Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameitaka TAKUKURU kujifunga kibwebwe ili kupambana na rushwa na ufisadi katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 nchini Tanzania. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameitaka TAKUKURU kujifunga kibwebwe ili kupambana na rushwa na ufisadi katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 nchini Tanzania. 

Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: TAKUKURU: Kupambana na Rushwa!

Serikali imewaagiza Makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini Tanzania kuhakikisha kwamba, wanawakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu. Wote wahakikishe kwamba hakuna vitendo vya rushwa katika uchaguzi na yeyote ambaye anajihusisha na rushwa asiachwe!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Lindi, Tanzania.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameongoza wanachama 314 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Ruangwa, Lindi katika kujaza fomu za kumdhamini Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aweze kuteuliwa kugombea tena nafasi ya urais. Idadi hiyo inafanya jumla ya wanachama waliojitokeza kumdhamini Rais Dkt. Magufuli katika wilaya hiyo kufikia 2,565 baada ya wanachama wengine 2,251 kujaza fomu hizo jana (Jumamosi, Juni 20, 2020) na kumdhamini kiongozi huyo. Waziri Mkuu ameongoza wanachama hao wa CCM Jumapili, Juni 21, 2020 katika ofisi za CCM wilayani Ruangwa. Amewasihi wananchi hao waendelee kuwa na imani na Rais Dkt. Magufuli pamoja na Serikali anayoiongoza. “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza ahadi zote alizoziahidi ikiwemo ya kuwatumikia Watanzania wote hasa wanyonge. Amewatumikia Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa na hata za kidini. Nawapongeza wana CCM wenzangu mliojitokeza kumdhamini rais wetu.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Kitendo mlichokifanya leo kinaonyesha shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye wakati wote ameonesha mapenzi makubwa kwetu pamoja na Watanzania wote kwa ujumla.” Amesema kwa sasa wilaya ya Ruangwa imepata mabadiliko makubwa kimaendeleo ambayo hapo awali hayakuwepo kama nishati ya umeme, maji ambayo kwa sasa kila kijiji kina kisima, shule za msingi katika kila kijiji na sekondari kwenye kata zote pamoja na barabara za lami katika mitaa ya mji wa Ruangwa.” Haya yote ni Dkt. Mgufuli.” Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi, Fadhili Juma amesema wanaCCM wa mkoa huo wapo bega kwa bega na Rais Dkt. Magufuli na kwamba watahakikisha anapata kura nyingi katika uchaguzi ujao. Awali, Waziri Mkuu aliwashukuru WanaRuangwa wote kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano ambao ulimuwezesha kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo kwa ufanisi mkubwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imewaagiza Makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini Tanzania kuhakikisha kwamba, wanawakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu. “Watu wamezoea vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, Serikali tumeagiza kwa kamati za ulinzi na usalama zishirikiane kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya rushwa katika uchaguzi na yeyote ambaye anajihusisha na rushwa asiachwe.” Alitoa kauli hiyo Jumamosi, Juni 20, 2020) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea akiwa njiani kuelekea wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi. Waziri Mkuu alisema kitendo cha kutoa na kupokea rushwa ni kosa, hivyo viongozi hao wa TAKUKURU nchini Tanzania hawana budi kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo. Vilevile, Waziri Mkuu amewataka Makamanda wa TAKUKURU katika wilaya zote nchini wahakikishe wanawakamata watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa wakiwemo na wapambe ambao ndio wachochezi wa vitendo hivyo.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu unakuwa huru na wa haki, hivyo kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi wanaowahitaji na si kwa msukumo wa rushwa. Katika hotuba yake aliyoisoma Juni 15, 2020 bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi wazingatie katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi. Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla waendelee kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa Uchaguzi Mkuu. Mheshimiwa Majaliwa alikwenda Zanzibar ambako alishiriki katika tukio la Kuvunja Baraza la Wawakilishi liliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwenye ukumbi wa Baraza hilo. Pia tukio hilo lilihudhuliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai.

22 June 2020, 08:25