Tafuta

Vatican News
UNESCO: Tarehe 8 Septemba ya Kila mwaka ni siku ya kupambana na ujinga duniani. UNESCO: Tarehe 8 Septemba ya Kila mwaka ni siku ya kupambana na ujinga duniani. 

UNESCO: Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani 8 Septemba 2020

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani kwa Mwaka 2020 imekuwa ni fursa ya kutafakari jinsi ya kutumia mbinu mpya za kufundishia na kujifunza, ili kuendeleza mchakato wa walimu kutoa elimu na mafunzo na wanafunzi kujifunza kusoma kwa juhudi na bidii katika mazingira ambayo si rafiki sana. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto kubwa ya kupata huduma hii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani “International Literacy Day” yaliasisiwa kunako mwaka 1965 katika mkutano wa Mawaziri wa Elimu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliokuwa wamekutanika huko mjini Tehran nchini Iran. Mawaziri hao wakapendekeza kuanzishwa kwa Siku ya Kupamba na Ujinga Duniani kwa kuhimiza dhana ya usomaji endelevu. Wazo hili liliibuliwa kutokana na kiwango kikubwa cha watu wasiojua kusoma na kuandika duniani. Kunako mwaka 1966, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), lilitangaza kwamba, tarehe 8 Septemba ya kila mwaka ni Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani. Lengo ni kuhamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kujizatiti katika mapambano dhidi ya baa la ujinga duniani. Hata leo hii, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bado kuna umati mkubwa wa watu wasiojua kusoma na kuandika! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 773 ambao hawakubahatika kupata elimu ya msingi.

Ikumbukwe kwamba, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Juhudi zote hizi zitaweza kufanikiwa ikiwa kama kutakuwepo na mfumo bora na imara wa elimu.

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani kwa Mwaka 2020 yamejielekeza zaidi katika mchakato wa kufundisha kusoma na kujifunza katika kipeo cha janga la Virusi vya Corona, COVID-19 na zaidi. UNESCO imejikita zaidi kupambanua dhamana na wajibu wa waalimu pamoja na mabadiliko ya ufundishaji. Hapa mkazo zaidi ni mchakato endelevu wa kufuta ujinga maishani, walengwa wakuu wakiwa ni vijana wa kizazi kipya pamoja na watu wazima. Ni katika muktadha huu, Rais Sergio Mattarella wa Italia katika ujumbe wake katika maadhimisho haya anakazia umuhimu wa kupambana kufuta ujinga, ili kuboresha hali ya maisha. Baa la ujinga ni hatari sana katika mahusiano na mafungamano ya kijamii kwani linaweza kumtenga mtu katika medani mbalimbali za maisha, lakini hasa kitamaduni na kiuchumi.

Madhara ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19 yamepelekea mabadiliko makubwa katika mchakato wa kufundisha na kujifunza kusoma, sera na mikakati ya kiuchumi na kijamii. Sehemu mbalimbali za dunia, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vilifungwa kama sehemu ya itifaki ya kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa nchi zilizoendelea katika sayansi na teknolojia ya mawasiliano, zikaanzisha kutoa elimu na mafunzo kwa njia ya mitandao ya kijamii pamoja na radio. Walimu walilazimika kufundisha huku wakiwa majumbani mwao na wanafunzi nao wakajizatiti kuhakikisha kwamba, wanapata elimu kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Changamoto hii kwa pande zote mbili, ilikuwa ni pevu sana na imefungua ukurasa mpya wa jinsi ya kufundisha na kusoma kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani kwa Mwaka 2020 imekuwa ni fursa ya kutafakari jinsi ya kutumia mbinu mpya za kufundishia na kujifunza, ili kuendeleza mchakato wa walimu kutoa elimu na mafunzo na wanafunzi kujifunza kusoma kwa juhudi na bidii katika mazingira ambayo si rafiki sana. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto kubwa kwa wale ambao hawana uwezo wa kupata na kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kumbe, mapambano dhidi ya baa la ujinga ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuhakikisha kwamba, idadi kubwa ya watu duniani inafahamu kusoma, kuandika na kuhesabu ili kutambua haki na wajibu wake.

Rais Sergio Mattarella anasema, watu wahamasike kuzama kwa busara katika ulimwengu wa kidigitali, jambo ambalo linahitaji maboresho ya uwezo wa kiuchumi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwekeza zaidi katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la ujinga duniani, kwa kuwajengea vijana na watu wazima uwezo wa kujenga jamii fungamani, yenye utulivu, amani, udugu, mshikamano na jumuishi. Ni katika muktadha huu, kinzani, chokochoko, mipasuko ya kijamii na vita; ukosefu wa haki na usawa na sanjari na uhamiaji wa shuruti vitaweza kupewa kisogo na Jumuiya ya Kimataifa.

ujinga duniani 2020

 

09 September 2020, 15:18