Tafuta

Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu Nchini Italia: Rimini 20202: Ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kuna haja ya kuwekeza zaidi miongoni mwa vijana kwa njia ya elimu, ujuzi, maarifa, maadili na nidhamu. Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu Nchini Italia: Rimini 20202: Ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kuna haja ya kuwekeza zaidi miongoni mwa vijana kwa njia ya elimu, ujuzi, maarifa, maadili na nidhamu. 

Mkutano wa Rimini 2020: Wekezeni Miongoni Mwa Vijana Inalipa!

Serikali zinapaswa kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya uwezo, ujuzi na maarifa ili kupambana na mazingira yao. Kanuni maadili na utu wema ni mambo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Utawala wa sheria pamoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni amana na utajiri mkubwa katika ujenzi wa uchumi fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake XLI, yaani Mwaka wa 41. Mkutano huu kuanzia tarehe 18 -23 Agosti 2020, unaongozwa na kauli mbiu: “Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu”. Huu ni mkutano unaopembua pamoja na mambo mengine, changamoto zinazoendelea kujitokeza baada ya janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kumbe, huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale watu waliovunjika na kupondeka moyo, kwa kubainisha sera na mikakati ya uchumi fungamani. Gonjwa la Corona, COVID-19 limesababisha utengano mkubwa, changamoto na mwaliko wa kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Siasa inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu kitaifa na hata katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Rais Sergio Mattarella wa Italia katika ujumbe wake kwenye mkutano huu aliomwandikia Bernhard Scholz anasema, janga la homa kali ya mapafu inayosabishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, limekuwa ni sababu ya vifo na mateso ya watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Janga hili limekuwa na madhara makubwa kiuchumi na kijamii, kiasi cha kutoa changamoto mpya ya maendeleo fungamani ya binadamu yanayoheshimu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu pia ni mwaliko wa kuvuka ubaguzi wa kijamii, kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kama chachu muhimu ya ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa! Rais Sergio Mattarella anaendelea kufafanua kwamba, kauli mbiu: “Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu”, ilikuwa tayari imekwisha kuchaguliwa hata kabla ya kuibuka kwa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Lakini ni ujumbe muhimu sana katika mchakato wa shughuli za ujenzi wa mfumo mpya wa uchumi unaotakiwa kutekelezwa kwa vitendo bila kuchelewa hata kidogo. Lengo liwe ni kukuza na kudumisha miradi itakayosaidia kukuza uchumi fungamani, binadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza.Ni changamoto ya kukuza na kudumisha ukweli, uwazi, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kuondokana na baadhi ya watu na mataifa kutaka kujifungia katika ubinafsi wao, hali ambayo itapelekea kuteleza na hatimaye kuanguka kwa uchumi wa Jumuiya ya Kimataifa. Tangu kuanzishwa kwake, Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini, umekuwa ukitoa kipaumbele cha pekee kwa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya, EU, kama dira na mwongozo wa kuangalia masilahi yake mapana. Umoja wa Jumuiya ya Ulaya, EU umeweza kujibu kwa ufanisi mkubwa changamoto ambazo zimesababishwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa sasa ni wakati wa Italia, kujielekeza katika ujenzi na mchakato wa kufufua uchumi.

Italia imeonesha na kushuhudia tunu msingi za maisha ya kimaadili na kiutu; kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani na mshikamano wa kidugu, kama sehemu ya mbinu mkakati wa ujenzi wa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya mpya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wake. Rais Sergio Mattarella wa Italia anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, watu wote wanawajibika katika mchakato wa maboresho ya sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni, kwa kutambua kwamba, watu wote wanawajibika, kila mtu kadiri ya dhamana na nafasi yake katika jamii. Taasisi mbali mbali na jamii katika ujumla wake, zinapaswa kutekeleza dhamana na wajibu huu kwa kutumia nguvu zake za kiuchumi sanjari na amana na utajiri wake wa kijamii, ili kujenga na kuimarisha Italia na maendeleo fungamani ya vijana wa kizazi kipya.

Kwa upande wake, Mario Draghi, Rais Mstaafu wa Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya “The European Central Bank” katika hotuba yake kwenye mkutano wa Rimini kwa Mwaka 2020 amegusia kuhusu: Athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, uliojitokeza takribani miaka 12 iliyopita na kupelekea kuporomoka kwa uzalishaji wa fursa za ajira; kwa kukwama kwa uwekezaji na vitega uchumi na matokeo yake uwezo wa watu kiuchumi ukashuka na wengi wao wakajikuta wakitumbukia katika umaskini wa hali na kipato. Waathirika wakubwa zaidi ni vijana wa kizazi kipya ambao hawana matumaini makubwa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Bila amani na utulivu wa ndani, si rahisi sana kuweza kufanya mageuzi makubwa ndani ya jamii. Mario Draghi, Rais Mstaafu wa Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya anakaza kusema, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limepeleka watu wengi kuwekwa karantini, uchumi kuporomoka, ukosefu wa fursa za ajira; taasisi za elimu kufungwa, athari kubwa katika sekta ya afya pamoja na deni la ndani kuongezeka maradufu.

Gonjwa la Virusi vya Corona, COVID-19 bado litaendelea kuiandama Jumuiya ya Kimataifa, kumbe kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwa sasa na kwa siku za usoni. Sheria, kanuni, taratibu na nidhamu ya matumizi ya rasilimali fedha lazima zizingatiwe na wote, kwa kukuza na kudumisha demokrasia na uchumi shirikishi na fungamani. Sera na mikakati ya ukuaji wa uchumi lazima izingatie: ukweli na uwazi; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, utu, heshima, haki na mahitaji msingi ya binadamu yakipewa kipaumbele cha kwanza. Kuna haja ya kuwekeza katika familia kwa kuzijengea uwezo wa kiuchumi ili kukuza mchakato wa ongezeko la ulaji kitaifa na kimataifa. Ni muda wa kuwekeza zaidi katika ulimwengu wa kidigitali, ili kuongeza muda wa kazi hata wafanyakazi wanapokuwa majumbani mwao. Serikali zinapaswa kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya uwezo, ujuzi na maarifa ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao.

Kanuni maadili na utu wema ni mambo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Utawala wa sheria pamoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni amana na utajiri mkubwa katika ujenzi wa uchumi fungamani duniani. Kimsingi, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa karibu na vijana, kwa kuwajengea uwezo wa kiakili, kiuchumi, kimaadili na kiutu kama msingi wa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Rimini 2020

 

20 August 2020, 07:02