Tafuta

Vatican News
Watanzania wameonywa kwamba, wasitumie vigezo vya udini, ukabila na itikadi ya vyama vyao na badala yake wachague viongozi watakaowaletea maendeleo yao na ya taifa katika ujumla wake. Watanzania wameonywa kwamba, wasitumie vigezo vya udini, ukabila na itikadi ya vyama vyao na badala yake wachague viongozi watakaowaletea maendeleo yao na ya taifa katika ujumla wake.  (AFP or licensors)

Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: Msitumie Udini, Ukabila na Itikadi

Watanzania wametahadharishwa kwamba, wasichague viongozi kwa kutumia vigezo vya udini, ukabila, itikadi za vyama na badala yake wachague watu watakaokuwa tayari kushirikiana nao katika kuboresha maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. Wapime sera na utekelezaji wake. Watumie haki msingi ya demokrasia kuwachagua viongozi watakaosimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kilimajaro, Tanzania

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wasichague viongozi kwa kutumia vigezo vya udini, ukabila, itikadi za vyama na badala yake wachague viongozi watakaokuwa tayari kushirikiana nao katika kuboresha maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo Jumanne, Septemba 8, 2020, wakati akimwombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Hai, Saasisha Mafuwe na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Masama Kusini kwenye uwanja wa Kwa Sadala wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro. “Ndugu zangu Watanzania, ndugu zangu wanaHai na wanaKilimanjaro mnatambua uwezo na uelewa mkubwa alionao Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli wa kutambua na kuona nini Watanzania wanahitaji, nawaomba siku ya kupiga kura itakapofika tujitokeze kwa wingi bila kujali itikadi zetu tumpigie kura nyingi ili akaendeleze miradi ya maendeleo aliyoianzisha.”

Amesema wakati umefika kwa wakazi wa Hai kuchagua kiongozi mwenye kujali na kutambua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi na kamwe wasikubali kupiga kura kwa ushabiki au kufuata mkumbo. “Mchague Rais Dkt. Magufuli kwa nafasi ya urais na Saasisha nafasi ya ubunge pamoja na wagombea udiwani wote wa CCM.” Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Magufuli ni kiongozi anayetokana na Chama Cha Mapinduzi chenye utaratibu wa kuratibu miradi yote inayotakiwa kutekelezwa katika maeneo yote nchini kupitia ilani ya uchaguzi na kina mipango mizuri ya kuboresha maendeleo ya wananchi. Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kupitia mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa sh. bilioni 520 kutoka Machame hadi Arusha.

Visima vimekamilika kuchimbwa na usambazaji wa mabomba umeanza. “Katika mradi huu wananchi wa Hai walio katika kilomita 12 kushoto na kulia kando kando ya maeneo ambayo bomba la maji litapita tutahakikisha Mamlaka ya maji AWSA inaweka matanki kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi katika ukanda wa chini.” Amesema sh. bilioni 3.3 zimetumika kukamilisha mradi wa ujenzi na upanuzi wa skimu ya maji LOSAA – KIA. Maeneo yanayonufaika ni pamoja na kata ya Masama Magharibi, Masama Kati, Masama Kusini na kata ya KIA. Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. milioni 844 zimetumika kukamilisha ukarabati na ujenzi wa mifereji ya maji katika skimu za Nsanya, Musa Mwinjanga na Kikavu Chini. “Skimu ya Uroke – Bomang’ombe imekamilika na inahudumia maeneo ya Machame Uroki, Kwa Sadala, Kware, Romu na Mji wa Hai. Kwa upande wao, wananchi walisema watahakikisha wanawachagua wagombea wa CCM kwa sababu katika kipindi cha miaka 15 walichokuwa wakichagua viongozi wa upinzani hakuna kitu chochote walichokifanya cha maendeleo katika wilaya yao.

Miongoni mwa wananchi hao Betha Massawe amesema Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwe kufufua usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha usafiri ambao ulisimama kwa miaka 30 jambo ambalo hadi leo haamini anaona kama ndoto. Mkazi mwingine wa Hai, David Kiseyi amesema katika uchaguzi wa mwaka huu wamejipanga kuchagua viongozi kutoka Chama Cha Mapinduzi kwa sababu wamekuwa wakiwachagua viongozi wa upinzani bila ya faida yoyote. “Rais Dkt Magufuli ameonesha upendo mkubwa kwetu kwa kutuletea miradi ya maendeleo kwetu sasa tunakwenda kuacha ushabiki na tutachagua viongozi watakaotuletea maendeleo. Watu wa Hai tuache ushabiki tuchague maendeleo.” "Huyu Mbunge ametufanya sisi kama watoto anakuja tunampa kura kwa ahadi zake nyingi na anapopata hutumuoni tena anakimbilia Dar es salaam na Dodoma utafikiri wananchi wa huko ndio wamemchagua sasa hatupo tayari kudanganywa na maneno ya uongo ni bora akaanza kukusanya virago vyake" alisema Halima Mushi mkazi wa Machame.

Wakati huo huo, Waziri wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana kila sababu ya kumchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020 kwa sababu ni kiongozi makini, shupavu, mbunifu na mwenye uwezo wa kusimamia vizuri rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wote. Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wake, Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini na yamewanufaisha Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro bila ya ubaguzi wa aina yoyote. Ameyasema hayo Jumanne, Septemba 8, 2020 alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Godwin Mollel na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Matadi kata ya Ndemet wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro.

Amesema Watanzania wanatakiwa wamchague Rais Dkt. Magufuli ili aweze kuwaongoza katika kusimamia vizuri matumizi ya rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini Tanzania. Amesema Tanzania ni nchi tajiri yenye uwezo wa kuwaletea wananchi wake maendeleo bila ya utegemezi, hivyo wachague viongozi makini kwa manufaa ya Taifa. “WanaSiha wote nimekuja hapa kwenu leo nina kazi moja tu ya kumuombea kura mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM, Rais Dkt. Magufuli ambaye ni kiongozi imara, mzalendo na mchapakazi, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Mollel na wagombea udiwani wote wa CCM katika wilaya hii. Ikifika siku ya kupiga kura tuhakikishe tunawachagua.” Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa lazima wananchi waamini kwamba uongozi unatoka kwa Mwenyezi Mungu na Rais Dkt. Magufuli ameletwa na Mwenyezi Mungu, hivyo amewaomba wampe ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano mingine ili aendeleze kazi za maendeleo alizozianza.

“Nawasihi inapofika siku ya kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu tunapotumia haki ya msingi ya kidemokrasia, tukamchague Rais Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi anayejali maslahi ya Watanzania wote na ni kiongozi anayeweza kujua nchi inawakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara ambao kila mmoja anatakiwa afanye shughuli zake kwa uhuru bila ya kusumbuliwa.” Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wa Siha kuwa Serikali itayarudisha mashamba yote ya Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) yanayomilikiwa kinyemela na watu wachache kwa manufaa yao binafsi “Kuna watu wamejimilikisha mahekari ya mashamba ya KNCU ambayo ni mali zenu, nawahakikishia tutawanyang’anya na kuyarudisha kwenu ili atakayelima alime, atakayefuga afuge”

Amesema KNCU ni mali ya wananchi (wanaushirika) na kwamba Serikali imefanya kazi kubwa ya kurudisha hadhi ya ushirika katika kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani waliohusika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo na itaendelea kurejesha mali zote kwa wananchi ili wafanyie shughuli za maendeleo. Akizungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme wilayani Siha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 60 vilivyopo Siha vijiji vyenye umeme ni 58 na viwili tu ndio havina umeme na kwamba navyo vitaunganishwa umeme, amewaomba wakazi wake waendelee kuwa na subira. Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Rombo. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu. Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.

 

09 September 2020, 14:53