Tafuta

2014.11.25 Papa Francisko katika ziara ya Bunge la Umoja wa nchi za Ulaya jijini,Strasburg. 2014.11.25 Papa Francisko katika ziara ya Bunge la Umoja wa nchi za Ulaya jijini,Strasburg. 

Siku ya mabunge duniani:Utambuzi wa chombo hiki kama kipaza sauti za wananchi!

Baraza la Umoja wa Mataifa lilipitisha tarehe 30 Juni kuwa siku ya mabunge duniani kwa kutambua mchango wa chombo hicho katika mipango na mikakati ya kitaifa katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika ngazi za kitaifa na kimataifa.Bunge ni kama kipaza sauti za wananchi na ambalo linatoa ushawishi wa uundaji wa sera.

Tarehe  30 Juni  ya kila mwaka ni siku ya wabunge duniani iliyopitishwa tarehe 22 Mei 2018, kuwa kilele cha siku hii ya wabunge. Siku hii  tarehe inakumbusha mwaka 1889, kuanzishwa kwa chama cha mabunge duniani, (IPU). Katika kilele cha kumbu kumbu hii,  Umoja wa Mataifa unasema ni siku muhimu ya kutambua mchango muhimu wa mabunge katika kupaza sauti za wananchi na pia kushawishi uundaji wa sera.

Katika ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anasema kuwa “mimi nimewahi kuwa mbunge, na ninaguswa sana na wajibu na heshima ya kuwakilisha wananchi na kukidhi matarajio yao. Mabunge yana jukumu mahsusi katika kusìendeleza  haki za binadamu na kuendeleza maendeleo endelevu.”

Katibu Mkuu amesema kuwa hivi sasa ni kuliko wakati wowote kwenye  zama za janga la la virusi vya Corona au COVID-19, jamii inakumbushwa majukumu hayo muhimu, kwa maana hiyo amesema, “Kadri dunia inapokabiliana na janga hili, tunaona umuhimu wa kipekee wa uwepo wa mifumo thabiti ya afya, mitandao ya uhakika na bora ya hifadhi ya jamii na ukuaji uchumi wa kutosheleza unaochechemua ajira zenye hadhi.”

Aidha Bwana Guterres  kwa kutazama mbali zaidi amesema kuwa, “tunaona pia wale walio hatarini zadi kwenye jamii zetu kama vile wanawake wakibeba mzigo mkubwa. Ukosefu wa usawa, unyanyapaa, mgawanyiko na utete katika dunia yetu vimeongezeka maradufu mbele ya macho yetu.” Kwa kuzingatia mazingira ya sasa, amesisitiza kuwa “ni lazima tuchukue hatua pamoja kujenga upya, mustakabali wenye usawa zaidi, wenye mnepo na wenye manufaa kwa wote. Nasihi mabunge ya nchi kokote pale kutekeleza kwa kina majukumu yao na kuendeleza mbele hatua endelevu na jumuishi.”

Katibu Mkuu amesema hilo linapaswa kujumuisha na kuratibiwa pamoja na mashirika ya kiraia, ili kuwa na mipango ya kitaifa dhidi ya ubaguzi wa rangi. Kwa kuongezea amesema “tukumbuke kuwa hakuna taifa ambalo linaweza kufanikiwa peke yake. Hebu na tutumie fursa hii kujenga upya mustakabali wetu wa pamoja, tuchukue hatua za kijasiri na kubwa kwa tabianchi na kuweka haki za binadamu na utu kuwa kitovu cha kazi yetu.” Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio lake namba A/72/278  la tarehe 22 Mei 2018, lilipitisha Juni 30 kuwa siku ya mabunge duniani kwa kutambua mchango wa chombo hicho katika mipango na mikakati ya kitaifa katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

 

30 June 2020, 12:23