Rais Mteule nchini Marekani ni Joe Biden. Rais Mteule nchini Marekani ni Joe Biden. 

Maaskofu nchini Marekani wampongeza Biden:sasa ni kipindi cha umoja

Askofu Mkuu Gomez rais wa Baraza la Maaskofu Nchini Marekani kwa niaba ya maaskofu wote amempongeza rais Mteulena kwamba wanatambua kuwa wanaunganishwa na marehemu rais John F.Kennedy kama rais wa pili wa Marekani ambaye anakiri imani katoliki.Ni matarajio ya kuwa na wakati wa umoja.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Marekani, Askofu Mkuu wa Los Angeles José H. Gomez, ametoa taarifa juu ya uchaguzi wa rais kuwa kulingana na makadirio ya vyombo vya habari msingi huko Marekani vimeona ushindi wa mgombea wa Kidemokrasia ni Bwana Joe Biden. Ufuatao ni ujumbe wake:

Tunamshukuru Mungu kwa baraka ya uhuru. Watu wa Amerika wamesema katika uchaguzi huu. Sasa ni wakati wa viongozi wetu kuungana pamoja kwa roho ya umoja wa kitaifa na kujiandaa katika mazungumzo na kujitoa kwa ajili ya faida ya wote. Kama Wakatoliki na Wamarekani, vipaumbele vyetu na utume ni wazi. Tuko hapa kumfuata Yesu Kristo, kushuhudia upendo wake maishani mwetu na kujenga ufalme wake hapa duniani. Ninaamini kuwa wakati huu katika historia ya Marekani, Wakatoliki wana jukumu maalum la kuwa wapatanishi, kukuza udugu na kuaminiana, na kuombea roho mpya ya uzalendo wa kweli katika nchi yetu.

Demokrasia inahitaji kwamba sisi sote tuwe kama watu wema na wenye nidhamu. Inahitaji kwamba tuheshimu maoni na tuhudumiane kwa upendo na ustaarabu, ingawa tunaweza kutokubaliana kabisa katika mijadala yetu juu ya masuala ya sheria na sera ya umma. Kwa kufanya hivyo, tunatambua kuwa Joseph R. Biden, Jr amepata kura za kutosha kuchaguliwa kuwa rais wa 46 wa Marekani. Tunampongeza Bwana Biden na tunakubali kwamba anaungana na Rais wa Marehemu John F. Kennedy kama rais wa pili wa Marekani akikiri imani Katoliki. Tunampongeza pia Senet wa California Kamala D. Harris, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza katika historia kuchaguliwa kuwa makamu wa rais.

Kwa kuhitimisha ujumbe huo Askofu Mkuu Gomez anasema:Tumwombe Bikira Maria Mwenyeheri, mlinzi wa taifa hili kubwa, atuombee. Atusaidie kufanya kazi pamoja ili kutambua maono mazuri ya wamisionari na waanzilishi wa Marekani: taifa chini ya Mungu, mahali ambapo utakatifu wa maisha yote ya mwanadamu unatetewa, uhuru wa dhamiri na dini umehakikishiwa!

09 November 2020, 14:03