Tafuta

Tanzania inalenga la kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi chakula na nafaka kutoka tani 250, 000 za sasa hadi kufikia tani 501, 000 kwa mwaka. Tanzania inalenga la kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi chakula na nafaka kutoka tani 250, 000 za sasa hadi kufikia tani 501, 000 kwa mwaka.  

Tanzania inapania kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao yake!

Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa vihenge vya kisasa (silos) sita (6) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na maghala mawili (2) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 katika kanda ya Makambako unaogharimu shilingi Bilioni 26.5. Watanzania wametakiwa kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea ili kuwasaidia wakulima.

Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Kilimo, -Mufindi, Tanzania.

Wakala wa Ujenzi (TBA) wametakiwa kufanya kazi ya kumsimamia kwa karibu mkandarasi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa na maghala ili akamilishe kazi mapema kabla ya mwisho wa mwaka huu wa 2020 ili nchi iweze kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao yake. Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa vihenge vya kisasa (silos)  sita (6) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na maghala mawili (2)  yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000  katika kanda ya Makambako  unaogharimu shilingi Bilioni 26.5  chini ya kampuni ya Feerum toka nchini Poland. Maagizo hayo ya serikali yametolewa tarehe 12.07.2020 na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipofanya ziara katika ofisi za NFRA kanda ya Makambako mkoa wa Njombe ambapo ameeleza kusikitishwa kwake na kasi ndogo ya kampuni ya Feerum kutekeleza mradi huo “Ikifika Desemba 31, 2020 nitakuja hapa Makambako, nataka TBA mnikabidhi kazi yangu ya maghala na vihenge ikiwa imekamilika.Hatuwezi kukubali mradi huu ushindwe kukamilika wakati serikali imeshatoa fedha nyingi” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu alisema kuwa hajafurahishwa na kasi ndogo ya mkandarasi iliyofikia asimilia 58 licha ya muda wake wa mkataba kuongezeka. Akiwa eneo la mradi Katibu Mkuu Kusaya ameagiza msimamizi wa mradi huo TBA kupitia Mhandisi Mkazi wake Pedon Mshobozi kupata mpango kazi wa mkandarasi kuuwakilisha wizarani ili apate kujua endapo maghala na vihenge vitakamilika kwa wakati. Kusaya alisema mradi huo ni sehemu ya miradi ya kimkakati ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli hivyo hatapenda kuona mkandarasi mzembe anavumiliwa bali hatua za kisheria ikibidi zichukuliwe kwa mujibu wa mkataba kumwondosha. “Serikali imeweka lengo la kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi chakula na nafaka kutoka tani 250,000 za sasa hadi kufikia tani 501,000 mradi huu utakapokamilika nchini mwaka huu kwenye vituo nane NFRA” alisisitiza Kusaya

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa NFRA kanda ya Makambako Frank Felix alisema katika msimu wa 2020/2021 wamepangiwa kununua tani 25,000 za mahindi na mpunga toka kwa wakulima. Hadi kufika sasa amesema wakala umenunua jumla ya tani 4.258.986 kati hizo tani 2,933.174 za mahindi na tani 1,325.782 za mpunga na ametoa wito kwa wakulima kupeleka mazao yao kwenye vituo ili yanunuliwe. Akizungumzia akiba iliyopo kituoni hapo Frank alisema wakala katika maghala yake ya Makambako una akiba ya tani 11,896.63 za nafaka  Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya ametoa onyo kali kwa mameneja wa NFRA kanda zote nane kuacha mara moja kufanya kazi kwa maslahi binafsi. Amesema anazo taarifa kuwa baadhi ya watendaji hao wa serikali wanajihusisha kuhujumu mali kwa maslahi binafsi kinyume na taratibu na sheria za utumishi wa umma. “Nachukia sana mtumishi anayetumia vibaya fedha za umma.Sina huruma na watumishi wa aina hii.Sitasita kuwafukuza kazi wabadhirifu “alisema Kusaya Ameitaka menejimenti ya wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula kujituma zaidi na kuweka mpango wa kuwezesha kujiendesha kibiashara ili kutumia nafasi ya maghala na vihenge vipya kutunza mazao mengi zaidi ya sasa.

Wakati huo huo, wawekezaji wa ndani ya nchi wamehamasishwa kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kusaidia upatikanaji wa mbolea bora na yenye gharama nafuu kwa wakulima. Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa wito huo tarehe 11.07.2020 wakati wa ziara yake ya kikazi  wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa kujionea hali ya uzalishaji mazao ya pareto na chai. Kusaya alisema kuwa hali ya uzalishaji mazao hayo umekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka kutokana na malalamiko ya wakulima kushindwa kumudu gharama ya bei kubwa ya pembejeo na mbolea. “Nitafurahi zaidi nikisikia watanzania wanaanzisha uwekezaji katika viwanda vya mbolea ili tusaidie wakulima wetu kwani kwa sasa katika baadhi ya maeneo wakulima wengi wanashindwa kununua mbolea mfuko wa kilo 50 kwa shilingi 90,000” alisema Kusaya

Akiwa kijiji cha Mkonge wilaya ya Mufindi Katibu Mkuu huyo alipokea malalamiko ya wakulima wadogo wa chai kuwa chai yao inakataliwa na wenye viwanda kwa madai kuwa ina ubora mdogo uliosababishwa na kutumia mbolea yenye ubora mdogo. Wakulima hao wa chama cha ushirika cha wakulima wa chai Mkonge wanadai kukopeshwa mbolea na kampuni ya Uniliver ya Mufindi ambayo pia ni mmoja wa wanunuzi wanaokataa kununua majani mabichi ya wakulima hao na kusababisha hasara kwa wakulima. “Chai tulipeleka mwaka huu kiwandani Uniliver tukaambiwa haina ubora kisha wakaimwaga kwa kuwa tulitumia mbolea ya Minjingu isiyo na ubora, hii hasara nani atatulipa “alisema Jimson Sigala mkulima wa chai. Katibu Mkuu aliongeza kusema wizara ya kilimo inahitaji mkulima atumie mbolea itakayoongeza tija katika uzalishaji hivyo amewasihi watanzania kujitokeza kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda ndani ya nchi na kuwa serikali ya Awamu ya tano itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji. Kwa mujibu wa Wakala wa Udhibiti wa Mbolea  (TFRA) hali ya upatikanaji wa mbolea nchini Tanzania imeongezeka kutoka tani 302,482 mwaka 2015/2016 hadi tani 604,978 mwaka 2019/2020 hata hivyo mahitaji bado ni makubwa sana kwani mbolea nyingi inaagizwa nje ya nchi na hivyo kuwa na bei kubwa.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya amewasihi wakulima wa chai Mufindi na kote nchini kutumia Kituo cha Utafiti wa zao la Chai ( TRIT) kupata huduma za ushauri ili waongeze tija katika uzalishaji wa zao la chai nchini. “Wakulima nendeni kwenye kituo chetu cha Utafiti TRIT kupata elimu juu ya kilimo cha chai ikiwemo kupata huduma ya upimaji afya ya udongo kujua aina ya virutubishi na mbolea inayotakiwa kuongeza uzalishaji na kuwezesha mkulima anufaike na kilimo” Kusaya alisisitiza. Wakulima wadogo wa chai Mufindi waliomba serikali iwasaidie kupata bei nzuri ya chai kwani bei ya sasa ni ndogo na haiendani na gharama za uzalishaji. Akizungumza kwa niaba ya wakulima Abeid Mhongole mkazi wa Luhunga Mufindi alisema bei ya shilingi 314 kwa kilo moja ya majani ya chai haileti manufaa kwa wakulima na zaidi inawakatisha tamaa kuendelea kuzalisha zao la chai.

Akijibu kero hiyo Katibu Mkuu Kusaya alisema atakutana na Katibu Mkuu wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe hivi karibuni kujadili namna ya kupata ufumbuzi wa malalamiko ya bei ya zao la chai na kuwa ikibidi wasaidie kupatikana kiwanda cha chai kwa wakulima wadogo. Aidha Kusaya aliwataka viongozi wa chama hicho cha ushirika kuwasilisha maombi yao ya kupta mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili waweze kupata uwezo wa kununua mbolea bora moja kwa moja toka kwenye viwanda badala ya kupitia mawakala. “Tukiwa na bei nzuri ya zao la chai, tutawavutia vijana wengi kulima na kuondoa utegemezi wa wazee kuendeleza kuzalisha zao hili muhimu kwa uchumi wa nchi” alisema Kusaya.

13 July 2020, 08:47