Tanzania itaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania. Tanzania itaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania.  

Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: 28 Oktoba! Huduma Bora za Kijamii!

Serikali ya Awamu ya Tano imefanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii nchini ikiwa ni pamoja utoaji elimumsingi bila ada na kuwawezesha watoto wa Kitanzania kusoma bure na bila ya ubaguzi wowote. Pia imeboresha huduma za afya na kuwawezesha wananchi kutibiwa karibu na makazi yao pamoja na miundo mbinu ya barabara!

Na Ofisi ya Waziri mkuu, - Kigoma, Tanzania.

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa Kigoma wahakikishe wanamchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwa sababu ni kiongozi shupavu, mpenda maendeleo na si mlalamishi. Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo Jumapili, Oktoba 18, 2020 alipozungumza na wakazi wa Kigoma kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Mwanga Centre wakati akimwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda na wagombea udiwani wa CCM. “Tumchague Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi tunayemfahamu na ametumikia katika nafasi ya urais kwa ufanisi mkubwa. Dkt. Magufuli ameweza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, barabara na maji katika kipindi cha muda mfupi wa miaka mitano, tumpe ridhaa ya kuongoza miaka mitano mingine ili tupate maendeleo zaidi.”

Amesema CCM ndio chama pekee chenye dhamira ya kuwaletea maendeleo na wasifanye makosa kwa kuchagua wagombea wasiokuwa na uwezo wa kuwatumikia na badala yake wachague wagombea kutoka CCM kwani ina ilani ambayo imeorodhesha miradi yote ya maendeleo itakayotekelezwa nchi nzima ikiwemo na Kigoma. Amesema wananchi wanatakiwa wamchague Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi muadilifu, mchapakazi na mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu na upendo kwa watu wa dini zote na anauwezo wa kusimamia kazi ipasavyo na ndio sababu Tanzania sasa inamaendeleo makubwa. “Oktoba 28 mwaka huu nendeni mkamchague Dkt. Magufuli.

Akizungumzia kuhusu miradi ya ujenzi wa barabara iliyotekelezwa Kigoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. bilioni 63.323 kwa ajili ya ujenzi barabara kutoka Kidahwe hadi Kasulu kwa kiwango cha lami na tayari mradi huo umekamilika na utanufaisha maeneo ya Wilaya za Kasulu na Kigoma. “Serikali imetoa shilingi bilioni 47.159 kwa ajili ya mradi wa ujenzi barabara kutoka Nyakanazi hadi Kabingo yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami, ambapo kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 86 na utanufaisha maeneo ya Wilaya ya Kakonko." Mheshimiwa Majaliwa amesema miradi mingine ya barabara za mkoa wa Kigoma ambazo zimetengewa fedha katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2020/2021 ni pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Manyovu – Kasulu – Kabingo, shilingi bilioni 372.109 zitatumika kujenga kilomita 260.6 kwa kiwango cha lami.

Awali, katika kuonyesha kuwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma wamechoshwa na upinzani wanachama 200 wa Vyama vya Upinzani wengi wao kutoka ACT Wazalendo wakiongozwa na aliyekuwa meneja wa kampeni wa Zitto Kabwe, Patrick Mzigama wamekihama chama hicho na kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na kasi kubwa ya maendeleo iliyofanywa na serikali ya CCM katika awamu ya kwanza ya  Uongozi wa Rais Dkt. Magufuli. Mzigama ametumia fursa hiyo kuwaomba radhi wakazi wa Kigoma Mjini kwa sababu yeye ndiye aliyewaongoza katika kuchagua vibaya mwaka 2015, hivyo amewaomba wabadilike na siku ya kupiga kura itakapofika wakawachague wagombea wote wa CCM. “Rais Dkt. Magufuli amejenga miradi mikubwa na maendeleo, amerudisha nidhamu kwa watumishi wa umma na wanafunzi wanasoma bure hivyo hatuna sababu ya kumchagulia mtu ambaye hawataongea lugha moja.”

Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema ni muhimu kwa Watanzania wakatumia busara kwa kumchagua mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aendelee kuliletea Taifa maendeleo kwa kuwa kazi ya urais si ya kumpa mtu ambaye hajawaji kujaribiwa na kuonesha kuwa ana uwezo wa kuongoza. “Rais Dkt John Pombe Magufuli ndiye mgombea mwenye sifa thabiti za kuliongoza Taifa hili na katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ameweza kuwatumikia Watanzania kwa uaminifu mkubwa na mnajua ni kwa namna gani ambavyo ametuletea maendeleo watu wote bila kujali vyama, makabila na uwezo wetu.”

Ameyasema hayo Jumamosi, Oktoba 10, 2020 alipokuwa anazungumza na wananchi wa Kata ya Daluni wilayani Mkinga, Tanga katika mkutano wa kampeni ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt. Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Mkinga, Dastan Kitandula na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Magufuli amefanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii nchini ikiwa ni pamoja utoaji elimumsingi bila ada na kuwawezesha watoto wa Kitanzania kusoma bure na bila ya ubaguzi wowote. Pia ameboresha huduma za afya na kuwawezesha wananchi kutibiwa karibu na makazi yao. “Maendeleo hayana chama tukamchague Dkt. Magufuli ni mchapakazi.” Amesema kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Serikali itaendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma za kijamii nchini, hivyo amewaomba Watanzania wahakikishe ifikapo Oktoba 28 mwaka huu wajitokeze kwa wingi na kwenda kuwachagua wagombea wa CCM katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imekamilisha taratibu za kuwagawia wananchi shamba la Mwele lililoko wilayani Mkinga ili waweze kulitumia kwa ajili ya shughuli za kilimo, baada ya shamba hilo kuachwa kwa muda mrefu bila ya kuendelezwa. Hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema mashamba matano ya mkonge yanayomilikiwa na Bodi ya Mkonge pamoja na mashamba mengine ambayo hayajaendelezwa Serikali imeagiza yagawiwe kwa wananchi walime mkonge ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi wa kipato. Amesema katika kipindi cha miaka mitano (2015/2016 – 2019/2020) sambamba na kuimarisha uzalishaji wa zao la mkonge ikiwa ni sehemu ya mazao ya kimkakati ya biashara Serikali imeweza kurejesha mali mbalimbali za Serikali zilizouzwa kinyume na utaratibu ikiwemo nyumba za makazi zaidi ya 30.

Mheshimiwa Majaliwa amezitaja mali nyingine zilizorejeshwa kuwa ni pamoja na jengo la Makao Makuu ya Bodi ya Mkonge Tanzania, maghala, hisa na fedha taslim (USD 78,000 na Shilingi milioni 34) zilizokuwa zimehifadhiwa zaidi ya miaka 20 kwenye akaunti ya mfilisi (Liquidator) bila ya kuwasilishwa Serikalini. Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kuimarisha mfumo wa kilimo cha mkonge kwa wakulima wadogo nchini ambapo katika mwaka 2019/2020 idadi yao iliongezeka na kufikia 7,551 ikilinganishwa na wakulima 5,828 wa mwaka 2015/2016 na itaendelea kufufua na kuendeleza mashamba yaliyokuwa yametekelezwa yakiwemo Marungu Sisal Estate (Tanga mjini) Kwamgwe Sisal Estate (Handeni). Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa mkonge nchini na kutoa ajira kwa wananchi wengi hususani kwa vijana na hivyo kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. “Mwitikio wa wananchi wa wilaya ya Mkinga  ni mkubwa katika kufufua zao la mkonge.”

19 October 2020, 11:20