Serikali ya Tanzania imepania kukuza sekta ya utalii sanjari na kuongeza fursa za ajira kwa vijana. Itaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya wananchi wake wote. Serikali ya Tanzania imepania kukuza sekta ya utalii sanjari na kuongeza fursa za ajira kwa vijana. Itaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya wananchi wake wote. 

Tanzania: Maendeleo Endelevu! Utalii na Ajira kwa Vijana!

Serikali ya Tanzania imeandaa mazingira mazuri ya kuwawezesha Watanzania kujikwamua kiuchumi wakiwemo wafanyabiashara wadogo. Serikali pia itaendelea kuimarisha sekta ya utalii nchini Tanzania kwa kusimamia ipasavyo mikakati ya kukuza vivutio ili kuhakikisha Watanzania wengi wakiwemo wakazi wa jiji la Arusha hususani vijana wananufaika kwa kupata ajira na kuongeza kipato!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Kilimanjaro.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeandaa mazingira mazuri ya kuwawezesha Watanzania kujikwamua kiuchumi wakiwemo wafanyabiashara wadogo. Ameyasema hayo Jumapili, Septemba 6, 2020 alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Kirima Juu wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akimwombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi na wagombea udiwani. “Nimekuja hapa kuwaomba sana kura yenu ya ndio kwa Rais Dkt. Magufuli kwani mkiwa sehemu ya Watanzania mnafahamu kazi kubwa ya kupeleka maendeleo aliyoifanya nchi nzima bila ya ubaguzi wa aina yoyote, tuhakikishe tunampigia kura nyingi ili akaendeleze kazi aliyoianza.” Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya CCM imejenga miradi mingi ya kimkakati ikiwemo ya afya, maji, elimu, umeme, barabara, viwanja vya ndege kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya Watanzania.

Serikali imetengeneza fursa katika maeneo mbalimbali zilizowezesha wananchi kujikwamua kiuchumi. Akizungumzia kuhusu miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali katika halmashauri ya wilaya ya Moshi, Waziri Mkuu amesema jumla ya sh. bilioni 2.1 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Uru Kyaseni, Uru Kusini na Okaoni pamoja na upanuzi na ukarabati wa zahanati za Kahe, Kilema, Kisao, Chemchemi, Mowo, Kitowo na Kituo cha Afya Shimbwe. Pia sh bilioni 12.2 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Kuhusu elimumsingi bila ada, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa bilioni sh. 4.8 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maafisa elimu kata na walimu wakuu katika shule za msingi 252 kwenye halmashauri ya wilaya ya Moshi. “Serikali imetoa shilingi bilioni 10.2 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule katika shule za sekondari 59 kwenye halmashauri ya wilaya ya Moshi.” Amesema shilingi bilioni 1.6 zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 18, matundu ya vyoo 109, bwalo moja, nyumba sita za walimu na jengo moja la utawala na ununuzi wa mashine ya kudurufu mitihani katika shule za msingi Maweni, Mahoma, Ngaroni na Saghana.

Pia, Waziri Mkuu amesema sh. bilioni 7.3 zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 26, matundu vyoo 45, maabara 14, mabweni sita na ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari za Ashira, Umbwe, Sakayo Mosha na Muungano, Kisarika, Shimbwe na Kimochi. Amesema Serikali imetoa sh bilioni 5.3 kwa ajili ya miradi mikubwa ya maji ya Lyamungo-Umbwe, Njiapanda, Tella Mande, Mamba-Mruma, Shimbi Mashariki, Leto na Ngareni. Pia imetoa sh. bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi mingine ya visima virefu ya Mweka, Mamba Kusini, Mang’ana, Kyaronga, Kiwaya na Rudugai, Kaloleni, Mkashilingi, Vyanzo vya Kipure, Nikodemo na Mrusungu. Aidha Mheshimiwa Majaliwa alitumia jukwaa hilo kuvunja makundi ya wanachama wa CCM waliogombea nafasi ya ubunge na kuwaeleza wananchi kuwa Chama Cha Mapinduzi kinautaratibu wakati wa mchakato wa ndani, ambapo baada ya uteuzi wa chama wanaCCM wote huungana na kuwa kitu kimoja.

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya utalii nchini Tanzania kwa kusimamia ipasavyo mikakati ya kukuza vivutio ili kuhakikisha Watanzania wengi wakiwemo wakazi wa jiji la Arusha hususani vijana wananufaika kwa kupata ajira. Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeweza kupata mafanikio mbalimbali katika sekta ya utalii yakiwemo kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia 1,510,151 mwaka 2019, ambapo amewaomba wananchi wandelee kuiamini Serikali yao. Aliyasema hayo Jumamosi, Septemba 5, 2020 alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Relini jijini Arusha baada ya kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge jimbo la Arusha, Mrisho Gambo na wagombea udiwani wa CCM.

“Sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi hususani kwa vijana kwa sababu vijana wengi wameajiriwa na kujiajiri kupitia sekta ya madini. Serikali inawahakikisha kwamba itaendelea kuboresha mazingira ili kuweza kuvutia watalii wengi zaidi kuja nchini.” Alisema kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika sekta hiyo mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini Tanzania yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 1,901.95 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 2,612.99 mwaka 2019. Waziri Mkuu alisema mafanikio yote hayo yanatokana na uongozi thabiti na makini wa Rais Dkt. Magufuli, hivyo amewaomba wana Arusha na Watanzania kwa ujumla kumchagua tena ili aweze kutekeleza mikakati mingine ya kuongeza wigo wa utalii aliyoianzisha nchini.

“Ndugu wanaarusha na Watanzania wote sina shaka kwamba mtakubaliana na ombi langu la kuwataka tumchague tena Rais Dkt. Magufuli kwa sababu mnapenda maendeleo na kwa Tanzania mtu atakayewaletea maendeleo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli tujitokeze kwa wingi kumpigia kura.” Akizungumzia kuhusu Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 alisema inaielekeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kukuza wigo wa bidhaa na mazao ya utalii. Ilani imeelekeza Serikali ihakikishe inaongeza idadi ya watalii na kufikisha watalii 5,000,000 kwa mwaka ifikapo 2025 na kuongeza mapato kutoka Dola za Kimarekani bilioni 2.6 mwaka 2020 hadi Dola za Kimarekani bilioni 6.0 mwaka 2025. Pia kushirikisha sekta binafsi na kuandaa wataalam wa ukarimu na kuwatambua wataalam wenye ujuzi na weledi unaohitajika katika utoaji wa huduma za utalii ili kukuza sekta hiyo na kuongeza ajira kwa wananchi na pato la Taifa kwa kubuni na kutekeleza mikakati ya kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi na umma zishiriki kikamilifu katika uwekezaji wa utalii.

Kadhalika, Waziri mkuu alizungumzia kuhusu suala la bima ya afya, ambapo alisema Serikali iweka mikakati Madhubuti inayowawezesha wananchi kutibiwa ikiwa ni pamoja na kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo wananchi wanachangia kiasi kidogo na Serikali inawaongeza na kuwawezesha kutibiwa bure wao na familia zao. Pia, Waziri Mkuu aliongeza kuwa utaratibu mwingine ni kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ni maalumu kwa ajili ya watumishi wa umma kuchangia kiasi kidogo kupitia mishahara yao na mpango huo unawawezesha kutibiwa bure, hivyo hakuna tatizo la huduma ya bima ya afya nchini. Amewataka wananchi wasikubali kupotoshwa na waendelee kuiamini Serikali yao. Aidha, katika Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 CCM imeilekeza Serikali kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwamo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili kufikia lengo la serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote.

 

08 September 2020, 09:56