Tafuta

Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa familia ya Mungu nchini Lebanon kufuatia mlipuko mkubwa ambap umesababisha maafa makubwa sana. Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa familia ya Mungu nchini Lebanon kufuatia mlipuko mkubwa ambap umesababisha maafa makubwa sana. 

Mlipuko wa Beirut, Lebanon: Mshikamano wa Upendo Kimataifa!

Kuyumba kwa uchumi nchini Lebanon kutokana na vikwazo vya kiuchumi, athari za janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na mlipuko huu, ni kati ya mambo yatakayoendelea kusababisha mateso na hali ngumu ya maisha ya wananchi wa Lebanon. Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wameonesha mshikamano wa hali na mali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Sergio Mattarella wa Italia ni kati ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waliotuma salam za rambirambi kufuatia mlipuko mkubwa uliojitokeza kwenye viunga vya bandari ya Beirut na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Rais Sergio Mattarella katika ujumbe aliomwandikia Rais Michel Aoun wa Lebanon, anasema, amesikitishwa sana na taarifa za mlipuko uliotokea tarehe 4 Agosti 2020 huko Beirut. Kwa niaba ya wananchi wa Italia, anapenda kuchukua fursa hii kuonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano wa upendo kwa watu wote walioguswa na kutikiswa na mlipuko huo. Familia ya Mungu nchini Italia inapenda kutoa salam zake za rambirambi kutokana na msiba huu mkubwa kwa taifa la Lebanon. Wananchi wa Italia wanapenda kuungana na wenzao wa Lebanon, ili kuwafariji wale wote waliofikwa na msiba huu, kwa matumaini kwamba, majeruhi wataweza kupatiwa huduma makini na hatimaye, kupona na kurejea tena nyumbani mwao ili kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Wakati huo huo, Shirika la “Save the Children” linasema kwamba, kutokana na mlipuko huo mkubwa kuna hatari kwamba, watoto wakashindwa kupata huduma ya matibabu kutokana na hospitali nyingi kuzidiwa na idadi ya wagonjwa. Bandari ya Beirut inayohifadhi sehemu kubwa ya nafaka imeharibiwa sana. Kumbe, kuna hatari kwamba, watu wengi wakaanza kukumbwa na baa la njaa na magonjwa, ikiwa kama hatua za dharura hazitaweza kuchukuliwa mapema. Kuyumba kwa uchumi nchini Lebanon kutokana na vikwazo vya kiuchumi, athari za janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na mlipuko huu, ni kati ya mambo yatakayoendelea kusababisha mateso na hali ngumu ya maisha ya wananchi wa Lebanon.

Kwa upande wake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limebainisha kwamba, zaidi ya watoto 80, 000 hawana makazi ya kudumu kutokana na mlipuko uliojitokeza huko Beirut. Kwa sasa UNICEF inaendelea kuhakikisha kwamba, walau watoto wanapata chakula, maji na hifadhi kwani watoto wengi wameathirika vibaya sana kutokana na mlipuko huo. Kuna zahanati 12 kwa ajili ya watoto wadogo zimeharibiwa vibaya sana, kiasi hata cha kuathiri utoaji wa chanjo kwa watoto wa dogo. Makonteina 10 ya dawa na vifaa tiba yameharibiwa na kwamba, katika kipindi cha masaa kadhaa yaliyopita, idadi ya watu walioambukizwa kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 imeongezeka na kufikia wagonjwa 464.

Maafa Beirut

 

07 August 2020, 13:03