwelekeo wa ugonjwa huo na kufikia malengo yaliyokubaliwa kimataifa.  Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema, "ni wakati wa viongozi kote Afrika na ulimwengu  kuinuka tena kukabiliana na changamoto ya malaria, kama vile walivyofanya wakati walipoweka msingi wa maendeleo yaliyopatikana tangu mwanzoni mwa karne hii, kupitia hatua ya pamoja, na kujitolea kutomuacha mtu yeyote nyuma, tunaweza kufikia maono yetu ya pamoja ya ulimwengu usio na malaria."

Taarifa ya WHO kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa mnamo mwaka 2000, viongozi wa Kiafrika walitia saini azimio la kihistoria la Abuja wakiahidi kupunguza vifo vya malaria barani Afrika kwa asilimia 50 katika kipindi cha miaka 10. Kujitolea kwa nguvu kisiasa, pamoja na ubunifu katika zana mpya na kuongezeka kwa kasi kwa ufadhili, kulichochea kipindi cha mafanikio katika kudhibiti malaria ulimwenguni. Kwa mujibu wa ripoti ya sasa, maambuki ya malaria bilioni 1.5 na vifo milioni 7.6 vimeepukwa tangu 2000.  Mnamo mwaka wa 2019, jumla ya maambukizi ya malaria yalikuwa milioni 229, ambayo ni makadirio ya kila mwaka ambayo hayabadiliki katika miaka 4 iliyopita. Ugonjwa huo uliua watu 409, 000 katika mwaka 2019 ikilinganishwa na  watu 411,000 katika mwaka 2018.Ripoti ya WHO imeendelea kueleza kuwa kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, kanda ya Afrika imebeba zaidi ya asilimia 90 ya mzigo wa jumla wa magonjwa. Tangu 2000, ukanda huo umepunguza idadi ya vifo vya malaria kwa asilimia 44 kutoka wastani wa watu 680,000 hadi 384 000 kila mwaka. Hata hivyo, maendeleo yamepungua katika miaka ya hivi karibuni, hasa katika nchi zilizo na mzigo mkubwa wa ugonjwa. Upungufu wa fedha katika viwango vya kimataifa na vya ndani unaleta tishio kubwa kwa faida ya baadaye. Katika mwaka 2019, jumla ya ufadhili ilifikia dola bilioni 3 za kimarekani dhidi ya lengo la ulimwengu la dola za kimarekani bilioni 5.6. Uhaba wa fedha umesababisha mapungufu makubwa katika upatikanaji wa zana zilizothibitika za kuweza kuidhibiti malaria.  

COVID-19  katika mwaka huu wa 2020 imeibuka kama changamoto ya ziada kwa utoaji wa huduma muhimu za afya ulimwenguni. Kwa mujibu wa ripoti hii mpya ya WHO kampeni nyingi za kuzuia malaria ziliweza kusonga mbele mwaka huu bila ucheleweshaji mkubwa lakini shirika hilo lina wasiwasi kuwa hata uvurugwaji mdogo katika kupata matibabu, unaweza kusababisha upotezaji mkubwa wa maisha ya watu. Mathalani ripoti inatoa mfano kuwa mathalani asilimia 10 tu uvurugikaji wa upatikanaji wa dawa dhidi ya malaria katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara, kunaweza kusababisha vifo 19,000 huku asilimia 25 na 50 katika ukanda huo zinaweza kusababisha vifo 46,000 na 100,000.  "Wakati Afrika imeonesha ulimwengu kile kinachoweza kupatikana ikiwa tutasimama pamoja kumaliza malaria kama tishio kwa afya ya umma, maendeleo yamekwama." anasema Dk. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa Kanda wa WHO barani Afrika.  Mkakati muhimu wa kuchochea upya maendeleo kwa ni hatia ya "mzigo mkubwa kwenda matokeo makubwa" HBHI, uliochochewa mnamo mwaka 2018 na WHO na ushirikiano wa jukwaa la ulimwengu la kutokomeza malaria, RBM. Hatua inaongozwa na nchi 11 pamoja na 10 za kusini mwa Jangwa la Sahara eneo ambalo linachangia takriban asilimia 70% ya mzigo wa malaria ulimwenguni.   Tathmini ya hivi karibuni kutoka Nigeria, kwa mfano, iligundua kuwa kupitia mchanganyiko ulioboreshwa wa hatua, nchi inaweza kuzuia mamilioni ya visa vya ziada vya maambukizi na maelfu ya vifo vya ziada ifikapo mwaka 2023, ikilinganishwa na njia ya kawaida iliyozoeleka.  

WHO inasema ingawa ni mapema mno matokeo ya njia ya HBHI, ripoti hiyo imegundua kuwa vifo katika nchi 11 vilipunguzwa kutoka 263, 000 hadi 226, 000 kati ya mwaka 2018 na 2019. India iliendelea kupata faida za kushangaza, na kupunguzwa kwa maambukizi na vifo kwa asilimia 18 na asilimia 20 mtawalia kwa miaka miwili iliyopita. Hata hivyo kulikuwa na ongezeko kidogo la idadi ya maambukizi kati ya nchi zenye mzigo mkubwa, HBHI, kutoka wastani wa milioni mmambukizi 155 mnamo mwaka 2018 hadi milioni 156 mnamo mwaka 2019.  Ripoti ya mwaka huu inaangazia hatua muhimu na matukio ambayo yamesaidia kuunda mwitikio wa ulimwengu kwa ugonjwa wa malaria katika miongo ya hivi karibuni. Kuanzia miaka ya 1990, viongozi wa nchi zilizoathiriwa na malaria, wanasayansi na washirika wengine waliweka msingi wa majibu mapya ya malaria ambayo yalichangia moja ya faida kubwa kwenye uwekezaji katika afya ya ulimwengu.  Kwa mujibu wa na ripoti hii, nchi 21 zilifanikiwa kuondoa malaria katika miongo miwili iliyopita; kati ya hizi, nchi 10 zilithibitishwa rasmi kuwa hazina malaria na WHO.   Lakini nchi nyingi zilizo na mzigo mkubwa wa malaria zimekuwa zikipoteza pambano. Kulingana na makadirio ya ulimwengu ya WHO, lengo la 2020 la kupunguzwa kwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria litakosa kufikiwa kwa asilimia 37 na lengo la kupunguza vifo litakosa kwa asilimia 22. 

30 November 2020, 16:12