Tafuta

Vatican News
Serikali ya Zimbabwe imetoa shutuma nzito dhidi ya Kanisa Katoliki na viongozi wake kufuatia Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe kuandika Waraka wa Kichungaji Kuhusu hali halisi nchini humo. Serikali ya Zimbabwe imetoa shutuma nzito dhidi ya Kanisa Katoliki na viongozi wake kufuatia Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe kuandika Waraka wa Kichungaji Kuhusu hali halisi nchini humo.  (AFP or licensors)

Shutuma za Serikali ya Zimbabwe Dhidi ya Kanisa Katoliki

Serikali ya Zimbabwe inamtaja Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu kuwa na mawazo mabaya kwa ajili ya Zimbabwe na kwamba, Kanisa Katoliki linataka kuigawa Zimbabwe vipande vipande na hatimaye, kuitumbukiza katika mauaji ya kimbari. Serikali ya Zimbabwe inapinga na kulaani vikali Waraka wa Kichungaji uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, Agosti 2020.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Serikali ya Zimbabwe kupitia kwa Waziri wa habari na huduma ya mawasiliano Bi Monica Mutsvangwa, Jumamosi, tarehe 15 Agosti 2020 imetoa shutuma kali dhidi ya Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe, lakini kwa namna ya pekee kabisa dhidi ya Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu wa Jimbo kuu la Harare nchini Zimbabwe, ambaye ndiye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe. Serikali ya Zimbabwe inamtaja Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu kuwa na mawazo mabaya kwa ajili ya Zimbabwe na kwamba, Kanisa Katoliki linataka kuigawa Zimbabwe vipande vipande na hatimaye, kuitumbukiza katika mauaji ya kimbari kama ilivyojitokeza nchini Rwanda kunako mwaka 1994. Serikali ya Zimbabwe inapinga na kulaani vikali Waraka wa Kichungaji uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe tarehe 14 Agosti 2020 katika mkesha wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho.

Serikali ina laani mawazo potofu yanayotaka kuchochea ukabila utakao lisambaratisha taifa la Zimbabwe na hatimaye kulitumbukiza katika mauaji ya kimbari kama ilivyotokea mwaka 1994, mauaji ambayo yalichochewa na Askofu mkuu Arthanase Seromba ambaye kwa sasa anakabiliwa na shutuma za mauaji ya kimbari yaliyopelekea zaidi ya watu laki nane kupoteza maisha, wengi wao wakiwa ni Watutsi. Serikali ya Zimbabwe inasema, Kanisa linapaswa kuomba msamaha kwa kujihusisha na mauaji haya. Huu ndio mwelekeo ambao Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu unaofanyiwa kazi katika Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, yaani kuitumbukiza Zimbabwe katika mauaji ya kimbari! Serikali inamshutumu Askofu mkuu Ndlovu kwa kuchochea ukabila na ubaguzi dhidi ya umati mkubwa wa wananchi wa Zimbabwe kwa kujidai kwamba, anataka kusimama kidete kulinda haki na demokrasia sanjari na kutaka kuling’arisha Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe.

Serikali inawataja baadhi ya Maaskofu waliokuwa wanajihusisha na sera za ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini na jinsi ambavyo, waliishia pabaya kwenye miaka 1965. Ni kweli kwamba, Kanisa Katoliki kwa miaka ya nyuma lilichangia sana katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zimbabwe, lakini “Gukurahundi” ni mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Jeshi la Serikali dhidi ya wananchi wa kabila la Wandebele kati ya mwaka 1983 hadi mwanzoni mwa mwaka 1987 ni kutaka kudhohofisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Hata hivyo, Serikali ya Zimbabwe inakiri kwamba, mauaji ya kimbari katika kipindi hiki cha kihistoria, yalihitaji uponyaji, ili amani na umoja wa kitaifa viweze kushamiri tena na makubaliano ya kitaifa yakafikiwa kunako mwaka 1987. Vita vya kupigania uhuru ni sehemu ya mchakato wa mataifa mengi, kama ilivyokuwa hata kwa Marekani  kati ya mwaka 1861 hadi mwaka 1865. Je, maandamano yaliyoshindwa kunako tarehe 31 Julai 2020 bado yataendelezwa?

Serikali ya Zimbabwe inasema, Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe ni dalili za woga mtupu na kuwataka waamini kuipuuzia kwa sababu italitumbukiza taifa katika ukabila, umajimbo na ubaguzi wa rangi. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni mapambano ya kimataifa. Katika taharuki hii, Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu akaitisha maandamano makubwa dhidi ya Serikali na hivyo kwenda kinyume kabisa na mwaliko wa Papa Francisko anayetaka Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika misingi ya amani na utulivu, ili viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona. Rais Emmerson Dambudzo Mnangagwa wa Zimbabwe atawashughulikia wote wanaotaka kuhatarisha afya, ustawi na maendeleo na wananchi wa Zimbabwe.

Serikali Zimbabwe

 

18 August 2020, 08:17