Tafuta

Benki ya Dunia, tarehe 1 Julai 2020 imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati, hatua ambayo imefikiwa miaka mitano kabla ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Benki ya Dunia, tarehe 1 Julai 2020 imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati, hatua ambayo imefikiwa miaka mitano kabla ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. 

Benki ya Dunia: Tanzania na Uchumi wa Kipato cha Kati!

Mataifa yenye kipato cha kati ya dola 1,006 hadi dola 3,955 kwa mtu mmoja hutajwa kuwa Mataifa yenye kipato cha kati, lakini yaliyo na uchumi mdogo huku yale yenye kipato cha kati ya dola 3,956 hadi dola 12,235 yakidaiwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati yenye uchumi unaoimarika. Muhimu: Ni kuzidisha juhudi na maarifa katika uzalishaji na utoaji wa huduma ili kuongeza kasi ya uchumi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli wa Tanzania inasema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyobuni ajira kwa Watanzania wengi ni kati ya vitu ambavyo viliivutia Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kama taifa lenye kipato cha kati. Mbali na uongozi thabiti wa Rais John Pombe Magufuli katika kudhibiti matumizi ya fedha ya umma pamoja na kupambana na wale wanaotaka kufuja fedha ya umma, taifa la Tanzania limeimarika kiviwanda. Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuanzisha zaidi ya viwanda elfu nane katika kipindi cha miaka mitano. Benki ya Dunia, WB, tarehe 1 Julai 2020 imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati. Rais Magufuli alitumia fursa hii kuwashukuru watanzania kwa hatua hii waliyoifikia. Vigezo vinaonesha kwamba, Mataifa yenye kipato cha kati ya dola 1,006 hadi dola 3,955 kwa mtu mmoja hutajwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati, lakini yaliyo na uchumi mdogo huku yale yenye kipato cha kati ya dola 3,956 hadi dola 12,235 yakidaiwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati yenye uchumi unaoimarika.

Kinachotakiwa sasa ni kuzidisha juhudi na maarifa katika uzalishaji na utoaji wa huduma ili kasi ya ukuaji wa uchumi usishuke bali izidi kuongezeka maradufu. Kuna haja ya kuendelea kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo, “Kilimo kwanza” kwa kuongeza tija sambamba na kuongeza usindikaji wa mazao ya kilimo hii ikiwa ni katika jitihada za kuondokana na kilimo cha kujikimu na kujikita zaidi katika kilimo cha kibiashara chenye kulenga mahitaji ya soko la ndani na nje.  Bado kuna haja ya kuboresha uwekezaji katika rasilimali watu hususani kuboresha upatikaji wa huduma bora za afya, elimu bora pamoja na maji safi na salama kama njia ya uhakika ya kuondokana na umaskini ifikapo mwaka 2025. Tangu mwaka 2000, Tanzania imekuwa ikitekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa (Development Vision 2025) inayolenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Dira hii imelenga kubadili uchumi wa Tanzania kutoka kutegemea sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, lakini yenye tija ndogo na kuwa taifa lenye kutegemea zaidi uchumi wa viwanda na hasa viwanda vyenye kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kumudu ushindani wa soko la kimataifa. Tanzania imekuwa ikitekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa kupitia mikakati mbali mbali ikiwa ni pamoja na: Mkakati wa Kwanza na wa Pili wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini nchini Tanzania. Hii ni mikakati ambayo ilifahamika zaidi kwa jina la MKUKUTA na Mipango ya Miaka mitano mitano ya Maendeleo ya Taifa ambapo kwa sasa taifa la Tanzania linatekeleza mpango wa pili kwa kipindi cha miaka ya 2016/17 – 2020/21.

Wakati huo huo, Waziri  mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Watazania waendelee kufanya kazi kwa bidii ili nchi iendelee kukua kiuchumi na kufikia uchumi wa juu kwa kuwa tayari imekuwa ya uchumi wa kati. “Kama ni mkulima lima kwa bidii, mtumishi wa umma fanya kazi kwa bidii, mlio viwandani fanyeni kazi na mamalishe nanyi pikeni sana ili mzunguko wa fedha uweze kuendelea kuwa mkubwa nchini.” Alitoa kauli hiyo Jumamosi, Julai 04, 2020 alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mpanda kwa gharama ya sh bilioni 2.8. Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani pato la mwananchi kwa mwaka lilikuwa dogo na baada ya miaka mitano limeongezeka na kufikia sh, milioni mbili. Alisema ongezeko hilo la pato la mwananchi kwa mwaka limeliwezesha Taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya matarajio yaliyopendekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania ililenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini nchi imewezeka kufikia uchumi wa kati 2020. Baada ya kuzindua jengo hilo, Waziri Mkuu alitembelea kijiji cha Kasekese kilichoko wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambapo alizindua msimu wa ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka huu wa 2020. Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kurudisha ushirika ili uweze kuwa na tija kwa wakulima, aliwataka viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wawasaidie wanachama wao.  Vilevile, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Kilimo nchini Tanzania wawaelimishe viongozi wa vyama vya ushirika namna bora ya uendeshaji wa vyama hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia kwa kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia katika maeneo yao na kuwapa elimu itakayowawezesha kujiongezea tija.

Na taarifa iliyotolewa Jijini Washington DC nchini Marekani hivi karibuni imesema kuwa Bodi Tendaji ya Shirika la Fedha Duniani, IMF, imefikia uamuzi huo na fedha hizo ambazo Tanzania ilipaswa kulipa sasa zitatoka katika fuko la IMF la kudhibiti majanga na kuweka unafuu, CCRT. IMF inasema deni hilo lilipaswa kulipwa kati ya sasa na tarehe 13 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020, na kwamba nyongeza ya msamaha  wa deni linalotakiwa kulipwa kati ya Oktoba 14 mwaka 2020 hadi Aprili 13 mwaka 2022 itategemea uwepo wa fedha kwenye fuko hilo. IMF inasema kuwa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limedhoofisha matarajio ya ukuaji uchumi wa Tanzania ambapo sasa Tanzania inakabiliwa na kuporomoka kwa mapato yake kwenye sekta ya utalii, shinikizo kwenye bajeti na kuanguka kwa ukuaji wa pato la ndani la taifa, GDP, kutoka asilimia 6& hadi asilimia 4% katika kipindi hiki cha Mwaka wa fedha 2020-2021.

Mara baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo wa msamaha wa deni, Naibu Mkurugenzi Mwendeshaji wa IMF na Mwenyekiti wa Bodi ya IMF Bwana Tao Zhang amesema, “COVID-19 imekuwa na madhara makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania na kuongeza mahitaji ya kipekee katika ulipaji wa salio. Mamlaka zimetekeleza mikakati ya kudhibiti gonjwa hilo na kuepusha kukwama kwa uchumi. Wamesalia macho kwenye hatari za kusambaa kwa maambukizi na ukosefu wa uhakika utokanao na janga hilo.” Ni katika muktadha huu amesema fedha ambazo zingetakiwa kulipwa kwenye deni, sasa zitatumika kusaidia kukabiliana na janga kubwa la Corona, COVID-19. “Mamlaka za Tanzania zimejizatiti kutumia rasilimali za ziada kwa malengo yaliyopangwa na kwa uwazi ikiwemo kufanyika kwa ukaguzi wa fedha zinazoelekezwa kwenye kukabili COVID-19,”  amesema Bwana Tao. Tanzania inakuwa nchi ya 27 kunufaika na msamaha huo wa madeni kupitia mfuko wa CCRT wa IMF kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya COVID-19, ambapo jumla ya fedha zilizotolewa kuziba pengo la malipo kwa nchi hizo ni dola milioni 243. Mataifa mengine yaliyopata msamaha kupitia mfuko huo ni pamoja na Rwanda, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Afghanistan.

Tanzania: Uchumi wa Kati

 

05 July 2020, 13:18