Rais Mtsaafu wa Awamu ya Tatu Benjamini William Mkapa: 1938-2020: Mzee wa sera za ukweli na uwazi, amefariki dunia tarehe 24 Julai 2020 huko Jijini Dar es Salaam. Rais Mtsaafu wa Awamu ya Tatu Benjamini William Mkapa: 1938-2020: Mzee wa sera za ukweli na uwazi, amefariki dunia tarehe 24 Julai 2020 huko Jijini Dar es Salaam. 

Rais Mstaafu Ben William Mkapa: 1938-2020: Ukweli na Uwazi!

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa alizaliwa tarehe 12 Novemba 1938 huko Ndanda, karibu na Masasi, Mtwara, Kusini mwa Tanzania. Aliwaongoza watanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia tarehe 23 Novemba 1995 hadi tarehe 21 Desemba 2005 alipong’atuka kutoka madarakani. Wakati wote huo alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Watanzania wamepokea taarifa za msiba wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa aliyekuwa na umri wa miaka 81 kwa majonzi na simanzi kubwa. Taarifa hii imetangazwa moja kwa moja na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania kupitia televisheni kwa kusema kwamba, Mzee William Benjamin Mkapa amefariki dunia katika usiku wa kuamkia tarehe 24 Julai 2020 akiwa Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Rais Magufuli amewataka watanzania wote kuwa watulivu, wamoja na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Mzee Benjamin William Mkapa. Kwa muda wa siku saba, Tanzania itaendelea kumwombolezea Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Rais Magufuli katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, ataendelea kumkumbuka Mzee Mkapa kama mzalendo kwa nchi yake; kiongozi aliyeonesha uchaji wa Mungu. Alikuwa ni mchapakazi na utendaji wake wa kutukuka katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania. Kwa hakika, Tanzania imepoteza nguzo imara na thabiti.

Wachunguzi wa mambo wanasema, Rais Mstaafu Ben Mkapa ni kiongozi aliyesimama imara kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, akakazia utawala bora. Alitekeleza sera ya ubinafshaji wa Mashirika ya Umma nchini Tanzania, ili kuongeza tija na uzalishaji, ingawa lengo hili halikuweza kufikiwa kikamilifu na hivyo kuacha maswali yenye ukakasi. Alihimiza uchumi wa soko huria na kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania kuwekeza zaidi ili kukuza uchumi wa Tanzania. Sera na Mikakati ya Uchumi na Maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Tatu iliungwa mkono na Benki ya Dunia, WB., pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hali iliyopelekea Tanzania kufutiwa madeni yake ya nje. Ununuzi wa ndege ya Rais ulioigharimu Tanzania kiasi cha £ milioni 15 pamoja na ununuzi wa Rada kwa ajili ya matumizi ya kijeshi kwa kiasi cha £ milioni 30 pamoja na “sakata” la Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, ni kati ya mambo yaliyoacha doa katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya uongozi wa Rais Benjamin William Mkapa.

Nguvu ya safu ya Marais wastaafu Tanzania kwa sasa imepungua. Wazee hawa walipokuwa wakikaa na kuamua, Tanzania mambo yakanyooka. Mzee Ben Mkapa, vita amevipiga, mwendo ameumaliza, sasa apumzike kwa amani. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apokee kazi zake njema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Amsamehe mapungufu yake ya kibinadamu na hatimaye, aweze kumpokea miongoni mwa wateule wake huko mbinguni! Mzee wa ukweli na uwazi, nenda kapumzike Baba! Itakumbukwa kwamba, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa alizaliwa tarehe 12 Novemba 1938 huko Ndanda, karibu na Masasi, Mtwara, Kusini mwa Tanzania. Aliwaongoza watanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia tarehe 23 Novemba 1995 hadi tarehe 21 Desemba 2005 alipong’atuka kutoka madarakani. Wakati wote huo alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi, CCM. Mzee Ben kama wengi walivyozoea kumwita, alijipatia shahada yake ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda na baadaye alijiendeleza zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Colombia na huko akajipatia shahada ya uzamili katika taaluma ya mahusiano ya jamii.

Enzi ya maisha yake alibahatika kupata dhamana ya kuwaongoza watanzania katika ngazi mbali mbali. Amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada mwaka 1982 na hatimaye Marekani kati ya mwaka 1983 hadi mwaka 1984. Aliwahi kuteuliwa na Baba Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 1977 hadi mwaka 1980 wakati wa hali ngumu ya uchumi nchini Tanzania. Aliteuliwa tena kati ya mwaka 1984 hadi mwaka 1990. Kati ya Mwaka 1990 hadi mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji. Kati ya Mwaka 1992 hadi mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Mzee Ben Mkapa alikuwa ni mwanadiplomasia na mwandishi wa habari aliyebobea. Wengi “walizima fegi kwa umombo wake”. Wachunguzi wa mambo wanasema, Rais Mkapa ni kati ya watanzania wachache sana waliokuwa na uwezo wa kutawala na kumudu lugha ya Kiingereza kwa ufasaha, kiasi kwamba, hata alipokuwa anatoa hotuba zake kwa Jumuiya ya Kimataifa, wengi walivutwa kumsikiliza! Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini William Mkapa, Mzee wa Ukweli na Uwazi, hatunaye tena! Yaani sipati picha! Baba Mkapa Nenda kapumzike kwa amani!

Rais Ben Mkapa
24 July 2020, 12:41