Marekani: Marekani: 

Marekani:Rais Trump amekataa visa kwa wanafunzi wa kigeni!

Rais Donald Trump amekataa visa kwa wanafunzi wa kigeni ambao kozi zao zimefanyika kwenye mtandao tangu mwanzoni mwa mwaka mpya wa shule kutokana na janga la virusi corona.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Serikali ya Marekani chini ya uongozi wa rais Donald Trump imefutilia mbali mipango yake ya kuwarudisha makwao wanafunzi wa kigeni ambao masomo yao yanaendelea kupitia mitandao kutokana na mlipuko wa virusi vya corona. Mabadiliko haya yanajiri wiki moja baada ya kutangazwa kwa sera hiyo. Taasisi ya technolojia ya Masachussets (MIT) na chuo kikuu cha Havard kiliishtaki serikali kufuatia mpango huo. Jaji wa wilaya Allison Burroughs mjini Masachussets amesema kwamba pande zote mbili zimeafikiana.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, linaandika kuwa  Makubaliano hayo yanarudisha sera ilioidhinishwa mwezi Machi, kufuatia mlipuko wa virusi vya corona ambayo inaruhusu wanafunzi wa kigeni kuhudhuria masomo yao kupitia mtandao na kubaki nchini humo kwa kutumia visa ya masomo. Idadi kubwa ya wanafunzi wa kigeni husafiri kuelekea nchini Marekani kila mwaka na huwapatia vyuo vikuu nchini humo pato kubwa. Kwa mfano Chuo Kikuu Harvard kilitangaza hivi majuzi kwamba kutokana na hofu ya kusambaa kwa virusi vya corona, masomo yatatolewa kupitia mitandaoni wakati wanafunzi watakaporudi shule. Aidha Taasisi ya technolojia ya Masachussets MIT taasisi nyengine za masomo imesema kwamba itaendelea kutoa masomo kupitia mtandao.

Wanafunzi wa kigeni waliambiwa wiki iliyopita kwamba hawataruhusiwa kubaki nchini Marekani wakati huu wa msimu wa vuli la sivyo wafanye kozi ya masomo ya kibinafsi. Wale ambao walirudi katika mataifa yao wakati muhula ulipokwisha mwezi Machi huku mlipuko wa virusi vya  corona ukizidi kuongezeka, waliambiwa kwamba hawataruhusiwa kurudi iwapo masomo yao yatakuwa yakiendelea kupitia mtandaoni. Shirika la uhamiaji na forodha nchini humo ICE lilikuwa limesema kwamba raia watarudishwa makwao iwapo hawataafikia sheria hiyo. Mipango ya kubadilishana wanafunzi ambayo husimamiwa na Shirika la uhamiaji na forodha (ICE) ilikuwa imewaruhusu wanafunzi wa kigeni kuendelea na masomo yao ya mtandao wakati wa msimu wa joto na baridi mwaka 2020 huku wakiendelea kubaki nchini humo. Lakini kunako mwezi huu Julai kitengo hicho kimesema kwamba wanafunzi wa kigeni ambao watafeli kufanya masomo ya kujifunza binafsi watakabiliwa na sheria hizo za uhamiaji.

Hata hivyo siku mbili baadaye, Chuo Kikuu cha Harvard na Taasisi ya technolojia ya Masachussets (MIT) ziliwasilisha kesi mahakamani zikitaka kubadili msimamo huo wa serikali, wakidai kuwa agizo hilo ni ukiukwaji wa sheria usiostahiki na matumizi mabaya ya busara. Na makumi ya vyuo vingine pia yameunga mkono kesi hiyo. Kwa mujibu wa vyuo 59 vinavyounga mkono kesi hiyo “kinachowapatia shinikizo ni kwamba hakuna uhusiano wowote na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanajihusisha na kozi kamili ya masomo au kulinda uaminifu wa mpango wa visa ya wanafunzi. Badala yake, kusudi lake ni kuhamasisha shule kufunguliwa tena.”

Rais Donald Trump amekuwa akiwasukuma wanafunzi wa vyuo vikuu na wale wa shule kurudi madarasani katika muhula mpya. Mawazo yake ni kwamba kufunguliwa kwa shule kutaashiria kuimarika kwa uchumi kufuatia miezi kadhaa ya machafuko, hatua ambayo inaweza kumsaidia labda katika kampeni yake ya kuchaguliwa kwa kipindi kipya cha miaka minne kama rais mwezi Novemba kwa mujibu wa wachambuzi. Hata hivyo walimu wengi wana wasiwasi kuhusu ustawi wa wanafunzi na wanataka kuendelea kutekeleza sheria ya kutokaribiana huku mlipuko huo ukiendelea. Sera hiyo inawaathiri wamiliki wa visa za F-1 na M-1 visas, ambazo ni za wanafunzi wa kitaaluma na wa ufundi. Idara ya masuala ya kigeni ilitoa Visa 388,839 aina za F na 9,518 aina ya M katika mwaka wa 2019 kulingana na takwimu za shirika hilo la uhamiaji. Kwa mujibu wa idara ya biashara nchini Marekani, wanafunzi wa kimataifa walichangia $45bn (£36bn) katika uchumi wa taifa hilo 2018.

Hata hivyo Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji limesema wahamiaji katika sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakinyanyapaliwa kama waeneza virusi vya janga la corona au COVID-19 suala ambalo ni kinyume na hali halisi. Akizungumzia jambo hilo mjini Geneva Uswisi wiki hii mkurugenzi mkuu wa IOM Bwana Antonio Vitorino amesema wakati mamilioni ya watu wakisalia majumbani katika harakati za kupambana na COVID-19 wahamiaji wamekuwa kazini katika sekta mbalimbali muhimu kwa jamii hususan za afya na huduma za viwandani. Hivyo amesema suala hili “ni moja ya masuala yanayoitiwa wasiwasi, kwa shirika hili na kwamba katika maeneo mbalimbali janga hili linatumika kuwanyanyapaa wahamiaji kama wasambaza wa virusi. Lakini ukweli ni kwamba wahamiaji na watu wenye asili ya uhamiaji wako msitari wa mbele katika vita dhidi ya ugonjwa huu, katika nchi kama Uingereza, Marekani na Canada takribani asilimia 30 hadi 40 wale walio msitari wa mbele katika huduma za afya ni wahamiaji au watu wenye asili ya uhamiaji.” Ameongeza kuwa hata Uswisi na Italia bado sehemu kubwa ya wahudumu wa afya karibu asilimia 50 ni watu wenye asili ya uhamiaji au wahamiaji. Na ni muhimu kutambua kwamba katika nchi nyingi kila kitu kimefungwa lakini maisha yanaendelea katika sekta muhimu na huduma za msingi zinapatikana, hilo ni asante kwa wahamiaji. Hizo ndizo sekta ambazo wahamiaji wamebeba jukumu muhimu katika huduma za kufikisha bidhaa, huduma za usafirishaji, za masoko ya chakula na nina uhakika kwamba nyote mmeshuhudia jukumu linalofanywa na wahamiaji katika kipindi ambacho wote tumesalia majumbani tukiogopa virusi lakini wao walikuwa hapo wakifanya kazi kwa faida ya jamii nzima.” Kwa mantiki hiyo ameitaka jumuiya ya kimataifa kutambua kwamba mchango wa wahamiji ni mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na katika nchi nyingi kwani bila wahamiaji zitataabika.

15 July 2020, 12:42