Tafuta

Kutazama ulimwengu kupitia katika mawingu Kutazama ulimwengu kupitia katika mawingu  

Ulimwengu:Jicho letu linatazama kupitia mawinguni!

Bunge nchini Japan limemteua Bwana Yoshihide Suga kuwa waziri wake mkuu na kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Shinzo Abe baada ya kujiuzulu kutokana na sababu za kiafya.Rais wa EU Bi.Ursula von der Leyen amezama jinsi gani Umoja wa Ulaya utakavyofufua uchumi wake baada ya janga la virusi vya corona.Uhaba wa chakula umerudi kuwa shida huko Yemen.Ndege za Tanzania zimeruhusiwa kutua Kenya.

Na Sr. Angela Rwezaula

Bunge nchini Japan limemteua Yoshihide Suga kuwa waziri wake mkuu na kujaza nafasi iliyoachwa wazi na kiongozi wa muda mrefu Shinzo Abe baada ya kujiuzulu kutokana na sababu za kiafya. Yoshihide Suga ameteuliwa na bunge hilo tarehe 16 Septemba na kumfanya kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo baada ya muda wa miaka minane wa uongozi wa Abe. Suga ambaye awali alihudumu kama waziri na msemaji mkuu wa serikali, tayari ameunda baraza la mawaziri ambalo limechanganya mawaziri wa kitambo na wale aliowateuwa sasa. Suga mwenye umri wa miaka 71 na mshirika wa karibu wa Abe, ameahidi kuendeleza mipango mingi iliyoanzishwa na Abe inayojumuisha mikakati ya kiuchumi na mageuzi ya kimfumo ikiwa ni pamoja na kuondoa sheria na kufikisha mwisho mizozo ya urasimu. Pia amesema kuwa masuala atakayoyapa kipaumbele ni mapambano dhidi ya virusi vya corona na kufufua uchumi uliodorora kutokana na janga hilo.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU) amesema matumaini ya makubaliano ya kibiashara ya Brexit yafifia kila kukicha: Tarehe 16 Septemba 2020 majira ya asubuhi Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameionya Uingereza kuwa imesalia na muda mchache kabla mwisho wa mwaka huu kufikia maelewano ya kibiashara na Umoja wa Ulaya. Amelizungumzia suala hilo la Brexit kwa kifupi huku umuhimu mkubwa ukiwa ni katika jinsi Umoja wa Ulaya (EU) utakavyofufua uchumi wake baada ya janga la virusi vya corona. Katika hotuba yake ya sera ya kila mwaka Bi von der Leyen amezungumzia kwa kirefu pia uwekezaji wa kidijitali pamoja na masuala kuhusiana na mazingira.

Umoja wa Mataifa wasema ukosefu wa chakula umerudi tena Yemen: Mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba uhaba wa chakula umerudi tena katika nchi iliyozongwa na machafuko ya Yemen. Bwana Mark Lowcock amezitaja Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Kuwait kama nchi ambazo hazijatoa msaada wowote katika kiasi cha dola bilioni 3.4 zinazohitajika mwaka huu.  Bwana Lowcock amesema Umoja wa Mataifa ulilimaliza tatizo hilo nchini Yemen mwaka jana kwa kuwa wafadhili walitoa haraka michango iliyofikia asilimia 90 ya kiwango jumla kilichoombwa. Mkuu huyo amesema maisha ya mamilioni ya watu yaliokolewa kwasababu misaada iliongezwa. Ila kwa sasa anadai kwamba ni asilimia 30 tu ya kiasi cha pesa kilichoitishwa ambacho kimetolewa na kwamba Wayemen milioni tisa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chakula, maji na matibabu

Kwa mra nyingine tena Kenya na Tanzania zimerejesheana utaratibu wa kuziruhusu ndege zao kuingia kwenye mipaka yao ya angani kufuatia miezi miwili ya sintofahamu. Serikali ya Kenya sasa imeiweka Tanzania kwenye orodha ya mataifa ambayo raia wake wanaweza kuingia ndani ya mipaka yake pasina masharti makali ya kupambana na covid 19. Kwa mantiki hii wasafiri wanaotokea Tanzania wameondolewa sharti la kuwekwa kwenye karantini ya lazima ya wiki mbili pindi wanapowasili ndani ya mipaka ya Kenya. Kwa upande wake Tanzania nayo imeiondoa marufuku ya ndege zote za Kenya kuingia ndani ya anga yake kama njia ya kuimarisha uhusiano. Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usafiri wa ndege nchini Tanzania,Hamza Johari,ndege zote zinaruhusiwa kuingia kuanzia sasa.

Waziri wa uchukuzi wa Kenya James Macharia amesema kuwa walichokifanya ni kuweka bayana sera na vigezo vya afya mintarafu abiria wanaotokea nchi tofauti. Wanayo  kila wakati orodha ya abiria wasiohitaji kwenda karantini.  Naye Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usafiri wa ndege nchini Tanzania, Hamza Johari anaelezea kilichowapelekea kuchukua msimamo huo miezi miwili iliyopita kwamba Kenya walikuwa wameomba kuja Tanzania na kwa maana hiyo wao hawakuwa na tatizo na kuwapa hiyo ruhusa. Lakini baadaye wakasikia wao wanazuia tTanzania iseiende kule kwa maana ya kufuata misingi hiyo ya usawa basi na nao wakafuta ruhusa ambayo waliwapatia.

16 September 2020, 15:02